Na WMJJWM, Dae Es Salaam

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kupitia taasisi yake ya IMF Afritac East (AFE) imeandaa Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Mawaziri wa masuala ya Jinsia kuhusu utekelezaji wa usawa wa jinsia.

Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba amebainisha hayo katika mkutano na Waandishi wa Habari Novemba 13, 2023 jijini Dar Es Salaam.

Amesema Mkutano huo utafanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 15 hadi 17 Novemba 2023 na utahusisha Mawaziri wa Fedha na Mawaziri wa masuala ya Jinsia kutoka nchi 22.

Waziri Nchemba ameeleza Lengo la mkutano ni kutoa fursa kwa washiriki kujadili namna bora ya kushughulikia athari za mapungufu ya kijinsia katika uchumi na kuchochea ufadhili wa masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake ili kufikia malengo ya maendeleo ya kitaifa na malengo ya maendeleo endelevu.

Aidha, katika mkutano huo, Mawaziri watajikita kwenye kuangalia hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa ahadi zilizowekwa za jukwaa la usawa wa kijinsia (Generation Equality Forum) ambapo baadhi ya masuala yatakayojadiliwa ni athari za uchumi katika usawa wa kijinsia na jukumu la upangaji wa bajeti unaozingatia jinsia.

Ameendelea kusema kuwa, Mada nyingine muhimu zitakazojadiliwa katika mkutano wa mawaziri ni jinsi ya kuongeza uwekezaji ili kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia; uwekezaji kwenye teknolojia na uvumbuzi unaolenga usawa wa kijinsia na haki na usawa wa kiuchumi .

“Mkutano huu wa ngazi ya juu wa Mawaziri ni uwepo wa vipaumbele vya kuharakisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji kwa wanawake na ahadi ya kugharimia uekelezaji wake kutoka kwa washiriki na nchi husika.
Tumeiweka mahsusi kipindi hiki cha kuelekea kwenye bajeti tumewaweka pamoja Mawaziri wa Fedha na Mawaziri wa Jinsia ili masuala ya jinsia yawekwe kwenye mipango na bajeti wakati wa maandalizi.” amesema Dkt. Nchemba.

Sambamba na Mkutano huo, kutakuwa pia na warsha ya kujenga uwezo kwa wataalamu itakayojikita kwenye kujenga uelewa kwenye kuweka mipango na bajeti kwa kuzingatia usawa wa kijinsia katika Sera ya Umma.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema ni heshima kubwa kwa Mkutano huo kufanyika nchini ambapo unahusiana na masuala ya kuwekeza rasilimali kwa ajili ya maendeleo yanayogusa usawa wa kijinsia kwa sababu maendeleo yapo kwenye sekta mbalimbali.

“Tutaangalia mipango na mikakati ya sekta zote kama inazingatia usawa wa kijinsia au inabeba jinsia moja tu kitu ambacho ni tatizo kubwa kwa nchi za Afrika.

Tunashukuru sana kwa ujio wa mkutano huu kwani, unaakisi maono ya Dkt. SSH wa kuiunda Wizara hii, anachotaka sasa ni kuona mipango yetu inaelezea maono yake kwamba katika sekta fulani, mipango na mikakati ya kila mwaka inaakisi mizania ya kijinsia.” amesema Dkt. Gwajima.

Mkutano huo unahusisha nchi za Burundi, Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eritrea, Ethiopia, Guinea, Ivory Coast, Kenya na Liberia. Nchi nyingine ni Madagascar, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Senegal, Somalia, Afrika Kusini, Rwanda, Sudan ya Kusini, Uganda, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zambia and Zimbabwe.

By Jamhuri