Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Lindi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata mara moja wafugaji waliohusika katika mauaji ya watu 12 Mkoani Lindi.

Masauni ametoa kauli hiyo akiwa ameambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi katika Vijiji vya Kikole, Kipindimbi na Zinga Kibaoni Wilayani Kilwa, Mkoani humo Oktoba 31, 2022, katika ziara yao kufuatia mgogoro wa wakulima na wafugaji mkoani humo.

Amesema Serikali haiwezi kukaa kimya wakati matukio hayo ya kinyama yakiendelea na haitakubali kuona mfugaji au mkulima anavunja sheria, amani, hivyo lazima sheria ifuatwe na atakayekiukwa atashughulikiwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza katika Kikao cha Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kilwa, Mkoani Lindi wakati alipowasili Wilayani humo kwa ajili ziara ya kikazi, leo Novemba 1, 2022.

“Natoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha watu wote nchi nzima walioshiriki kuua watu wengine, ikiwemo hawa walioua wakulima katika Wilaya hii ya Kilwa na Wilaya zingine za Mkoa huu wa Lindi ambazo tunakwenda kwanza wakamtwe, ninashangaa mpaka leo hakuna mtu hata mmoja aliyekamatwa, inatutia mashaka makubwa.

“Kamishna upo hapa na RPC upo hapa hakikisheni hawa mnawakamata haraka ili iwe fundisho kwa watu wengine, haiwezekani mtu anaua raia kama anaua kuku, watu 12 wamekufa katika mkoa huu wa Lindi, hawa ni binadamu, leo ameua mmoja akamatwi, kesho kaua mwingime hakamatwi, na hata waliofanya uhalifu kuiba au kujeruhi nao wakamatwe.”

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka wafugaji waliopo katika vijiji ambavyo hawaruhusiwi kuwepo, waondoke katika maeneo hayo, waende katika vijiji vilivyopangwa kwa ajili ya mifugo.

“Nawataka wafugaji kuacha tabia ya kupeleka mifugo katika mashamba ya wakulima, marufuku kupeleka mifugo yenu katika maeneo ambayo hamruhusiwi ikiwemo katika Kijiji hiki cha Kikole, lazima utaratibu ufuatwe,” amesema Ndaki.

Naye Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Nchini, CP Awadhi Haji amesema Jeshi la Polisi litafanya msako wa nyumba kwa nyumba kuwasaka wahalifu ambao wameua watu 12 katika Mkoa huo na watakamatwa na pia amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika msako huo.

Mkazi wa Kijiji cha Kikole, Pili Mneka amesema kutokana na kifo cha mkulima mwenzao katika Kijiji hicho cha Kikole, Kata ya Kikole, Wilayani Kilwa, kimewaudhunisha na wanakosa amani kwa kuwa na uoga kutokana na wafugaji hao kufanya ukatili kwa mkulima mwenzao.

Waziri Masauni, Waziri Ndaki na viongozi wengine wanaendelea na ziara mkoani humo ambapo pia wanatarajia kutembelea Wilaya za Liwale na Nachingwea katika Mkoa huo kufuatilia matukio hayo ya mauaji ambayo yanasababishwa kwa sehemu kubwa na wafugaji.