Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kusimamia weledi, kanuni na taratibu zilizowekwa kwenye kila sekta ya utumishi wa umma. Aidha, pale patakapojitokeza uvunjifu wa maadili na miiko iliyowekwa, hatua stahiki za kinidhamu zitachukuliwa.

Pia, Majaliwa ametoa wito kwa walimu wakuu na wakuu wa shule kutumia walimu wa malezi, ushauri na unasihi pamoja na Viongozi wa Dini katika kuwarekebisha watoto na kuwajenga kimaadili ili kuepukana na matumizi ya adhabu ikiwemo viboko.

Ameyasema hayo leo Februari 2, 2023 wakati akitoa taarifa kuhusu masuala ya ukatili shuleni katika Kikao cha Tatu cha Mkutano wa 10 wa Bunge, Bungeni jijini Dodoma. Taarifa imelenga kufafanua changamoto ya nidhamu na malezi ya wanafunzi na adhabu zinazotolewa shuleni.

Waziri Mkuu amesema shule zimekuwa kioo cha malezi ya watoto katika kusimamia na kujenga nidhamu katika jamii na jukumu hilo limekuwa likitekelezwa na walimu na wazazi kwa lengo la kuwajenga watoto hasa wanapokwenda kinyume na nidhamu, ambapo viboko hutumika kama moja ya adhabu ya kuwarejesha katika mstari.

Amesema ili kuhakikisha adhabu hiyo inaleta tija na kufikia malengo yaliyokusudiwa, Serikali iliweka utaratibu maalumu wa namna ya kusimamia adhabu hiyo bila kuathiri afya na saikolojia ya mtoto. Licha ya kuwepo kwa mifumo hiyo, bado wapo baadhi ya watu wamekuwa wakifanya ukiukaji wa sheria na taratibu hizo na kusababisha madhara makubwa kwa jamii.

“Hivi karibuni tumeshuhudia kupitia vyombo vya habari, vitendo vya adhabu kali dhidi ya wanafunzi kwa baadhi ya shule zetu. Adhabu hizo zimefanywa na baadhi ya walimu walio na mafunzo ya kutosha ya malezi, mahali pengine Mwalimu Mkuu mwenye dhamana ya kuongoza shule, ambaye anafahamu utaratibu wa utoaji wa adhabu shuleni”.

Amesema Serikali haitofumbia macho na wala kukubaliana na aina hiyo ya adhabu kali na kwamba tayari imechukua hatua za kinidhamu kwa wahusika. “Nitumie fursa hii adhimu, kukumbusha mamlaka za Elimu nchini kuhakikisha kuwa utoaji wa adhabu shuleni unazingatia Waraka Na. 24 wa Mwaka 2002 wa Wizara ya Elimu na Utamaduni”.

Waziri Mkuu amesema waraka huo umeelekeza kwamba adhabu itazingatia ukubwa wa kosa, jinsia na afya ya mtoto na isizidi viboko vinne kwa wakati mmoja; mwanafunzi wa kike atapewa adhabu ya viboko mkononi na mwalimu wa kike tu isipokuwa kama shule haina mwalimu wa kike.

Pia adhabu ya viboko inapotolewa iorodheshwe katika kitabu kilichotengwa kwa kusudi hili ikiwa ni pamoja na jina la mwanafunzi aliyepewa adhabu, kosa alilotenda, idadi ya viboko na jina la mwalimu aliyetoa adhabu hiyo; Mwalimu Mkuu atie saini katika kitabu kila mara adhabu inapotolewa na mwanafunzi akikataa adhabu hiyo atasimamishwa shule.

Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa waraka umeweka bayana kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mwalimu yeyote atakayekiuka utaratibu wa adhabu ya viboko. “Hapa nisisitize kuwa hatua kali zitachukuliwa hata kwa walimu wakuu au wakuu wa shule wanaokiuka utaratibu uliowekwa”.

“Licha ya changamoto zilizojitokeza na hatua za awali zilizochukuliwa, naomba kusisitiza kuwa bado shule zetu ni mahali salama kwa malezi ya watoto wetu na walimu wetu wameendelea kufanya kazi nzuri kwa bidii na kujituma. Changamoto ya nidhamu mbaya ya wanafunzi si jukumu la walimu pekee kulisimamia”.

Hivyo, Waziri Mkuu amesema wazazi na jamii kwa ujumla wanapaswa kushirikiana kwa karibu na walimu katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ya kuwafundisha, kuwalea, kuwaongoza na kuwaendeleza wanafunzi kimwili, kiakili na kiroho kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria, mila, desturi na tamaduni za Kitanzania.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo walimu wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana kuliko mapungufu machache tunayoyaona hasa kupitia mitandao ya kijamii. Walimu wamekuwa wakifundisha, wakilea vijana wetu katika mazingira tofauti pamoja na kutoa huduma mbalimbali ambazo nyingine zilitakiwa kutolewa na wazazi au walezi.

“Bahati mbaya kwa jamii zetu ni kuwa, jambo baya husambaa kwa haraka zaidi kuliko jema. Hata hivyo, licha ya mapungufu kutoka kwa baadhi ya walimu kama nilivyoainisha, walimu wetu wanafanya mambo mengi na makubwa ya kimalezi kwa watoto wetu ambayo pengine hayasambazwi na kuonekana”.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi wa maelezo yangu hapo juu, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa jamii kutobeza juhudi zinazofanywa na walimu wetu badala yake tuwatie moyo, hasa wale wanaozingatia miiko ya taaluma zao na misingi ya malezi. Pia nitoe wito kwa jamii, hasa wale wanaochukua au kupata matukio haya na kuyarusha kwenye mitandao, kutofanya hivyo, kwani yanajenga chuki kwa walimu na taswira hasi kwa walimu wote badala ya wahusika wachache. Pale matukio kama haya yanapojitokeza, taarifa zake zitumwe kwa mamlaka husika ili hatua stahiki zichukuliwe badala ya kuleta taharuki kwa jamii nzima.

Mheshimiwa Spika, “ninaomba nieleweke hapa kuwa lengo si kuficha taarifa, bali ni kuzuia taharuki, chuki na uhasama ndani ya jamii zetu. Si kwa walimu tu bali kwenye nyanja nyingine za utumishi kama afya, vyombo vya ulinzi na usalama na maeneo mengine yanayofanana na hayo”.

Mheshimiwa Spika,ninatambua si kusudio la walimu kuwadhuru wanafunzi lakini tukubaliane kuwa kuna udhaifu katika utaratibu wa utoaji na usimamizi wa adhabu ya viboko shuleni”. Hivyo, nitoe wito kwa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya kuwakumbusha walimu wote nchini kuzingatia mwongozo wa utoaji adhabu shuleni chini ya kifungu Na. 61 cha Sheria ya Elimu, Sura ya 353 ya sheria zetu pamoja na kanuni zake.

Mwongozo umesisitiza kuwa, “Adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima”. Na kuwa adhabu hii itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi kama nilivyotangulia kueleza hapo awali.

By Jamhuri