Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala amewataka wakazi wa mkoa huo kuhakikisha wanafanya usafi wa mara kwa mara katika maeneo yao Ili watalii na wawekezaji waone Mkoa huo unang’aa.

RC Makala ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza katika zoezi la ufanyaji wa usafi wa Jumamosi ya mwisho wa mwezi ambalo limefanyika katika makutano ya barabara ya Azikiwe/Maktaba jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makala (kulia) akiwa na Mkuu wa wilaya ya Ilala Ng’wilabuzu Ludigija (kushoto) wakati akizungumza katika zoezi la ufanyaji wa usafi wa Jumamosi ya mwisho wa mwezi ambalo limefanyika katika makutano ya barabara ya Azikiwe/Maktaba jijini Dar es salaam.

Mkuu huo wa mkoa amepiga marufuku ya utupaji wa taka katika maeneo yote ya barabara zinazoingia katikati ya Jiji kwani ni kitovu cha watalii na wadau mbalimbali kutoka nje ya nchi pamoja na wawekezaji.

“Tusitupe takataka hovyo tusafishe maeneo yetu kuanzia nyumbani,mtaa na hata katika maeneo ya kazi lakini kikubwa mvua zimeanza kunyeesha hivyo ni vyema pia tukaanza kusafisha mitaro ili kufanya maandalizi”amesema RC Makala.

Awali akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng’wilabuzu Ludigija ameendelea kusisitiza kuwa ni marufuku kuweka taka kiholela kwani watachukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wanaofanya uchaguzi wa mazingira.

Pia amewataka wafanyabiashara wahakikishe kabla ya kufungua biashara zao mapema wanafanya usafi Katika maeneo yao ili yaweze kuwa katika Hali ya usafi.

Mkuu wa wilaya ya Ilala Ng’wilabuzu Ludigija akiwa Kwenye picha ya Pamoja na wadau wa mazingira akieleza mikakati ya Wilaya hiyo katika kuhakikisha suala la usafi linakuwa endelevu Kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji.

“Mitaa yote 156 na kata 36 tunaendelea kuwakumbusha wananchi na wafanyabiashara wote kuwa hatuzuii kufanya biashara bali ni vyema wakatambua kuwa ni wajibu wao wa kila siku”ameendelea kusisitiza DC Ludigija.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha wafanyabiashara Wadogo Wadogo (Machinga) mMoa wa Dar es Salaam, Yusuph Namoto amewakumbusha wafanyabiashara kuhakikisha wanaendelea kufanya biashara katika maeneo rasmi.

By Jamhuri