Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Lindi

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa anaendelea kuisimamia timu ya wataalam na Makandarasi kurejesha mawasiliano ya barabara ya Lindi – Dar es Salaam ambapo tayari eneo la somanga limeanza kupitika na amesisitiza kuwa ifikapo kesho leo mawasiliano ya barabara hiyo yatarejea.

Bashungwa amezungumza hayo Mei 08, 2024 mkoani Lindi wakati akisimamia zoezi la urejeshaji wa miundombinu ya barabara hiyo ambayo iliharibiwa mvua za El-Nino juzi Jumamosi ya tarehe 04 Mei, 2024 zilizombatana na Kimbunga Hidaya.

“Kwa namnna tulivyojipanga tuliahidi watanzania kuwa hadi kufikia Alhamisi barabara hii tutakuwa tumerudisha mawasiliano na tayari kipande cha Somanga kilichokuwa kimekatika kwa mita 200 tumeshakikamilisha na hivi sasa nguvu zote tunazielekeza katika eneo la Songas na kuendelea katika maeneo mengine”, ameeleza Waziri Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameeleza changamoto zinazowakabili wataalam ambao wanaendelea kurejesha mawasiliano katika barabara hiyo ni upatikanaji wa mawe ambayo yanafuatwa Kigamboni na Boko-Magereza Mkoani Dar es Salaam, huku zoezi hilo likifanyika usiku na mchana.

“Lakini kwa vile zoezi hili tunalifanya usiku na mchana pamoja na changamoto hizi tumeweza kurudisha mawasiliano eneo la Somanga na nguvu hiyohiyo tunaiamisha katika maeneo mengine”, ameeleza Waziri Bashungwa.

Pamoja na hayo ameipongeza timu ya wataalamu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Makandarasi na wasaidizi wake pamoja viongozi wa Wizara na Mkoa.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amepongeza timu ya wataalam na
Makandarasi kwa kufungua eneo cha Somanga ambapo amesema ana imani na eneo la Songas napo mawasiliano yataweza kurejea usiku wa leo Mei 08, 2024.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Somanga kusini, Mustafa Omari Mkunga ameishukuru Serikali kwa kazi kubwa katika eneo la Somanga ambalo lililkuwa korofi na sasa limeweza kupitika.

Please follow and like us:
Pin Share