Mambo ya kutisha yalitokea ndani ya kanisa la TB Joshua, adaiwa kuwabaka na kuwanyanyasa wanawake

Ushahidi wa unyanyasaji ulionea na mateso kutoka kwa mwanzilishi wa mojawapo ya makanisa makubwa ya kiinjili ya Kikristo duniani umefichuliwa na BBC.

Makumi ya waumini wa zamani wa Kanisa la Synagogue Church of all Nations – watano Waingereza – wanadai ukatili, ikiwa ni pamoja na ubakaji na utoaji mimba kwa lazima, uliofanywa na marehemu TB Joshua wa Nigeria.

Madai ya unyanyasaji katika eneo la siri la Lagos yamedumu kwa takriban miaka 20.

Kanisa la Synagogue Church of All Nations halikujibu madai hayo lakini lilisema madai ya hapo awali hayana msingi.

TB Joshua, aliyefariki mwaka wa 2021, alikuwa mhubiri na mwinjilisti mwenye mvuto mkubwa na mwenye mafanikio makubwa ambaye alikuwa na wafuasi wengi duniani.

Ripoti ya kiuchunguzi iliyofanywa na BBC, Iliyokusanya shuhuda kutoka kwa watu kadhaa walionusurika unaonesha kuwa TB Joshua alikuwa akiwanyanyasa, kuwabaka wanawake na vijana kutoka ulimwenguni mara kadhaa kwa karibu miaka 20.

Mashuhuda wa kwanza waliozungumza na BBC ni mabinti wawili Rae na Carla ambao wamedai kuwa mwanzoni mwa mwaka 2002 walisafiri pamoja kwenda nchini Nigeria kufuata huduma ya uponyaji ya Mtume TB Joshua kwenye Kanisa lake la Synagogue Church of All Nations Scoan], ambapo baada ya kukutana nae Rae akaamua kubaki kuishi kwa miaka 12 kwenye boma la mchungaji huyo kwa ajili ya huduma zaidi ya kiroho.

“Nilimwacha pale, Sitawahi kujisamehe kwa hilo” amesema Carla, huku machozi yakitiririka

Kwa sasa Rae amerudi nchini Uingereza akiishi katika kitongoji kizuri mashambani, Anatabasamu na kucheka kwa uhuru, lakini ukimuuliza tu kuhusu maisha yake ndani ya jumba la TB Joshua midomo yake inabana, anaongea akipumua, Wakati mwingine anabadilika rangi usoni, hii ina maanisha kuna jambo halipo sawa kwake.

Rae alisalia kwa miaka 12 katika boma la Joshua

Kanisa linaonekana kama hekalu la kale juu ya kitongoji cha Ikotun huko Lagos, jiji kubwa zaidi la Afrika, TB Joshua ametengeneza ghorofa zote 12 za jumba lililopakana nayo, ambapo aliishi pamoja na wafuasi wake wengi. Alisimamia ujenzi wa ngazi nyingi za chumba chake cha kulala, milango mitatu ya kuingia ndani ya chumba hicho, ndani na nje, pamoja na chumba cha maombi kilichofichwa kimejaa vioo vidogo na “kliniki” ya chini.

Wanawake wengi wanasema walishambuliwa kingono na Joshua, huku baadhi wakidai kuwa walibakwa mara kwa mara wakiwa wamefungiwa. Wengine wanasema walilazimishwa kutoa mimba baada ya kupata ujauzito.

Uchunguzi huo wa miaka miwili, kwa ushirikiano na jukwaa la kimataifa la vyombo vya habari Open Democracy, umehusisha zaidi ya waandishi wa habari 15 wa BBC katika mabara matatu. Walikusanya kumbukumbu za rekodi za video, hati, na mamia ya saa za mahojiano ili kuthibitisha ushuhuda wa Rae na kufichua hadithi zaidi za kutisha. Zaidi ya mashahidi 25, kutoka Uingereza, Nigeria, Ghana, Marekani, Afrika Kusini na Ujerumani, wametoa maelezo ya jinsi ilivyokuwa ndani ya boma la Joshua, na matukio ya hivi karibuni zaidi katika mwaka wa 2019.

Wafuasi wa zamani wa kanisa hilo walijaribu kuzungumzia unyanyasaji, lakini wanasema wamenyamazishwa au kudharauliwa na wengine wawili wamedai kupigwa, huku kwa upande wao Kanisa la Synagogue Church of All Nations halikujibu madai hayo, lakini lilisema madai ya hapo awali hayana msingi.

Wafuasi wengi wa TB Joshua walivutiwa na ufadhili wake, lakini wengi wao walikuja kwa kile kinachoitwa miujiza yake. Joshua alirekodi kwa utaratibu “uponyaji” wa kuvutia katika maisha yake yote. Baada ya Joshua kuwaombea, watu binafsi kwenye kamera walitoa ushuhuda wa kuponywa magonjwa kama saratani na VVU/Ukimwi, kipandauso na upofu wa kudumu.

Video kadhaa za Joshua zinaonesha wanaume walioambukizwa vibaya sehemu za siri, ambazo zilipasuka na kupona kimiujiza anapoinua mkono wake katika maombi, Nyingine zinaonesha wanawake wanaohangaika kuzaa, ambao huzaa watoto wao papo hapo Joshua anapokaribia. Baada ya kila tukio, wale waliohusika wangeshuhudia kuokolewa.

Agomoh Paul anasema kila kitu kilichokuwa kinafanyika kilipangwa, na yeye ndiye aliyekuwa akisimamia zoezi hilo.

“Walioponywa mara nyingi walikuwa wakilipwa kufanya au kutia chumvi dalili zao kabla ya uponyaji wao unaodhaniwa kufanyika, katika baadhi ya matukio, wanasema, watu walikuwa wamenyweshwa dawa bila kujua au kupewa dawa za kuboresha hali zao wakiwa kanisani, na baadaye kushawishiwa kutoa ushuhuda kuhusu kupona kwao, Wengine walidanganywa kuwa walikuwa na VVU/UKIMWI na kwamba, kutokana na huduma za Joshua, sasa walikuwa hawana virusi” amesema Agomoh.

Shuhuda mwingine aliyethibitisha kufanyiwa ukatili wa kingoni na TB Joshua ni Jessica Kaimu, ambaye sasa ni mwandishi wa habari nchini Namibia, anasema alikuwa na umri wa miaka 17 tu na bikira wakati Joshua alipombaka kwenye bafu la nyumba yake ya kifahari, ndani ya wiki chache baada ya kuwa mfuasi.

“Nilikuwa nikipiga kelele na alikuwa akininong’oneza sikioni kwamba niache kujifanya kama mtoto… niliumia sana, sikuweza kulia,” anasema.

Baadhi ya waliohojiwa ambao wanasema walibakwa na kupewa mimba na Joshua, wanaeleza jinsi walivyopewa pia mimba za kulazimishwa kuzitoa ndani ya boma – katika eneo linalojulikana kama “idara ya matibabu” au “kliniki”.

“Yote yalifanywa kwa usiri,” anasema Sihle, mfuasi wa zamani wa Afrika Kusini, ambaye ametoa mimba mara tatu kwa lazima kanisani.

“Unapewa mchanganyiko wa kunywa na unaugua au wanaweka vipande hivi vya chuma kwenye uke wako na kutoa chochote na hujui kama [kwa bahati mbaya] vinaweza kutoa mfuko wako wa uzazi au vipi”
Sihle alilia katika mahojiano yake yote, kama vile Jessica ambaye anasema alipewa mimba tano za kulazimishwa kutoa.
Wanafunzi walimhudumia kila haja yake, walimfanyia masaji, wakamsaidia kuvaa, wakapuliza manukato alipoingia chumbani walimwekea glavu za plastiki mikononi mwake ili aweze kula chakula chake bila kugusa hata chembe.

Badala ya kumwita kwa jina lake, wote waliamrishwa kumwita “daddy”, japo hilo sio jambo geni kwa mchungaji wa Kinigeria katika mila ya Kipentekoste kuitwa hivi, lakini wanafunzi wanasema lilikuwa jina ambalo Joshua alisisitiza.

Wanafunzi wanasema walilazimishwa kufanya kazi, bila malipo, kwa saa nyingi kila siku, wakiendesha mambo yote ya kanisa kuu, wote wanasema kuwanyima usingizi lilikuwa jambo la kawaida, huku taa zikiwashwa kwenye mabweni usiku.

Ikiwa mtu yeyote angekamatwa akilala bila ruhusa, au kuvunja sheria nyingine zozote za Joshua, angeadhibiwa. Wanafunzi 19 wa zamani walielezea kushuhudia mashambulizi ya kikatili au mateso ndani ya boma, yaliyotekelezwa na Joshua au kwa amri yake.

Wanafunzi wengine walielezea kuvuliwa nguo na kuchapwa kwa nyaya za umeme na mjeledi wa farasi unaojulikana kama koboko, miongoni mwa wale wanaodaiwa kuchapwa zaidi ni wanafunzi wenye umri wa miaka saba.

“Ilikuwa gereza la kisaikolojia, Ni vigumu sana kuelewa jinsi mtu anaweza kupitia unyanyasaji wa kisaikolojia hadi kupoteza mawazo yake muhimu”
Rae anasema kwake, ni mateso ya kisaikolojia ambayo yameacha makovu makubwa zaidi, TB Joshua alimpa adhabu ijulikanayo kama “adobe” kwa miaka miwili, ambapo alikatazwa kutoka nje ya boma, na hakuna mtu ndani aliyeruhusiwa kuzungumza naye.

“Kimsingi nilitengwa kabisa, nilikuwa na shida kamili,” Nilijaribu kujiua mara tano lakini sikufanikiwa, nilisubiri Mchungaji TB Joshua aliposafiri na kanisa katika ziara nchini Mexico, ndipo Nikatoroka na sikuwahi kurudi tena ” Amesema Rae

Baada ya kuzungumza na mashuhuda hao wote BBC wakafanya jitihada za kutafuta ukweli kutoka upande wa Scoan, lakini wamekanusha madai hayo dhidi ya TB Joshua.
“Kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Nabii TB Joshua si jambo geni… Hakuna madai yoyote yaliyowahi kuthibitishwa,” wamejibu Scoan.

Mtume TB Joshua ni miongoni mwa wachungaji waliowahi kujizolea umaarufu mkubwa na hata baada ya kifo chake kanisa lake ambalo kwa sasa linaongezwa na mjane wake Evelyn limeendelea kupata waumini kutoka maeneo mbalimbali ya dunia.

TB Joshua alifariki Juni 6, 2021 saa chache baada ya kumaliza huduma kanisani kwake siku ya Jumamosi, amewahi kuitembelea Tanzania mwaka 2015 kwenye kipindi cha uchaguzi mkuu, ambapo alifanya mazungumzo na aliyekuwa mgombea wa Urais wa Chadema, Edward Lowassa na mgombea wa CCM, John Magufuli.