Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Bagamoyo
Makawa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya zote, Mkoani Pwani wameaswa kuacha kujiingiza katika migogoro na kuwa sehemu ya wapiga debe kwa wanachama walioanza kucheza rafu ili kuwania nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa 2024 na uchaguzi Mkuu 2025.
Aidha wametakiwa kusemea Chama na Serikali kwa makubwa yanayofanyika chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa,Dkt Samia Suluhu Hassan na kumuunga mkono kwa jitihada kubwa anazozionyesha kupeleka miradi mingi ya kimkakati, mikubwa,ya kati na midogo katika mkoa huo.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Pwani, David Mramba aliyaeleza hayo, Mjini Bagamoyo wakati wa kufunga semina elekezi ya siku tatu kwa Makatibu hao, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Katibu wa Siasa na Uenezi Taifa Comred Sofia Mjema .
Alieleza, viongozi waliopo madarakani wakiwemo wabunge, madiwani,wenyeviti wa Vitongoji,Vijiji na Serikali za mitaa waachwe wamalize ngwe ya uongozi wao bila kubughudhiwa na kuyumbishwa.
Mramba alisema, wakati Utafika kwa mujibu wa katiba, kufuata kanuni na taratibu za Chama kutangaza muda wa uchaguzi lakini kwasasa bado ni mapema.
“Tukielekea maandalizi ya chaguzi za Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji mwakani na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025, Makatibu wa Siasa na Uenezi wa CCM ,tumetoa semina elekezi kwa lengo la kuwajengea uwezo kwaajili ya kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo”alifafanua Mramba.
Mramba alisema lengo la Semina hiyo ni kujenga uwezo wa kuhamasisha Watanzania kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kuhakikisha Taifa linapiga hatua za maendeleo.
“Yapo maelekezo sisi Makatibu wa Siasa na Uenezi wa CCM wa mikoa hapa nchini kutoka kwa Katibu wa NEC Comred Sofia Mjema kwaajili ya kuwashushia Makatibu wa Siasa na uenezi wa ngazi ya wilaya mafunzo haya yataenda kuwa chachu ya hamasa katika maeneo yetu ya Mkoa wa Pwani” alisema Mramba.
Alisema Idara ya uenezi ni idara kamili ndani ya CCM, idara hii ndio inayoweza kukifanya Chama kisonge mbele na, kitasonga mbele kwa kutangaza kazi zilizofanyika serikalini kupitia Chama cha Mapinduzi.
Katibu Siasa na Uenezi wa CCM Kibaha Mjini, Clemence Kagaruki alieleza, wamebeba maelekezo yaliyotolewa na wanaahidi kuendelea kwenda kuyasimamia.
Kagaruki alieleza, kikubwa ni wanachama kuwa wamoja,kushikamana kwa kuondoa mihemko, ili kushika dola kwenye chaguzi zijazo.