Computer generated 3D photo rendering.

Na Alex Kazenga

Dar es Salaam

Idara za mikopo katika baadhi ya benki zilizopo nchini zinatupiwa lawama kwa kuwa na wafanyakazi wasio waaminifu wanaozitumia kutapeli mali za watu.

Baadhi ya wakopaji na wadhamini akiwamo Mohammed Kipanga ambaye ni mkazi wa Tabata, Dar es Salaam amelithibitishia Gazeti la JAMHURI kuwapo kwa utapeli wa aina hiyo huku wahusika wakidaiwa kulindwa na Sheria ya Mikataba Na. 345 ya mwaka 1963.

Kipanga ambaye kwa sasa hana makazi ya kuishi, anasema anapitia kipindi kigumu kutokana na maofisa mikopo wa benki (jina la benki linahifadhiwa kwa sasa) kushirikiana na madalali wa kampuni (jina la kampuni linahifadhiwa) kuuza nyumba yake kwa njia za kitapeli.

“Sakata langu lina muda, lilianza zamani, ni la tangu mwaka 2007 nilipokubali kuweka nyumba yangu kama dhamana ili rafiki yangu apate mkopo benki,” anasema Kipanga.

Anamtaja Gaston Mahimbo kuwa rafiki yake aliyefika katika benki hiyo na kuomba mkopo wa Sh milioni tano lakini akapewa sharti la kuwa na wadhamini wenye mali zisizohamishika.

Baada ya kupewa sharti hilo, anasema kuwa Gaston alimfuata na kumuomba nyumba yake itumike kama sehemu ya dhamana ili aweze kupewa mkopo huo.

“Kwa sababu tulikuwa tunafanya biashara pamoja sikusita, bila kumshirikisha mke wangu nilimkubalia na kumpatia leseni ya makazi itumike kama nyaraka inayowakilisha umiliki wa nyumba yangu.

“Niliambatana naye hadi tawi la benki hiyo lililopo Kariakoo, akanikutanisha na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Claud Ngelesa aliyedai kuwa ni mjomba wake na mfanyakazi katika benki hiyo. Pia akasema yuko tayari kuwa mdhamini wa Gaston ili apate mkopo haraka,” anasema Kipanga.

Baada ya wote kukubaliana kumpa dhamana, anasema Gaston alijaza fomu za mkopo huo huku nyumba ya Kipanga ikitumika kama sehemu ya dhamana kwa mdhamini namba mbili na Claud akiweka dhamana ya gari aina ya Starlet na pikipiki aina ya Honda vikiwa ni mali za mdhamini namba moja.

Anasema mkopo aliopewa Gaston alitakiwa kurejesha ndani ya miezi 12 pamoja na riba yake, lakini baada ya kufanya biashara kwa miezi mitano tu akashindwa kufanya marejesho.

Anasema wakati huo Gaston alikuwa amefanya marejesho ya jumla ya Sh milioni 2.8, hali iliyomfanya kuikimbia biashara na kuamua kukitelekeza kiasi cha mkopo uliokuwa umebaki.

“Nilipigiwa simu na kuelezwa kuwa tuliyemuwekea dhamana amesitisha kupeleka marejesho benki, nikashituka, ikabidi niende nyumbani kwake alikokuwa amepanga. 

“Nilivyofika kwake niliambiwa amehamia Magomeni, nikaanza kujiuliza anahamaje bila kunipa taarifa?” alihoji Kipanga.

Anasema alivyomfuatilia hadi Magomeni alikoelekezwa kwamba amehamia alikutana naye kisha akamueleza kuwa asiwe na hofu kwa sababu amehama ili apate sehemu nzuri ya kufanyia biashara zake.

Pia anasema siku chache mbele alipewa taarifa kuwa Gaston ameuza vitu vyote vya ndani na amerejea nyumbani kwao Uyole, mkoani Mbeya.

Kutokana na Kipanga kuweka dhamana ya nyumba yake, anasema ilibidi afanye jitihada za kumsaka ili arudi kumalizia mkopo wake.

Anasema alimtafuta hadi Mbeya kwao lakini akaambiwa kuwa amekimbilia Malawi na hata baada ya kusafiri hadi nchini humo katika eneo aliloelekezwa hakufanikiwa kumpata.

“Nilirejea nchini, nikiwa Mbeya nikaambiwa kuwa Gaston amejificha sehemu moja inaitwa Mgeta iliyopo Ifakara, mkoani Morogoro.

“Pale kuna kituo cha Masista wa Kanisa Katoliki, napo nilifika lakini nikaambiwa hajafika. Nikiwa Morogoro mke wangu, Naima Mlawa, alinipigia simu na kunieleza kuwa benki imeuza nyumba yetu,” anasema.

Kipanga anasema kuwa mke wake alimtaarifu kuwa nyumba yao imeuzwa Sh milioni tano na benki walikuja na mtu aliyenunua nyumba hiyo ni Peter Shayo.

“Aliniambia kuwa wameacha notisi ya siku 14 tuwe tumeondoka katika nyumba yetu na kumpisha mtu ambaye ameinunua.

“Nilifika nyumbani kweli nikakuta uamuzi wa kuuza nyumba yangu umefanyika, ikabidi niwaulize viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Tabata Msimbazi Magharibi wakaniambia hata wao hawakupewa taarifa kama kuna nyumba inauzwa,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, anasema alikwenda Mahakama ya Mwanzo Ilala lakini akaambiwa suala hilo alipeleke Mahakama ya Ardhi kwa sababu kuna utapeli ndani yake.

Kabla ya kwenda mahakama hiyo, anasema alifika benki ambayo Gaston alichukua mkopo na kumueleza meneja wa tawi hilo kilichotokea.

Anasema meneja wa tawi hilo alishitushwa na taarifa hizo lakini na utaratibu uliotumika akasema umekiuka kanuni na sheria za utoaji mikopo.

“Meneja wa tawi aliniambia hawakamati mali za wadhamini bila kuwashirikisha. Alinihoji kama waliouza nyumba nawafahamu, nilimujibu kuwa sikuwapo,” anasema.

Baada ya kupata maelezo yake, anasema meneja huyo aliwaita maofisa wanaohusika na utoaji mikopo na kuwahoji kama kuna nyumba wameuza na walikiri kufanya hivyo.

Anasema alipowahoji kama wanamfahamu, walidai hawamfahamu. Ndipo meneja huyo akamtambulisha Kipanga kwao na baada ya wao kumtambua wakamuomba atoke nje ya ofisi ili wazungumze.

Baada ya mazungumzo hayo, Kipanga anasema aliitwa na kuelezwa kuwa meneja hakushirikishwa katika uuzwaji wa nyumba hiyo, huku akimueleza kuwa suala hilo alifikishe makao makuu ya benki hiyo akaliripoti kwa maofisa wa juu.

Anasema hata alipolifikisha makao makuu ya benki hiyo alielezwa kuwa amefanyiwa utapeli huku wakimtaka kufungua kesi mahakamani ili kuwashitaki wahusika.

Baada ya maelezo ya benki hiyo, anasema aliifuata kampuni ya udalali iliyoshiriki kuuza nyumba hiyo nao wakakana kutoshiriki uuzwaji huo.

Anasema alipotaja majina ya wafanyakazi waliodai kushirikiana nao mkurugenzi wa kampuni hiyo aliwaita nao wakakubali kuwa wameshiriki uuzaji wa nyumba hiyo.

Hata hivyo, anasema akamtaka kutoripoti sakata hilo mahakamani huku akimuahidi kuwa atawasiliana na wengine ili waone namna ya kulimaliza pasipo kufikishana katika vyombo vya sheria.

Anasema alirejea kwa meneja wa tawi hilo na kumueleza hatua alizofanya ndipo akamshauri kukaa meza moja na mnunuzi ili amrudishie gharama zake za ununuzi na nyumba ibakie kuwa yake kama ilivyokuwa hapo awali.

Anasema benki walimueleza kuwa katika gharama za mauzo ya nyumba yake imebaki Sh 1,200,000 na wako tayari kuirejesha kwake, hivyo, atafute Sh 3,800,000 waliyoitumia katika matangazo na usafiri wakati wa kwenda kuuza nyumba hiyo ili akamilishe fedha anayopaswa kulipwa mnunuzi.

Kipanga anasema alikubaliana na ushauri huo na meneja wa tawi hilo akampigia simu mnunuzi wakakubaliana siku ya kukutana kwa ajili ya kukabidhiana fedha hizo.

“Nilitafuta fedha hizo nikafanikiwa kuzipata. Siku nazileta benki ili tumkabidhi mnunuzi, yeye alipiga simu kwa meneja na kudai kuwa hayuko tayari kupokea Sh milioni tano kwa sababu ametumia gharama kubwa kupata nyumba hiyo.

“Alisema amewapa zaidi ya Sh milioni 15 maofisa mikopo wakagawana na madalali ndipo wao wakakubali kumuuzia nyumba ya Kipanga kwa bei ndogo,” anasema Kipanga huku akibainisha kuwa thamani ya nyumba pamoja na kiwanja ni zaidi ya Sh milioni 50.

Baada ya kutokea sintofahamu hiyo, anasema meneja huyo alitamka kujiondoa katika sakata hilo na kudai suala hilo lipelekwe mahakamani.

Kipanga kupitia wakili wake anasema alifungua kesi katika Mahakama ya Ardhi na Nyumba wilayani Ilala Na. 195 ya mwaka 2008 akiwashitaki  watu watano ambao ni meneja wa tawi hilo, Gaston Mahimbo (mkopaji), Claud Ngelesa (mdhamini wa kwanza), kampuni ya udalali (jina linahifadhiwa) na Peter Shayo (mnunuzi wa nyumba hiyo).

Anasema hukumu ya kesi hiyo ilitoka mwaka 2016 lakini alishindwa na kukata rufaa mara mbili ambapo zote ameshindwa pia.

Akizungumzia kilichomtokea Kipanga, mmoja wa maofisa waandamizi wa makao makuu ya benki hiyo, anasema kilichofanywa na tawi la benki yao ni kwa mujibu wa sheria ya mikataba Na. 345 ya 1963.

Anasema sheria hiyo imeweka wazi kuwa mtu anapomdhamini mkopaji anakuwa na majukumu sawa na yale ya mkopaji wa awali pindi inapotokea deni halijalipika.

Pia anasema wakiwapo wadhamini zaidi ya mmoja na mkopo ukashindwa kulipika, mdai anaweza kushika na kuuza mali ya mdhamini yeyote ili kufidia deni.

Naye wakili aliyesimamia kesi ya Shayo anasema sakata hilo linatokana na uelewa mdogo alionao Kipanga.

“Tumepoteza muda mwingi mahakamani kutafuta uhalali wa kuuzwa kwa nyumba, sasa huko kote amepigwa, sasa hivi ametolewa kwenye nyumba ameanza kutapatapa tena?” anahoji wakili huyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.

By Jamhuri