*Ni yule anayetuhumiwa kwa

 mauaji ya mfungwa Liwale

*Adaiwa kupelekewa kitanda cha

 futi tano kwa sita alalie gerezani 

*Askari magereza walalamika kulazimishwa 

kumpigia saluti wakati ni mahabusu 

Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam

Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Liwale, Gilbert Sindani, amedaiwa kupelekewa kitanda chenye ukubwa wa futi tano kwa sita kwa ajili ya kukilalia wakati akiwa katika mahabusu ya Gereza la Mkoa wa Lindi anakoshikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya mfungwa Abdallah Ngatumbara.

Taarifa za uhakika kutoka vyanzo mbalimbali vilivyopo gerezani hapo na vilivyozungumza na Gazeti la JAMHURI kwa nyakati tofauti hivi karibuni, vimedai Sindani ameomba kupelekewa kitanda hicho cha mbao aina ya mkongo alichokuwa analalia nyumbani kwake Liwale.

Mbali na kitanda hicho, pia chanzo kimoja kimedai kuwa Sindani amepelekewa runinga na kufungiwa dishi lake peke yake kwa ajili ya kuangalia vipindi mbalimbali vya televisheni.

“Katika Gereza la Mkoa wa Lindi kuna ‘special wing’ au tunaiita ‘condemn’, hii ni mahabusu maalumu kwa wafungwa wanaosubiri kunyongwa, kwa sasa pale gerezani wafungwa wanaosubiri adhabu za kunyongwa hawapo.

“Kwa hiyo Sindani akapelekwa katika mahabusu hiyo ya wafungwa wanaosubiri kunyongwa na amepewa chumba cha peke yake, yaani anakaa peke yake lakini akaomba apelekewe kitanda alichokuwa anakilalia nyumbani kwake na kweli amepelekewa. Pia amepelekewa runinga yake na kafungiwa dishi lake kwa ajili ya kuangalia mambo mbalimbali,” kimedai chanzo hicho.

Chanzo kingine kimedai kuwa baadhi ya askari magereza wanaofanya kazi gerezani hapo nao wanalalamika kulazimishwa kumpigia saluti Sindani wakati akiwa katika mahabusu hiyo.

“Kuna mambo ya kulindana yanaendelea. Hata kama Sindani ni Mkuu wa Gereza la Liwale lakini kama amekuwa ni mahabusu hapa gerezani ni lazima sheria zifuate mkondo wake.

“Tunamshangaa (anamtaja jina) anatulazimisha tumpigie saluti Sindani wakati yeye ni mahabusu, ukishakuwa mahabusu hata kama ulikuwa ni mkubwa huko uraiani, lakini ukiwa humu ndani lazima sheria na taratibu za magereza zifuatwe kama inavyotakiwa,” kimedai chanzo hicho. 

Vilevile chanzo kingine kimedai ni jambo la ajabu kulazimishwa kumpigia saluti Sindani kwa sababu tafsiri ya kitendo hicho ni kama kumheshimu mahabusu kwa kumpa salamu ya kijeshi.

“Kitendo cha kulazimishwa kumpigia saluti Sindani kinatukwaza, yaani haiwezekani askari magereza ampigie saluti mahabusu, hiki kitendo hakiwezekani na huko ni kuvunja sheria zetu za magereza,” kimedai chanzo hicho.

Julai 3, 2022, Mkuu wa Gereza la Mkoa wa Lindi, Fadhili Donile, amezungumza na JAMHURI kwa njia ya simu lakini ameshindwa kukiri au kukanusha madai hayo yakiwamo ya Sindani kupelekewa kitanda gerezani.

“Hilo jambo siwezi kulizungumzia kwa sasa. Kwanza, kesi iko mahakamani, kwa hiyo siwezi kuzungumza chochote,” amesema Donile.   

Sindani na askari magereza wawili; Sajenti Yusuph Selemani na Koplo Fadhili Mafowadi, wamefikishwa gerezani hapo kwa tuhuma za mauaji ya mfungwa huyo yaliyotokea hivi karibuni baada ya kufikishwa mahakamani.

Watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani mkoani Lindi baada ya JAMHURI kuripoti hivi karibuni kifo cha Ngatumbara ambaye pia ni mnyampala mwenye namba 70/2020 kilichotokea Juni 8, 2022 na mwenzake Siaba Mbonjola mwenye namba 76/2021 kujeruhiwa kwa kipigo wakilazimishwa kuwataja askari magereza walioiba mahindi ya Sindani.

Pia JAMHURI limeripoti hivi karibuni habari kutoka kwa vyanzo mbalimbali kuwa akiwa mahabusu katika Gereza la Mkoa wa Lindi, Sindani, anadaiwa kutumia simu yake ya mkononi kuwasiliana na watu walioko nje.

“Hakuna sheria inayoruhusu mtuhumiwa aliyeko mahabusu kukaa na simu au mawasiliano ya aina yoyote, wala kufanya mawasiliano ya simu na watu walio nje ya gereza bila kibali cha bwana jela.

“Hili linafanyika kwa Sindani, ameingia na simu mahabusu, anaitumia kuwasiliana na watu. Tunajiuliza, jeuri ya kumiliki simu akiwa mahabusu anaitoa wapi? Ipo shaka kwamba huenda anatumia simu hiyo kuwasiliana na vigogo wanaosadikiwa kuwa karibu yake ili wamsaidie kujinasua katika kesi hiyo,” kimedai chanzo kingine.

Juni 26, 2022, Donile, amezungumza na JAMHURI kwa njia ya simu na akakiri Sindani kufanya mawasiliano ya kiofisi baina yake na anayekaimu nafasi ya Mkuu wa Gereza la Liwale kwa ajili ya kumpa maelekezo.

“Sindani naye ni mfungwa kama wafungwa wengine, haijalishi ni ‘convicted’ au ni ‘un convicted’. Naye tunamsikiliza kama tunavyowasikiliza wengine.

“Siku analetwa hakujua kama hatarudi tena, tulimpatia simu awasiliane na ndugu zake, hii haki ya kuwasiliana na ndugu si kwake tu ni kwa hata wafungwa wenzake, hata wao tuliwaruhusu kuwasiliana na ndugu zao na kuwapa taarifa kuhusu walipo na namna ya kuwatunzia mali zao,” amesema.

Donile amesema suala la Sindani kufanya mawasiliano akiwa mahabusu gerezani halina tatizo, wala haliwezi kuharibu uchunguzi unaoendelea kwa sababu tukio likiwa na jinai ndani yake huwa halina namna ya kulikwepa.

“Mambo ya kiupelelezi yana hatua zake, kuhusu kuwasiliana na watu ni lazima, kwa sababu ndiye alikuwa anafahamu masuala ya fedha ya kule alikokuwa na hata utawala, sasa katika mazingira aliyochukuliwa aliyeachwa ni lazima ahitaji maelekezo yake,” amesema.

Vilevile amesema naye analazimika kumpelekea simu mara kwa mara mahabusu kwa ajili ya kufanya mawasiliano.

Sindani na wenzake wamekamatwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa mahakamani hivi karibuni baada ya taarifa za kifo cha mfungwa huyo na kujeruhi mwingine.

Sajenti Yusuph na Koplo Fadhili walikamatwa siku chache baada ya kutokea kwa kifo cha mfungwa huyo na kumjeruhi mwingine aliyenusurika kifo baada ya kuwahishwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) alikolazwa kwa takriban wiki tatu sasa akipatiwa matibabu katika wodi ya wagonjwa walio katika uangalizi maalumu (ICU).

Safari ya Mbonjola kufika Gereza la Liwale inaanzia Kisarawe ambako Desemba 10, 2015 Mahakama ya Wilaya ilimhukumu kifungo cha miaka 30.

JAMHURI limeripoti hivi karibuni kwamba linafahamu kifo cha Ngatumbara kimetokea baada ya yeye na mpambe wake kutembezewa kipigo na askari magereza, wakilazimishwa kuwataja watu walioiba mahindi ya Sindani.

Awali, wafungwa hao walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Liwale ambako wataalamu walithibitisha kifo cha Ngatumbara na baadaye Mbonjola akahamishiwa Hospitali ya Mkoa ya Sokoine na kisha kupelekwa MOI.

Inadaiwa kuwa wizi wa mahindi ya Sindani ulitokea wakati wafungwa wakivuna kutoka katika shamba la magereza.

“Mahindi yaliyoibwa yalikuwa yamekusanywa barabarani tayari kusombwa na magari kupelekwa ghalani na mengine kwa Afande Sindani ambaye siku hiyo alikuwa safarini Dar es Salaam.

“Akatumiwa taarifa za kuibwa kwa mahindi yake yaliyovunwa. Aliporejea Liwale, akamuita msaidizi wake na kuhoji juu ya taarifa za wizi. Akajibiwa kuwa zipo lakini hazikuwa zimefanyiwa uchunguzi,” amesema mtoa taarifa mwingine aliyezungumza na JAMHURI hivi karibuni.

Amesema hadi wakati huo hakukuwa na yeyote anayetuhumiwa kwa sababu hakuna aliyebainika kupelekewa au kukutwa na mzigo wa mahindi.

Taarifa hizo hazikumridhisha Sindani, ambaye kesho yake, Juni 8, 2022 akawaita nyampala (Ngatumbara) wa gereza na mpambe wake (Mbonjola) na kuwataka wampe taarifa kamili lakini wakamjibu kuwa hawajui chochote.

“Palepale akaanza kuwapiga akiwataka wamtaje aliyechukua mahindi na amechukua kiasi gani. Alipochoka, akaona haitoshi, akawaita askari wawili; Sajenti Yusuph na Koplo Fadhili wamsaidie kuwapiga hadi watakapotaja wezi,” amesema.

Mtoa taarifa huyo amesema kuwa kipigo hicho hakikuwafurahisha askari wengine ambao waliwazuia Sajenti Yusuph na Koplo Fadhili wasiendelee kuwapiga, wakihoji iwapo kama wana uhakika kweli kuna wizi umetokea; wengi wakiamini kuwa uchache wa mavuno ya mwaka huu ndiyo sababu ya kudhani kwamba wizi umefanyika.

Pia amesema baada ya Sindani kubaini kuwa wafungwa hao wameumizwa sana, akaondoka kisha muda mfupi baadaye akarudi na kuwapakia katika gari kuwapeleka hospitalini ambako madaktari walibaini kuwa tayari Ngatumbara alikuwa ameshafariki dunia huku  matumaini ya kupona kwa Mbonjola ni madogo.

Amesema madaktari wakashauri tukio liripotiwe polisi na kupewa ‘PF3’ ili taratibu za matibabu kwa Mbonjola zifanyike.

Ndugu wa Ngatumbara aliyezungumza na JAMHURI hivi karibuni, Said Mohamed, amesema awali taarifa kuwa mfungwa huyo ana hali mbaya walizipata kutoka kwa mtu wasiyemfahamu, aliyewaeleza kuwa amemuona Hospitali ya Wilaya ya Liwale.

“Muda mfupi baadaye tukapigiwa simu na Diwani (Nassoro) akatueleza kuhusu tukio hilo. Siku ile afya yangu haikuwa nzuri, hivyo nikampigia simu Kassim Arafi (ambaye ni ndugu yake) nikamwambia aende hospitalini kuhakiki taarifa,” amesema.

Anasema alipofika hospitalini, Arafi, alizuiwa kumuona Ngatumbara kwa maelezo kuwa akatafute kibali kutoka kwa Mkuu wa Gereza.

Kutokana na kizingiti hicho, Arafi, aliamua kuulizia taarifa za ndugu yake kutoka kwa watu wengine, ndipo akaelezwa kuwa alifikishwa hospitalini akiwa na mfungwa mwingine, lakini yeye amefariki dunia.

Kutokana na utata wa taarifa na kwa kushauriana na diwani, Mohamed na ndugu zake wakaona ni vema kuwasiliana na mkuu wa wilaya aliyewataka wafike ofisini kwake siku inayofuata.

“Tukaenda kuzungumza naye. Akakiri kuwa anazo taarifa za tukio na kuwa amewasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi atume vyombo vya dola kufanya uchunguzi.

“Siku iliyofuata tukaitwa na Mkuu wa Gereza akisema tunahitajika kwenda Kipule liliko gereza tukapate maelekezo. Sisi tukamwambia hatuna usafiri. Akatutumia gari. Mimi, Arafi na Omari Mchite tukaenda gerezani ambako tuliwakuta maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama,” amesema.

Miongoni mwa maofisa waliokuwapo ni Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Lindi na Sindani akawaeleza ndugu wa Ngatumbara kuwa kifo cha ndugu yao kimetokana na shinikizo la damu (pressure).

Mohamed anasema walipohoji zaidi, wakaelezwa kuwa katika gereza hilo kuna kawaida ya kutokea wizi wa mahindi na mara nyingi wafungwa wanapoyasomba kutoka shambani hupotea.

“Sindani akadai kuwa askari wasimamizi ndio watekelezaji wa aina hiyo ya wizi. Akatuambia kuwa siku ya tukio yeye alikuwa amesafiri, akamuacha msaidizi wake afuatilie wizi wa mahindi unaofanywa na askari magereza kwa kushirikiana na wafungwa,” amesema.

Aidha, amesema Sindani mbele ya maofisa wengine kutoka mkoani, akawaambia kuwa aliporudi alipewa orodha ya askari wanaohusika, lakini hakutaja majina yao.

Amesema Sindani akaendelea kusema kuwa kesho yake aliitisha gwaride rasmi likijumuisha wafungwa wote na askari magereza, na kutamka kuwa wezi wa mahindi wamekwisha kufahamika, akiwataka kutorudia tabia hiyo.

Baada ya onyo hilo, amesema Sindani alipanda gari lake na kuelekea mjini na wakati akiwa njiani ndipo akapigiwa simu na msaidizi wake kumpa taarifa za Ngatumbara kuzidiwa, kupelekwa zahanati, na kwamba walikuwa wanaomba kibali apelekwe Hospitali ya Wilaya.

“Akasema kuwa msaidizi wake alitoa kibali, Ngatumbara akapelekwa hospitalini. Nako hali ikazidi kuwa mbaya hadi akafariki dunia,” amesema Mohamed.

By Jamhuri