#Apinga majungu sekta ya madini

#Dkt. Kiruswa asisitiza njia ya kufikia malengo 2030

#Mahimbali asema Wizara itasimamia kikamilifu ukusanyaji wa Maduhuli Mwaka wa Fedha 2023/2024

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amewataka Watumishi wa Wizara na Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo kushirikiana ili kuongeza ufanisi katika utendajikazi wao na hatimaye kufikia malengo waliyopangiwa.

Ameeleza hayo Septemba 14, 2023, wakati akizungumza katika Kikao cha Watumishi wa Wizara ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma.

Amesema kuwa, Wizara ina vitu vikubwa inavyotakiwa kufanya vizuri ambavyo ni Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa pamoja na kukusanya maduhuli ya Serikali zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

“Ili kufikia malengo haya mawili tunapaswa kuimarisha ushirikiano wetu kama Wizara pamoja na taasisi zote tano zilizopo chini ya Wizara, hii itatusaidia kuwa na umoja na upendo baina yetu, ndani na nje ya ofisi. Niwaeleze tabia yangu binafsi, sipendi majungu kwasababu mimi ni mhanga wa majungu, sitovumilia tabia ya kuharibiana kazi, tushirikiane kuimarisha Sekta hii” amesema Waziri Mavunde.

Aidha, amesisitiza kuwa kupitia kaulimbiu ya Maono 2030; Madini ni Maisha na Utajiri, Sekta yetu inaenda kupiga hatua kubwa na kuheshimisha Nchi kupitia rasilimali Madini na kwamba Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) itaongezewa uwezo ili kupitia Utafiti wa kina isaidie kufikia maono na malengo hayo.

“Mbali na Sekta ya Madini, taarifa hizi zitasaidia upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu na shughuli za kilimo cha umwagiliaji, malighafi za viwanda, yaani tunaenda kufunganisha Sekta ya Madini na Sekta nyingine, tutafikia malengo kwa kuwa na taarifa sahihi za kisayansi na sio kubahatisha” amesema Waziri Mavunde.

Ameongeza kuwa, Wizara imepanga kusimamia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili ifikie hatua ya kuwa miongoni mwa Shirika kubwa barani Afrika katika shughuli za mnyororo mzima wa Sekta ya Madini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa ili kufikia malengo ya maono Wizara iliyojiwekea hamna budi kuweka mipango na kutengeneza njia ya kufikia malengo.

“Ni matumaini yangu kuwa maono mazuri aliyokuja nayo Mhe. Waziri tutayawekea mpangokazi ikiwezekana hata tuwe na majumuisho ya kila mwezi, ili isionekane kuwa ni maono yaliyobakia kwenye makaratasi na sio utekelezaji, lazima kila mtu kwa nafasi yake afanye kazi kwa ufanisi wa juu ili kufikia malengo tuliyojiwekea kufikia mwaka 2030” amesema Dkt. Kiruswa.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amesema Wizara itahakikisha inasimamia ukusanyaji wa maduhuli kama ilivyopangiwa na Serikali kukusanya Shilingi trilioni moja kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 na kwamba watumishi watafanyia kazi maelekezo na miongozo waliyopewa ili kufikia malengo.

Please follow and like us:
Pin Share