WASHINGTON, MAREKANI

Shirika la Anga za Mbali la Marekani (NASA) limepanga kurusha vyombo viwili kwenda kwenye Sayari ya Venus.

Shirika hilo limetangaza hivi karibuni kuwa limepanga kufanya safari mbili zitakazofanyika katika kipindi cha miaka 30 ijayo.

“Safari hizi mbili zinazohusiana zote zinalenga kujua ni kwa nini Sayari ya Venus ina joto kali katika uso wake linaloweza kuyeyusha hata madini ya risasi. Tunaamini kuwa taarifa tutakazokusanya zitawasaidia wanasayansi kupata taarifa za kufanya uchunguzi wa kina wa sayari hiyo ambayo hatujawahi kuiangalia kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita,” anasema Bill Nelson, Msimamizi wa NASA.

“Tunatarajia kuwa safari hizi zitatusaidia kujua jinsi dunia ilivyotokea na kwa nini ina mazingira yanayoweza kukaliwa na viumbe wakati sayari nyingine katika mfumo wa jua tunamoishi hazikaliki,” anaongeza.

Chombo kimoja cha safari za anga za mbali kiitwacho DAVINCI+, kitakusanya taarifa kuhusiana na hali ya anga la sayari hiyo linalozungukwa na wingu zito la hewa za carbon dioxide na sulfuric acid.

Chombo kingine kilichopewa jina la VERITAS, kitapiga picha na kutengeneza ramani za ardhi ya sayari hiyo na kujaribu kuunda historia ya utengenezwaji wake.

Vyombo hivyo vimeshinda kufanya safari kwanza mbele ya vyombo vingine viwili ambavyo vimepangwa kusafiri hadi kwenye mwezi wenye volcano wa Sayari ya Jupiter uitwao Io

au katika mwezi wa Sayari ya Neptune, Triton.

Safari hizo mbili za kwenye miezi ya sayari nyingine ndizo zilizokuwa zimepewa kipaumbele katika uchunguzi wa anga la mbali na NASA.

Tangazo la safari hizo limewavutia wanasayansi kadhaa ambao wanaamini kuwa Venus ni sayari iliyosahaulika kutokana na kutofanyiwa utafiti kwa kipindi kirefu.

Venus ni sayari inayofanana sana na dunia kwa ukubwa na ujazo, na ingawa leo hii haikaliki inaaminika kuwa awali ilikuwa na mazingira yaliyowawezesha viumbe kuishi juu yake.

Wanasayansi wanaamini kuwa sayari hiyo ilikuwa na joto la wastani na mazingira mengine kama vile bahari.

Hivyo, kuelewa ni nini kimesababisha sayari hiyo kubadilika na kuwa na joto kali kutasaidia kujua tabia za sayari zinazofanana nayo, ikiwamo dunia.


Mwonekano wa Sayari ya Venus kwa mbali.
859 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!