Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC)- Itikadi na Uenezi Komredi Paul Makonda leo Oktoba 26,2023 amekabidhiwa rasmi ofisi na Dk Sophia Mjema ambae ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais kwenye masuala Wanawake na Makundi Maalumu ambapo mamia ya Wanachama wa CCM walifurika Ofisi Ndogo za Makao makuu ya CCM Lumumba Dar es Salaam kumpokea.

Makonda akizungumza katika mapokezi hayo, amewatoa shaka wale wote waliodhani yupo na mpango wa kulipa kisasi kwa wale waliomkosea na badala yake atafanya kazi aliyotumwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan na Chama Cha Mapinduzi.

Aidha Makonda amemshukuru Mwenyekiti wa CCM Rais Samia na Kamati Kuu ya Chama hicho kwa imani na dhamana kubwa waliyompatia kiasi cha kumpatia nafasi kama hiyo na ameahidi kuifanya vyema kazi waliyomtuma.

Pamoja na hayo Makonda ametumia nafasi hiyo kuwaomba wana CCM na wananchi wote kumpa ushirikiano wa kutosha Ili aweze kuifanya kazi kwa ufanisi huku akiwataka Viongozi wakewemo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu Wilaya na watendaji kuwatumikia Wananchi kwa kushughulika na kero na changamoto za wananchi.