Wakazi wa mkoani Mwanza na maeneo ya jirani ya mkoa huo wamejitokeza kwa wingi kupata elimu ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwenye banda la Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu ambapo kupitia Idara ya Hifadhi ya Jamii na Mifuko ya PSSSF, NSSF na WCF.

Hayo yamejiriameri katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea katika viwanja vya Rock City Mall, jijini humo yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Elimu ya Fedha kwa Maendeleo ya Watu.”

Akizungumza na wananchi waliotembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Hifadhi ya Jamii, Bw. Omary Mziya ameeleza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Idara ya Hifadhi ya Jamii ina wajibu wa kusimamia, kuratibu na kujenga mazingira wezeshi yanayolenga kuendeleza sekta ya hifadhi ya jamii nchini.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Hifadhi ya Jamii, Bw. Omary Mziya akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Kifedha yanayofanyika katika viwanja vya Rock City Mall, Jijini Mwanza leo Novemba 25, 2022.

“Sekta ya hifadhi ya jamii ni sehemu ya sekta ya fedha nchini na inafahamika mifuko ya hifadhi ya jamii inakusanya michango ya wanachama na inalipa mafao, yote hiyo ni sehemu ya huduma za kifedha, hivyo ushiriki wa Ofisi ya Waziri Mkuu katika maonesho haya kama waratibu wa mifuko ya hifadhi ya jamii tumedhamiria kutoa elimu zaidi kwa umma kuhusiana na sekta hii,” amesema

Ameongeza kuwa, majukumu mengine ya Idara hiyo ni; Kuongeza wigo wa huduma ya Hifadhi ya Jamii kwa kuzifikia sekta zote ikiwa ni pamoja na sekta isiyo rasmi, kusimamia utendaji bora wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yote, Kulinda na kutetea maslahi ya wanachama, kushughulikia migogoro na malalamiko ya waeja kuhusiana na hifadhi ya jamii, kufanya kaguzi ili kuangalia hali ya mifuko sambamba na kuendesha shughuli zinazolenga kuelimisha umma na kuwajengea uelewa juu ya sekta ya Hifadhi ya Jamii.

Aidha, Bw. Mziya amewasihi wananchi kutumia fursa ya maadhimisho hayo ili kupata elimu na huduma zinazotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ikiwemo kujihakiki, kuangalia taarifa za michango yao, kufuatilia mafao na kupata taarifa mbalimbali za uwekezaji wa Mfuko.

Wakielezea kwa nyakati tofauti wananchi waliotembelea banda hilo wamepongeza Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sekta ya hifadhi ya jamii na kuwajengea uelewa wa sekta hiyo.

By Jamhuri