Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Wananchi wa Mitaa ya Zepisa A na B kata ya Hombolo,Jijini Dodoma wameilalamikia Serikali kuwatelekeza na kushindwa kuwapa huduma ya maji, umeme na miundombinu ya barabara hali inayokwamisha maendeleo.

Wamesema adha hiyo kwa muda mrefu toka mwaka 1972 hali inayokwamisha kukosa huduma za kijamii.

Wakizungumza na waandishi wa habari Dodoma kwa lengo la kufikisha ujumbe wao kwa serikali wamesema matatizo hayo hayavumiliki na kwamba yanaleta adha kwa wanafunzia na wajawazito.

“Kutokana na ubovu wa barabara wajawazito hujifungulia njiani na wagonjwa kukosa huduma usiku katika kituo cha afya cha karibu ambacho huduma hutolewa mwisho saa 9 jioni kutokana na wahudumu kushindwa kuishi hapa kwa sababu ya kukosekana kwa umeme,maji wala choo, “amesema shuhuda mmoja

Naye Ernest Mchuno mkazi wa mtaa wa Zepisa A, amesema wamekuwa wakilalamika kwa viongozi mbalimbali wanaokuja mtaani hapo kila mara kuhusu huduma hizo zinavyowatesa bila mafanikio kwa muda mrefu.

“Tunateseka hadi tunajiuliza tumemkosea nini Mungu,viongozi wa serikali wanakuja huku na magari yao mazuri mengi lakini hawafanyi chochote nyie wenyewe mashahidi mmeona barabara ile inawatesa wake zetu wakati wa kujifungua hadi kufika hospitali ile mlioina kule,cha kushangaza hapa wametujengea kituo cha afya ambacho hakina maji,sehemu ya kuchomea taka hakuna,hata choo hakuna na umeme pia hakuna, mtu akiumwa usiku hakuna pa kwenda, “amesema

Naye Mzee Emily Makasi amesema”Pamoja na waliyozungumza wenzangu lakini suala la maji ni shida sana wanawake zetu wanaenda kwenye maji saa sita usiku wanarudi saa nne asubuhi kwajili ya kisima kimoja cha maji na haya toki kama inavyotakiwa tunayasubiria na foleni ni kubwa.”

Amesema licha ya kuwa na vyoo vizuri katika shule wanaosoma watoto wa mitaa hiyo lakini wanaenda chooni bila maji huku vyoo walivyojengewa na wafadhili vinatakiwa kutumia maji mengi lakini hakuna maji hata kidogo hivyo kupelekea kuwa na wasiwasi ya magonjwa ya mlipuko kwani hali ya vyoo hivyo ni mbaya na ukiangalia watoto wanaingia bila hata ya viatu.

“Huku hata walimu wanaletwa lakini wakiangalia mazingira wanaondoka,hakuna umeme wala maji na kila mara tumekuwa tukilalamika kwa viongozi wetu wa mitaa wanafuatilia lakini hakuna majibu yakueleweka na hadi leo tunateseka halafu tupo ndani ya jiji,”amesema Mzee Makasi.

Pendo Wilson ni mwanachi wa mtaa wa Zepisa B alisema wanawake ndiyo wanaoteseka zaidi hasa wanapoumwa uchungu kwani kituo cha afya kipo mbali halafu barabara siyo nzuri imejaa mchanga kupita na pikipiki ni hatari kwa afya zao.

“Mmeona mlikopita pale sisi ndo tunapota kwenda kujifungua tunadondokea pale kwenye lile daraja na lile daraja lilikuwa ndani ya barabara lakini sasa hivi limetengana barabara ipo sehemu nyingine na daraja sehemu nyingine na imejaa mchanga,”alisema Pendo.

“Kwenye maisha kila kitu ni maji lakini siyo kwetu sisi tunaishi maisha magumu sana kwenye suala la maji tunatembea usiku kutafuta maji ni mateso,serikali tusaidieni hali ni mbaya,”

Kutokana na hayo Mwenyekiti wa Mtaa wa Zepisa B , Mussa Rashid akiongelea changamoto hizo katika mtaa wake alisema kweli limekuwa tatizo kubwa huku akiahidi kutogombea tena nafasi ya uwenyekiti wakati wa uchaguzi kama matatizo hayo hayatatuliwa kwani amechoka kuwajibu wananchi vitu visivyo na matumaini.

“Sioni sababu ya kugombea tena uenyekiti wa mtaa kama wananchi wangu wanateseka hivi bila mafanikio,kama mnavyojua wenyeviti wa mitaa hawana mishahara tumekuwa tukiuza hadi kuku wetu ili tupate nauli ya kwenda Tanesco,Rea na Tarura kwajili yakufuatilia masuala yetu bila mafanikio,”

Alisema kuwa matatizo hayo yamekuwa yakiwagombanisha wao na wananchi wao kwani wakiwaita kwenye mikutano wananchi hawaji kwasababu wanaona wanaenda kuongelea mambo yale yale yasiyotekelezeka.

Huku Mwenyekiti wa Mtaa wa Zepisa A ,Daudi Kamunya,akisema kuwa kweli changamoto hizo zipo na wao kama viongozi wa mitaa wamefutilia sana bila mafanikio lakini yeye hajakata tamaa kwani ataendelea kufuatilia kwani wananchi wanataka maendeleo na maendeleo ni huduma za kijamii kama hizo ambazo bado hawajazipata.

“Nawasihi wananchi wawe wavumilivu tunaendelea kuiomba Serikali itusaidie hizi huduma ni za lazima ndiyo maana hadi leo tunaendelea kuzilalamikia,”alisema Kamunya.

Naye Katibu wa Tawi la CCM ,Yona Dickson alisema haelewi awambie nini wananchi kwani wamepoteza imani na chama kabisa kutokana na matatizo yao kutotatuliwa kwa muda mrefu huku viongozi wakiwa na taarifa za mara kwa mara lakini hakuna vitendo.

“Oneni hizi kadi kuna jambo tunataka kulifanya linahitaji kukusanya hizi kadi lakini ninazochache wengine wamegoma kutoa wanasema sisi waongo hali hii inaumiza sana,”amesema Dickson.

By Jamhuri