Na Cresensia Kapinga,JamhuriMedia,Songea

MRAJIS msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Ruvuma,Peja Mhoja amewataka mameneja wa vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika, kutumia mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU )mfumo ambao utakwenda kurahisisha zoezi la upatikanaji wa takwimu na taarifa sahihi kutoka kwenye vyama vyao na si vinginevyo.

Mhoja ameyasema hayo jana wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu ambacho kimewashirikisha mameneja wa vyama vya msingi na vyama vikuu kutoka wilaya za Tunduru na Songea mkoani Ruvuma kinachofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Ushirika Manispaa ya Songea.

Amesema kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kuelekezana namna ya kutumia mfumo wa usimamizi wa vyama vya ushirika na kuhakikisha kwamba sekta ya ushirika inasimamiwa na kudhibitiwa ipasavyo ili kukuza uchumi wa nchi lakini na uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.

“Wito wangu kwa mameneja wa vyama vya ushirika nawaomba wawe wasikivu kwani mara tu baada ya kupata mafunzo haya tunaanza kutumia mfumo mara moja ili kupata tawimu na taarifa sahihi kutoka kwenye vyama” amesema Mhoja.

Aidha amesema kuwa mfumo huo wa kidigital utasaidia kudhibiti shughuli za vyama vya ushirika na utakwenda kuondokana na makaratasi na kusafiri safiri mara kwa mara na muda mwingine kutoa taarifa ambazo zinakinzana na kuifanya tume kushindwa kuwa na takwimu zilizo sahihi.

Kwa upande wake Afisa Ushirika wa Wilaya ya Tunduru, George Bisan, amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuendana na wakati kwani Dunia Sasa ipo kwenye mfumo wa kidigitali na inatoka wenye mfumo wa analogi lakini pia itasaidia kusimamia na kuingiza takwimu mbalimbali za ushirika kama tume ya ushirika inavyotaka.

Nao mameneja wa vyama vya msingi na vyama vikuu wameishukuru ofisi ya mrajis pamoja na maafisa ushirika wa Mkoa wa Ruvuma kwa ushirikiano wanaoutoa kwenye mafunzo hayo na kwamba mafunzo hayo yatasaidia kuondokana na changamoto ya mawasiliano pia yatapunguza gharama ya kusafiri umbali mrefu kupeleka Takwimu japo kuna baadhi ya vyama havina bado kompyuta.

Please follow and like us:
Pin Share