Ujana ni mtihani. Ujana ni kama mtindo unapita haraka. Ujana ni moshi, ukienda haurudi. Hakuna mzee yeyote ambaye ana utajiri wa kununua tena siku zake za ujana. Kipindi cha ujana ni kimoja, ingawa baadhi ya wazee wanaitwa vijana wa zamani.

Umri wa uzeeni unategemea ujana. Umri wa kati unategemea ujana. Ukweli huu unabainishwa na methali ya Wahaya: “Mvi anakula vilivyolimwa na nywele nyeusi.”  Hivyo, ujana ni mtihani. Ujana ni umri mzuri sana wa kuwa tajiri sana na umri mzuri sana wa kuwa maskini sana.

Hivyo ujana ni mtihani.  Ujana ni mtihani kwa vile una fursa nyingi zinazopotea. “Kosa la ujana ni kuamini akili inachukua nafasi ya uzoefu, na kosa la uzee ni kuamini uzoefu unachukua nafasi ya akili,” alisema Lyman Bryson.

Akili na uzoefu vinakamilishana. Ujana unaishi kwa kutumaini uzee unaishi kwa kukumbuka. Ujana una kesho, uzee una jana. Ujana una nguvu, uzee una uzoefu.

Vijana hawapaswi kudhalilishwa wala kudharauliwa. Kuna methali ya Kiafrika isemayo: “Muogope ambaye bado anakua.” Kijana unayemdharau leo anaweza kuwa mtu mashuhuri na wa maana kesho.

Mwanafunzi aliyeitwa Noah Webster (mtunzi wa Webster’s Dictionary) alijulikana kwa kuwa mchafu. Siku moja mwalimu wake alimwambia: “Ukionekana na mikono michafu nitakutoa darasani.”

Webster alionekana akiwa na mikono michafu tena. Mwalimu alimwambia: “Nyosha mkono wako.” Webster alitemea mate kiganja chake na kujipangusa kwenye suruali yake akitaka kusafisha mkono wake kabla ya kuunyosha.

Mwalimu alitazama sinema hii akihisi kichefuchefu. Mwalimu alimwambia Webster: “Kama unaweza kunionyesha mkono mchafu zaidi ya kwako darasani nitakuachia bila adhabu.”

Muda mfupi baada ya kuombwa mkono mchafu zaidi ya wakwake, Webster alimuonyesha mkono wake mwingine ambao ulikuwa mchafu zaidi. Ni huyu Webster ambaye alitokea kuwa msomi wa hali ya juu na kutunga kamusi ya Kiingereza – Kiingereza. Usimdharau kijana haujui kesho atakuwa nani. “Vijana wanahitaji watu wa kuwaiga na si wakosoaji,” alisema John Wooden.

Ujana ni umri wa kuthubutu. Kijana ana mbawa za kumwezesha kupaa na kwenda mbali, mbawa hizo ni mbawa za matumaini na ujasiri. Ukiwa kijana kila kitu kinawezekana.

“Karibu kila kitu kikubwa kimefanywa na vijana,” alisema Benjamin Disraeli.  Isaac Newton aliweka katika maneno kanuni ya uvutano akiwa na umri wa miaka 24. Hugo Grotius, Baba wa Sheria za Kimataifa alikuwa mtaalamu wa lugha ya Kilatini akiwa na umri wa miaka tisa.

Alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu akiwa na umri wa miaka kumi na miwili, mwanasheria akiwa na umri wa miaka kumi na mitano, mwanahistoria akiwa na umri wa miaka ishirini na mwanasheria wa kimataifa akiwa na umri wa miaka ishirini na moja.

Edius Katamugora, aliandika kitabu chake cha kwanza kinachoitwa ‘Barabara ya Mafanikio’ akiwa na umri wa miaka ishirini. Cyrus McCormick aligundua mashine ya kuvuna akiwa na umri wa miaka ishirini na mitatu.

Kwame Nkrumah, Rais wa kwanza wa Ghana, alikuwa mwalimu mkuu wa shule akiwa na umri wa miaka 22. Charles Dickens aliandika kazi inayoitwa ‘Oliver Twist’ akiwa na umri wa miaka ishirini na mitano.

Natamani ningejua ukweli huu kabla ya kufikisha miaka kumi na minane. Ukweli kuwa chochote bila chochote haupati chochote. Ukweli kuwa ili kupanda lazima kushuka. Ukweli kuwa fursa inaonekana ikiwa ndogo wakati inakuja na kubwa wakati inatoweka.

Ukweli kuwa apandaye haba atavuna haba. Ukweli kuwa ukipanda upepo utavuna tufani. Ukweli kuwa kutumikia ni kutawala. Ukweli kuwa muda ni mali. Ukweli kuwa Roma haikujengwa kwa siku moja. Ukweli kuwa afya ni mtaji. Ukweli kuwa muda ni mali. Ni jambo muhimu ukweli huu vijana wakaufanyia kazi.

Please follow and like us:
Pin Share