đź“ŚAagiza Mkurugenzi wa Huduma kwa wateja Tanesco kuondolewa

đź“ŚAsisitiza miradi ya mafuta ya Gesi Asilia kubadilisha maisha ya wananchi

Msimbati – Mtwara

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza kuondolewa kwa Meneja Mawasiliano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutokana na kushindwa kutoa taarifa mbalimbali na kutofanya mikutano na wananchi wanaozunguka miradi ya gesi asilia ikiwemo dharura zinazotokea katika Mkuza wa Bomba la Gesi.

Dkt. Biteko ametoa maagizo hayo tarehe 14 Novemba, 2023 wakati aliposimama katika Kijiji cha Msimbati wilayani Mtwara, Mkoa wa Mtwara ili kuzungumza na wananchi akiwa anatokea kukagua visima vya kuzalisha na mitambo ya kuchakata Gesi ya Mnazi Bay iliyopo katika Kata ya Msimbati wilayani humo.

Wananchi wa Kata ya Msimbati walimweleza Dkt.Biteko kuhusu changamoto walizonazo ikiwemo barabara, kituo cha afya, kutopata fedha zozote kutokana na kazi za uzalishaji wa uchakataji Gesi Asilia unaofanyika kwenye kijiji hicho na kutopata taarifa mbalimbali za mradi ikiwemo zinapotokea changamoto kwenye bomba la Gesi Asilia.

“Changamoto kwenye miradi hii zinatokea lakini lazima awepo mtu ambaye ni daraja kati ya Serikali na Wananchi, na Mtu huyu analipwa mshahara kwa kazi hiyo, haiwezekani Waziri au Rais kuja kutoa taarifa kwa wananchi wakati kuna mtu kaajiriwa kwa kazi husika, wananchi hawa wanapaswa kupata taarifa.” Amesisitiza Dkt.Biteko

Katika hatua nyingine, ameagiza Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuondolewa katika nafasi hiyo kutokana na majibu yasiyo stahiki wanayojibiwa wananchi wanapopiga simu kwenye Shirika hilo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.

Vilevile, Dkt. Biteko ameagiza kuwa, miradi inapotekelezwa katika eneo lazima ibadilishe maisha ya wananchi, ikiwemo pia upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile Shule, Vituo vya Afya, Barabara na Maji.

“Changamoto zote mlizozieleza hapa nataka niwahakikishie kuwa zitashughulikiwa, nataka muone tofauti kuanzia sasa, kama Gesi Asilia inatoka hapa na inaendesha mitambo ya umeme kwa asilimia 65, haiwezekani wala haiingii akilini, watu hawa wakalia kituo cha Afya, Polisi, ubovu wa barabara, haiwezekani, nataka niwaeleze kwamba ushuru wa huduma unaokusanywa na halmashauri sehemu ya fedha lazima irudi hapa.” Amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko, amewaagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara pamoja Mkuu wa Wilaya kukaa pamoja na wananchi wa eneo hilo ili mpango wa maendeleo wa kijiji hicho uandaliwe, hivyo fedha zinapotolewa zifanye maendeleo kulingana na mpango wa kijiji.

Aidha, ameiagiza TPDC kuweka mpango maalum wa Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Jamii (CSR) katika eneo hilo ili wananchi hao waone faida ya kuwepo kwa miradi kwenye maeneo yao na kuwaelekeza kuwaagiza wajenge kituo cha afya, taa za barabarani na Kituo cha Polisi.

Ili kuhakikisha kuwa, Jamii zinazozunguka na miradi ya Mafuta na Gesi Asilia zinafaidika na uwepo wa miradi hiyo, Dkt.Doto.Biteko amesema kuwa Serikali itakuja na kanuni zitakazoongoza masuala ya CSR lengo likiwa ni kuhakikisha jamii zinazozunguka miradi ya Mafuta na Gesi zinanufaika.