Makubaliano ya msingi kati ya Marekani na Iran yenye lengo la kumaliza vita yameanza rasmi kutekelezwa baada ya kutiwa saini kidiijitali na marais wa nchi hizo mbili. Hayo ni kwa mujibu wa maafisa wa pande zote mbili.

Kwa mujibu wa msemaji katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, rasimu ya mwisho ya makubaliano hayo imekamilika na sasa imeanza kufanya kazi rasmi.

Kwa upande mwingine Ikulu ya Marekani White House nayo imedokeza kuwa Rais Donald Trump amesaini makubaliano ya awali ya kuongeza usitishaji vita kati yake na Iran kwa siku 60, na kuweka msingi wa kuufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz sambamba na kuanzishwa kwa majadiliano juu ya programu yake ya nyuklia.

Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amesema kupitia mtandao wa X kwamba Marekani na Iran zote mbili zimesaini makubaliano hayo na pia zimemtambua kama mpatanishi katika mchakato huo.

Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimeripoti kuwa hakutakuwa na hafla rasmi ya kutiwa saini nchini Uswisi siku ya Ijumaa kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Siku ya Jumatano, Marekani na Iran zilichapisha rasimu ya makubaliano yao ya kumaliza vita katika eneo la Mashariki ya Kati, ambapo Tehran ilikubali kupunguza kiwango cha urutubishaji wa madini ya urani, huku ikiruhusiwa kuanza tena kuuza mafuta.

Marekani kwa upande wake imeahidi kulegeza baadhi ya vikwazo na kusaidia kuanzishwa kwa mfuko wa dola bilioni 300 kwa ajili ya ujenzi mpya wa Iran. Kulingana na nyaraka hizo, ujenzi huo utaungwa mkono na mataifa ya kanda hiyo, mara tu makubaliano ya mwisho kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yatakapofikiwa.

Hata hivyo, Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuwa hatua kali zinaweza kuchukuliwa iwapo Iran itakiuka masharti ya makubaliano hayo.