Imeelezwa kuwa kuna adhabu zilizowekwa kwa makosa ambayo hayapo wazi kinyume na Ibara ya 13 (6)(C) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambacho kinachangia wadau wa habari kupiga kelele kubadilishwa kwa baadhi ya viungu vya sheria ya habari.

James Marenga, wakili wa kujitegemea (kushoto) akimkabidhi flash yenye mapendekezo ya mabadiliko ya sheria za habari Lilian Timbuka, Mhariri wa Gazeti la Mwananchi.

Akizungumza na wahariri wa magazeti ya Mwananchi leo,wakili wa kujitegemea James Marenga ambaye pia anawakilisha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), amesema kuwa sheria hiyo kupitia Kifungu 7 (i)(g) iliyotungwa mwaka 2015, imevuruga uhuru wa faragha ambapo taarifa binafsi za mtu zinaweza kuchukuliwa na Polisi kinyume na Ibara ya 16(i) ya Katiba ya Tanzania.

“Sheria hii katika Kifungu cha 50(2)(b) kinaondoa haki ya mtu kukata rufaa kinyume na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, lakini pia Kifungu cha 38(2)(b) cha sheria hii kinaruhusu usikilizwaji wa shauri mahakamani hata bila muhusika kuwepo.

“Hukumu ikitolewa, ndio unatafutwa na kufungwa bila kujua kesi yako ilipelekwa mahakani lini, na kwa kosa gani. Ndio maana tunasehma sheria hii inatakiwa kupitiwa upya,”amesema Wakili Marenga

Wakili wa kujitegemea James Marenga (kushoto) akizungumza na wahariri kuhusiana na mapendekezo ya mabadiliko ya sheria za habari , kulia ni Samuel Kamdaya, Mhariri wa Gazeti la The Citizen na Llilian Timbuka Mhariri wa Gazeti la Mwananchi.

Wakili marenga pia amesema kuwa sheria ya habari inayohusu kashfa kuwa jinai, inakulinda pale tu kauli hiyo inayoweza kutafsiriwa kuwa ya kashfa, imetolewa bungeni ama na rais, basi.

Lakini andishi lingine lolote ambalo kama mahakama itasema ni kashfa, hapo mwandishi anaingia kwenye jinai, sasa sheria ya namna hii ya kibaguzi, haiwezi kuwa rafiki kwa wanahabari.

Wakili Marenga amezungumza na wahariri gazeti la Mwananchi Lilian Timbuka ambaye ni mhariri wa habari Mwananchi na Samuel Kamdaya, ambaye ni Mahariri wa Habari wa The Citizen wakati wa mazungumzo ya mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari nchini.

“Pamoja na kwamba mwandishi amelindwa katika kipengele hicho, lakini bado sheria hiyo hiyo haimpi kinga kama habari hiyo itakwaza viongozi wa juu. Unaweza kuandika ila inategemea itapokelewa vipi.

“Ndani ya sheria hizo kuna maeneo mwandishi anaweza kujikuta anaingizwa mkenge hata kwa nia njema ya habari aliyoiandika kwa taifa lake. Ndio maana tumeona kuna kila sababu ya kufanyia maboresho,” amesema Wakili Marenga.

By Jamhuri