Masoko kuvutia uwekezaji uwekezaji wa viwanda vya bidhaa, tiba, dawa

Na. WAF Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo imejipanga kuwavutia wawekezaji wa viwanda vya ndani vya dawa kwa kutengeneza masoko ya bidhaa tiba na dawa zitakazo zalishwa Nchini.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Oktoba 19, 2023 wakati wa kikao cha kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi kilichofanyika katika kumbi za Bunge Jijini Dodoma.

“Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuweka mazingira wezeshi ili bidhaa tiba pamoja na dawa zitakazo zalishwa na viwanda hivyo ziweze kuuzika nchini Tanzania, Afrika Mashariki na Nchi zote za ukanda wa SADC”. Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Ili viwanda vya ndani vya dawa viweze kupata soko, kwa sasa wawekezaji wa viwanda vya dawa wanasubiri mkataba wa AMA upite ili kuwavutia zaidi na waweze kuuza kwa watu zaidi ya milioni 500 wa ukanda wa SADC.

“Bado tunajukumu la kuimarisha mifumo ya kusimamia usajili na udhibiti wa bidhaa tiba za dawa ili kuweza kufikia matokeo chanya katika uwekezaji wa viwanda vya bidhaa tiba za Dawa nchini”. Amesema Waziri Ummy

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu-Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amesema nchi za Afrika zimeungana kupitia mkataba wa AMA ili kuweza kutengeneza wataalam ambao watasaidia nchi moja moja huku akiongeza kuwa wataalamu hao watapatikana kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Awali Waziri Ummy akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu, pamoja wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Afya, amesikiliza wasilisho la Maamuzi ya kamati ya Bunge ya Afya na masuala ya Ukimwi ambapo mwenyekiti wa kamati hiyo Stanslaus Nyongo amesema kamati hiyo imeridhia na imebariki Serikali kuendelea na hatua zaidi za Mkataba huo.