Katika familia yangu tuliwahi kupata jeraha. Septemba 14, 1999 lilitokea tukio la kuhuzunisha kwenye familia yangu. Dada yangu kipenzi, Cecilia aliuawa kikatili, na aliyetenda tukio hilo ni mumewe. Dada aliuawa akiwa anamnyonyesha mtoto wake wa kike aliyekuwa na umri wa miezi mitano.

Tukio hili tulilipokea kwa mwono wa dharau. Tuliamini kwamba, mume wa dada yetu amemuua dada yetu kwa kutudharau. Vijana tuliapa kulipa kisasi. Tulitaka nasi kuua. Katika hali ya usiri sana, mama yetu mzazi alifahamu nia yetu. Akatuita wote kwa pamoja na kutuambia: “Wanangu nia mliyonayo ni mbaya. Acheni. Ninyi ni Wakristo! Kristo aliwapenda maadui zake. Mpendeni aliyemuua dada yenu. Kumpenda adui ni wito wa Kikristo. Nawaombeni mnisikilize.” Busara hii iliyokuwa imejaa upendo na hekima ilitawanya mawazo yetu. Mpaka leo tunasalimiana na kutembeleana vema na aliyemuua dada yetu. Tunampenda. Palipo na upendo kuna maisha. Tupendane. Methali ya watu wa Ufilipino  inasema: “Upendo ni chumvi ya maisha.”

Ukweli ni kwamba, unapokuwa umemchukia mtu yeyote yule aliyekuumiza, unakuwa bado uko kifungoni. Ili utoke kifungoni ni lazima umfungue yule aliyekupeleka kifungoni. Maumivu na uchungu hutufanya kuwa wafungwa wa mazingira ya zamani na hutukumbusha daima kile kilichotokea zamani. Mwaka 2018, nilitoa chapisho langu la kitabu kinachoitwa: ‘Usikate tamaa katika maisha.’’ Hiki ni kitabu ambacho kimegusa maisha ya wasomaji wengi. Wengi waliokisoma kitabu hiki wamekiri kubarikiwa na wengi kubadilisha mienendo yao ya kimaisha. Nilipata mshituko pale ambapo msomaji wangu mmoja aliponitumia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yangu ya kiganjani. Ujumbe wake ulikuwa unasomeka hivi: “Bw, William, nilipokuwa na umri wa miaka tisa nilibakwa na rafiki yangu aliyekuwa na miaka 14. Sijawahi kumwambia mtu yeyote kilichotokea, lakini nimeitunza chuki hii moyoni. Imepita miaka 19 lakini moyo wangu bado una maumivu na hasira dhidi ya wanaume. Kila ninapokutana na mume wangu kimwili ninajisikia kubakwa. Ninashiriki tendo la ndoa kwa shinikizo la mume wangu.”

Moyo wangu uliumia nilipogundua maumivu aliyokuwa ameyabeba mwanadada huyu kwa miaka 19. Hasira inatunza chuki moyoni. Katika mazungumzo yangu binafsi na mwanadada huyu nilimuuliza: “Ungependa Yesu akufanyie nini?” Alilia kwa nguvu. Niligundua kwamba ana maumivu ya nafsi na moyo. Moyo wake ulikuwa umejeruhiwa sana. Mioyo ya watu wengi imevunjika vunjika. Mioyo ya watu wengi inavuja damu. Watu wengi wameumizwa. Watu wengi wana majeraha na wanashindwa namna ya kuyaondoa majeraha yao. Watu wengi wametunza majeraha kwenye mioyo yao.

Ninaomba kukuuliza swali: “Je, moyoni mwako umebeba nini?” Kama  umembeba mtu, mtue. Mtue mume wako aliyekuumiza. Mtue mke wako aliyekuumiza. Mtue mtoto wako aliyekuumiza. Mtue jirani yako aliyekuumiza. Mtue mzazi wako aliyekuumiza kwa kukubaka, kukunyanyasa, kukutukana au kukukataa. Mtue rafiki yako aliyekuumiza. Mtue mfanyakazi mwenzako aliyekuumiza. Mtue mteja wako aliyekudhulumu fedha na rasilimali nyinginezo. Kama una kinyongo, kidondoshe. Kama umeitunza hasira, iondoe. Itafute amani. Utafute upendo. Kristo anasubiri kukuponya. Anasubiri kuyaponya majeraha yako. Anasubiri uwe tayari kuyaachilia yote uliyoyatunza moyoni mwako. Amua kuwa huru kuanzia leo. Tangu huko gerezani ulipofungwa.  Balidilisha historia ya maisha yako kuanzia leo.

Nakusihi, ‘Usitunze chuki moyoni kwa muda mrefu’. Ajabu ni kwamba ukiwa na uvundo mwingi wa chuki moyoni mwako unaweza ukaanza kuwaza mawazo ya kujinyonga, kulipa kisasi, kunywa pombe kupita kiasi ama kunywa sumu. Unapokuwa umeshindwa kusamehe usitegemee kupata amani ndani ya moyo wako.

Hatuwezi kuishi pasipo kutoa msamaha au kuupokea msamaha. Kumbuka! Msamaha unajenga uhusiano uliovunjika. Una kila sababu ya kutoa msamaha. Una kila sababu ya kuwa na amani. Una kila sababu ya kuwa na uhusiano mzuri na familia yako. Una kila sababu ya kuwa mshauri mzuri, hivyo basi kuwa mwepesi wa kutoa msamaha kwa wanaokukosea. Anza leo kuomba msamaha kwa Mungu. Anza leo kuomba msamaha kwa uliowakosea. Anza leo kuwasamehe waliokukosea. Leo hii utakuwa mwana wa Mungu na mbinguni ndiko kutakuwa nyumbani kwako milele yote.

899 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!