Mali iliyopatikana kabla ya ndoa inahesabika ya familia?

Mara kadhaa linapoibuka suala la kugawana mali pale ndoa inapohesabika kushindikana, masuala kadhaa ya msingi na yanayohitaji uelewa huwa yanaibuka. Moja ya suala kati ya masuala ambayo huibuka ni hili la kutenganisha na kufafanua hadhi ya mali za wanandoa ili mgawanyo uweze kufanyika kwa haki.

Yawezekana mwanandoa akadhani ana haki katika mali fulani lakini kumbe kisheria hana haki hiyo, ni mtazamo wake ndio unamsukuma kuamini hivyo. Halikadhalika yawezekana mwanandoa kudhani hana haki katika mali fulani kumbe anayo haki.  Ili kujua una haki ipi katika mali ipi na hauna haki katika mali ipi, ya hitajika kujua misingi ya kisheria inayotumika kugawanya mali za wanandoa.

Kugawana mali za wanandoa

Ieleweke kuwa tunapoongelea wanandoa kugawana mali tunaongelea talaka. Hakuna kugawana mali bila talaka. Na kisheria talaka inapotoka tu, swali linalofuata ni habari ya mali na watoto kama wapo. Mali si lazima magari na nyumba, lakini  pia hata vyombo vya ndani vikiwemo vitanda, makabati, sahani nazo ni mali kwa mujibu wa sheria. Navyo huhitaji mgawo.

Kugawana nusu kwa nusu?

Linapokuja suala la kugawana mali, wengi hudhani mtindo unaotumika kugawa ni ule wa nusu kwa nusu.  Jambo hili si kweli, kwa kuwa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 haisemi kuwa utaratibu wa kugawana mali ni nusu kwa nusu. Sheria hii imeweka msingi mkuu wa kugawana mali ambao ndio hutumika katika mahakama zetu katika kutoa maagizo ya kugawa mali za wanandoa.  Msingi uliowekwa na sheria ni msingi wa kiwango cha  mchango wa mwanandoa katika kupatikana kwa mali husika.

Kiwango alichochangia mwanandoa katika kupatikana kwa mali hiyo ndicho kitakachokadiriwa na kiwango hicho ndicho atakachopewa. Kwa hiyo kama ni nyumba ya vyumba sita, mmoja anaweza kupata chumba kimoja na mwingine akapata vitano kutegemea na mchango wake. Na mchango hapa siyo leta ni lete.

Mchango si hela tu, hata kazi za nyumbani anazofanya mama wa nyumbani ambaye haleti hela nazo huitwa mchango ambapo hukadiriwa na kupata kile anachostahili.

Mali kabla, baada ya ndoa

Katika kutenganisha mali za wanandoa, huwa zinatenganishwa katika makundi makuu matatu. Kwanza, kuna mali ambazo mtu alikuwa nazo kabla ya ndoa na wakati anaingia katika ndoa ameingia nazo. Kwa mfano, mwanamke ameolewa akamkuta mwanamume tayari ana nyumba yake. Pili,  kuna mali ambazo zimepatikana wakati wawili wakiwa katika ndoa.

Kwa mfano, ndoa imefungwa wawili wakaanza kuishi pamoja na taratibu wakaanza kujenga na kukamilisha. Tatu, ni mali ambazo zimepatikana katika ndoa lakini zikiwa hazina uhusiano wowote wa kindoa, kwa mfano kurithi au kuzawadiwa mali.

Mali kabla ya ndoa

Mali iliyopatikana kabla ya ndoa na ikaendelea kuwepo kipindi cha  ndoa inaendelea kuwa ya huyo mhusika tu bila ushirika wa mwenza wake. Kama  ni nyumba mwanamke alikuwa nayo kabla ya kuolewa au ni mwanamume alikuwa nayo kabla ya kuoa, basi inaendelea kuwa ya kwake peke yake na haihusiki katika mgawo, suala la mgawo linapojitokeza.

Hata hivyo inaweza kuingizwa katika mgawo ikiwa kuna mchango wowote wa kuiendeleza uliotolewa na mwenza. Kwa mfano, kabla ya ndoa ilikuwa na vyumba viwili, lakini katika kipindi cha ndoa imepanuliwa na kufikia vyumba vitano au ilikuwa haina uzio au haina madirisha kabla ya ndoa lakini baadaye vitu hivi vikawepo.

Katika hali kama hiyo itatakiwa iingizwe katika mgawo na kutazama kiwango cha mchango wa kila mmoja katika uendelezaji huo. Ni hapo ambapo mchanganuo utafanyika ili kila mmoja apate haki kutokana na kiwango cha mchango  wake.

Ikiwa hakuna uendelezaji wowote uliofanyika katika mali, yaani labda nyumba ilivyokuwa kabla ya ndoa ndivyo hivyo hivyo ilivyoendelea kubaki hata baada ya ndoa, basi mali hiyo haitatakiwa kuingizwa katika mali za mgawo, bali itabaki mali ya mwanandoa mmoja pekee ambaye ndiye mmiliki wa tangu awali.

Hali ni hiyo hiyo hata kwa mali ambayo imepatikana katika ndoa lakini ikiwa haina uhusiano na kipato cha wanandoa. Kwa mfano, mali ya urithi au zawadi. Hii ina maana ikiwa mali hii itaendelezwa, basi mchango wa uendelezaji utatathminiwa na ikiwa haitaendelezwa, basi itabaki mali ya mrithi au mpewa zawadi pekee na haitahusu mgawo.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, kampuni au ndoa tembelea SHERIA YAKUB BLOG.