Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi ametolea ufafanuzi mkopo uliotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa Serikali ya Tanzania.

Amesema Tanzania imeshapata mikopo ya masharti ya nafuu kutoka EDCF ya Korea mara kadhaa ambapo mara ya kwanza ilikuwa Dola za Marekani milioni 733 kwa kipindi cha mwaka 2014/2020 na mara ya pili ilikuwa Dola bilioni moja (2021/2025).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 4, 2024 amesema mkopo wa sasa uliotolewa  ni wa tatu na unafanya kuwa na jumla Dola bilioni 2.5 sawa na Sh trilioni 6.7 kwa ajili ya miradi ya miundombinu chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi (EDCF).

Ameongeza kuwa mkopo huo utakuwa wa riba ya asilimia 0.01 kwa muda wote wa malipo.

“Mkopo huu utakuwa wa riba 0.01 kwa muda wote wa malipo,mkopo huu kuanzia mwaka 2024 hadi 2028 na ni muendelezo wa mikopo mingine ya aina hii kutoka Korea kuja Tanzania,

Tanzania haijaweka rehani kitu chochote au mali yoyote kama inavyopotoshwa na baadhi ya vyombo vya habari na wanaojadili katika majukwaa mbalimbali ya mitandaoni na yasiyokuwa na mitandaoni” amesema Matinyi .

Matinyi amesema mbali na mkataba huo Rais Samia pia ameshuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano( MoU) mbili ambapo ya kwanza ni ushirikiano katika sekta ya Uchumi wa Bluu ambapo kutakuwa na Utafiti, Mafunzo na Miradi ya Uvuvi na pili ni kwenye madini ya kimkakati ambapo kutakuwa na utafutaji na utafiti .

Kwa mujibu wa Matinyi miradi mingine iliyotokana na ushirikiano baina ya Tanzania na Korea ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Mloganzila, uboreshwaji wa Hospitali ya Muhimbili na Daraja la Tanzanite jijini Dar es salaam.

By Jamhuri