Na Alex Kazenga Dar es Salaam.

Kampuni ya SUMAJKT Bottling Co. Ltd inayozalisha maji ya Uhuru Peak Pure Drinking Water, imetanua bidhaa hiyo na sasa kiwanda hicho kitazalisha hadi maji makubwa kwa ajili ya maofisini na majumbani.


Kiwanda hicho kilichopo Mugulani Dar es Salaam, kimefikia uwezo huo baada ya kuzindua mikondo miwili ya kuzalisha maji; mmoja ukiwa na uwezo wa kuzalisha maji makubwa ya lita 13 hadi 18.

Akizindua mikondo hiyo, muonekano mpya wa chupa ya maji ya Uhuru Peak pamoja na magari mawili ya kubebea bidhaa hiyo, Mkuu wa Majeshi ya ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda jana jijini Dar es Salaam amesema ; “Matarajio ya awamu ya sita kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ni makubwa.”


“Rais anatambua na kujivunia uwepo wa JKT, jukumu la malezi kwa vijana mnalifanya kwa weredi na kuifanya nchi kuwa na amani.”

Amesema,kutokana na mchango wa jeshi hilo, SUMAJKT wamepewa mradi wa kujenga nyumba tisa katika mji wa serikali Dodoma, nyumba 5000 Msomera Tanga sambamba na ulinzi wa bomba la mafuta linalojengwa kutoka Hoima hadi Chongeleani mkaoni Tanga.


Naye, Mkuu wa Tawi la Utawala la JKT, Brigadia Jenerali Hassan Mabena aliyemuwakilisha Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajab Mabele amesema kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2018 kikiwa na uwezo mdogo.


“Yalipitishwa mapendekezo ya kufanya maboresho ili kukiongezea uwezo, mapendekezo ya kuagiza mitambo yalipitishwa, imenunuliwa na imezinduliwa,” amesema Brigadia Jenerali Mabena.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT, Kanali Petro Ngata amesema mikondo hiyo miwili itaongeza wigo wa biashara ya maji hayo na kuchochea ongezeko la wateja na mapato.

Amefafanua, mikondo iliyozinduliwa; wa kwanza unazalisha maji ya chupa zenye ujazo wa mililita 350, mililita 600 na lita moja na una uwezo wa kuzalisha lita 10,000 kwa saa.


Wa pili, amesema unazalisha chupa za maji 500 kwa saa zenye ujazo wa lita 13 hadi 18.


“Mkondo wa kwanza pia utazalisha maji premier, haya ni kwa ajili wateja binafsi na wenye shughuli maalum,” amesema Brigadia Kanali Ngata.

By Jamhuri