Mbunge aandaa jimbo lake kujitenga

MWANZA

Na Antony Sollo

Mbunge wa Jimbo la Sengerama mkoani hapa, Khamis Tabasamu, anawaunganisha wananchi, husasan wakulima wa pamba wa jimbo hilo kujiondoa kutoka Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU).

Hali hiyo inakuja kama maono ya Tabasama kuwa hiyo ndiyo njia ya kuanzisha mchakato wa kufufua viwanda vya pamba vilivyopotea au kufa kwa takriban miaka 21 sasa.

NCU inaonekana kushindwa kukidhi matarajio ya wakulima na sasa Sengerema wameamua kuanzisha chama kipya cha ushirika kitakachokuwa mali ya wananchi.

Akizungumza na JAMHURI ofisini kwake Sengerema mwezi ulioipita, Tabasamu anasema uamuzi wa kuanza hamasa kwa wananchi kujitoa NCU unatokana na baada ya kubaini anguko la kilimo cha pamba na kifo cha taratibu cha vyama vya ushirika katika maeneo anayoyaongoza, hata eneo zima la Kanda ya Ziwa; suala ambalo halikubaliki.

Wakizungumza na JAMHURI, wadau wa pamba katika kanda hii pamoja na vyama vya ushirika kwa ujumla, wanasema kuanguka kwa vyama hivyo ni matokeo ya kuanzishwa kwa soko huria nchini na Serikali ya Awamu ya Tatu iliyokuwa ikiongozwa na Rais Benjamin Mkapa.

Vyama hivyo vilitetereka baada ya Serikali ya Awamu ya Tatu kuruhusu wanunuzi binafsi wa pamba, wanaodaiwa kuwakatisha tamaa wakulima kutokana na kununua zao hilo kwa bei ya chini tofauti na ilivyokuwa imezoeleka awali.

“Wakulima wakashindwa kuendeleza kilimo cha pamba kutokana na kupewa bei duni. Lakini pia kulikuwa na njama za baadhi ya viongozi na wafanyabiashara waliokuwa na masilahi yao, huku wakiwa katika mfumo wa serikali,” anasema mmoja wa wadau hao.

Sasa, Mbunge wa Sengerema, Khamis Tabasamu, anaeleza kusikitishwa kwake na namna wananchi walivyokatishwa tamaa kujishughulisha na kilimo cha pamba, hivyo baadhi ya miundombinu kama majengo yaliyokuwa yakitumiwa na vyama vya ushirika kutelekezwa, kuchakaa na kuua ajira za maelfu ya wananchi.

“Nimesikitishwa sana kuhusu namna zao hili linavyopotea huku kukiwa na unyanyasaji kwa wananchi wa jimbo langu. Hali hii imedumu kwa takriban miaka 21 tangu viwanda vya kuchambua pamba vizimwe; yaani viache kufanya kazi.

“Sasa mimi na wasaidizi wangu tunaelekeza nguvu katika kuendesha mchakato wa kujitoa NCU na kuanzisha chama kipya cha ushirika kitakachowanufaisha wananchi wote kwa pamoja,” anasema Tabasamu.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kutokana na serikali kushindwa kuvisaidia vyama vya ushirika, kumesababisha uchakavu mkubwa wa miundombinu na majengo yaliyosheheni mashine za kuchambua pamba, ambapo serikali ingeweza kusimamia vyama vya ushirika maelfu ya ajira za wanachi zingerejea na kuleta matumaini mapya.

JAMHURI limemtafuta Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Sengerema, Mark Makoye, ili kuzungumzia maoni ya mbunge wake kuhusu mchakato wa kujitoa Nyanza Co-operative Union na kuanzisha chama kipya.

Kama ilivyotarajiwa, mwenyekiti huyo ameunga mkono mawazo ya Tabasamu akiamini kuwa huo utakuwa mwanzo wa nuru ya maendeleo kwa wilaya nzima ya Sengerema.

“Ni mtazamo mzuri kabisa na mimi kama mwenyekiti na msemaji wa CCM ndani ya wilaya hii, ninaunga mkono mawazo ya mbunge wetu. Ni mazuri sana!

“Chama cha Ushirika Mkoa wa Mwanza kipo kwa miaka mingi sana lakini ukiangalia utendaji wake haufanani kabisa na umri wake. Chama hiki kimeshindwa kuwaletea maendeleo wananchi, hasa wakulima wa pamba si Sengerema pekee, bali hata kwenye maeneo mengine,” anasema Makoye.

Pamoja na hayo, Makoye anaishauri serikali kufanyia kazi na hata kuyaunga mkono kwa kiasi kikubwa mawazo ya Mbunge wa Sengerema ili kuleta mapinduzi ya kilimo cha pamba nchini.

“Mbunge wetu amekuja na mawazo ya kujiondoa NCU; chama kikongwe na cha zamani sana nchini ambacho kimeshindwa kukomaa na kuonyesha dhamira ya kweli katika kuwasaidia wakulima.

“Matokeo yake kumekuwa na changamoto kubwa kwa wakulima na zao lenyewe. Hivyo naishauri serikali kufanyia kazi mawazo ya Mbunge wa Sengerema ili kuleta mapinduzi ya kilimo cha pamba,” anasisitiza Makoye.

Anaendelea kufafanua akisema NCU inatazamwa na jamii kama chama chenye lengo la kuwanufaisha wachache na kushauri kuwa ufanyike utafiti utakaopima mawazo ya Mbunge Tabasamu na ingawa hana hofu nayo hata kidogo, basi yakionekana yanafaa utekelezaji uanze mara moja.

“Zitazamwe sheria (za Ushirika) zinasemaje.  Hili likifanyika hakutakuwa na hofu ya kuwapo migogoro inayoweza kujitokeza baadaye Sengerema itakapojitenga kutoka NCU,” anasema.

JAMHURI limezungumza na mmoja wa watumishi wakongwe wa Idara ya Uhasibu katika vyama vya msingi Katwe na Katoma, Levin Ng’weli.

Mkongwe huyo akizungumzia hoja ya Mbunge wa Sengerema kuanza mchakato wa kuiondoa wilaya au jimbo lake NCU, anasema huenda huu ndio muda muafaka wa kutekeleza mawazo ya kimapinduzi kama hayo.

“Nina uzoefu mkubwa katika masuala haya ya ushirika. Kwa sababu historia inaonyesha kwamba vyama vya ushirika vilianza miaka ya 1950.

“Kwa miaka mingi kulikuwapo wizi uliokuwa ukifanywa na wanunuzi wa pamba ambao walikuwa ni wafanyabiashara wenye asili ya Asia.

“Ni wakati huo ndipo wananchi walipoanza kuhamasishana wao kwa wao kuanzisha mchakato wa kupata chama chao wakiamini kuwa hatua hiyo ndiyo itawaletea maendeleo na mafanikio katika kilimo cha pamba” anasema Ng’weli.

Aidha, anasema kuwa mazingira hayo yaliwapa hamasa wananchi wakaamua kuunda vyama vya ushirika na Chama Kikuu cha Ushirika kilichokuwa kinajumuisha vyama vya msingi vya ushirika kilikuwa kikijulikana kama Victoria Federation of Cooperative Unions.

“Chama hiki kilipata ufanisi mkubwa na kuwapa wananchi heshima kubwa pamoja na kuiona thamani ya mazao na malipo yao yakawa malipo halali.

“Victoria Federation of Co-operative Union kikawa ni chama kikubwa kuliko vyama vyote! Ikawa ni taasisi tajiri kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo katika miaka ya 1970, serikali ilianza kuleta mabadiliko makubwa kwa kuunda Mamlaka ya Pamba na baadaye kulikuwa na mfumo madhubuti wa kusimamia ununuzi wa zao la pamba ambapo ufanisi huu ulitokana na usimamizi mzuri kutoka kwa wanachama,” anaeleza.

Katika kipindi hicho hicho cha miaka ya 1970 serikali ilibadilisha mfumo na kuwafanya wanachama kuwa ni wale tu ambao watakuwa wakiishi katika eneo hilo na tayari uuzaji wa zao la pamba kupitia mfumo huu ukawa hauna udhibiti ndipo yakawa ni matokeo ya pamba hewa kikawa chanzo cha kutetereka kwa vyama vya ushirika.

Serikali katika kipindi kifupi baadaye ikaleta utaratibu mpya kwa kusimamisha vyama vya ushirika na ununuzi wa zao la pamba ukafanywa na Bodi ya Pamba na baada ya muda mfupi serikali ilishindwa kusimamia ufanisi, jambo lililosababisha watu kuwa na madeni makubwa na baadaye serikali ilibaini kuwa ilikuwa imefanya makosa kusimamisha vyama vya ushirika.

Mwaka 1984 serikali ikarudisha tena vyama vya ushirika vikaanza upya lakini katika kuvirudisha upya vyama vya ushirika serikali haikurudisha masharti yote yanayofanya ushirika usimame imara kwa sababu bado ununuzi wa pamba uliendelea kuwa wa holela.

Mambo yaliendelea kuharibika hasa kipindi ambacho serikali iliruhusu soko huria na wanunuzi binafsi ambapo hapo ndipo mwanzo wa kuuawa kwa vyama vya ushirika na kwamba mkopeshaji ambaye alikuwa ni Benki ya CRDB kipindi hicho ilianza kutoa kipaumbele kwa kuwapatia fedha wanunuzi binafsi ambao hawakuwa na dhamana, jambo ambalo ni ubadhirifu.

Akiendelea kufafanua, Ng’weli alisema wanunuzi hao ambao hawakuwa na dhamana walikuwa wanapewa fedha kwa ajili ya kununua pamba msimu unapofunguliwa tu, huku vyama vya ushirika vikiwekewa vikwazo na kuwa Loked kwa kutopatiwa fedha kwa wakati huku vikipewa masharti magumu.

Ng’weli anafafanua kuwa vitendo hivi vilisababisha watu binafsi kununua pamba kwa zaidi ya miezi miwili ndipo vyama vya ushirika vikaruhusiwa kupatiwa fedha tena kwa masharti magumu na hatimaye baada ya kupatiwa fedha pamba vijijini ikiwa tayari imekwisha kununuliwa na watu binafsi, hivyo kusababisha mfumo huu kusababisha kuuawa kwa vyama vya ushirika.

Kutokana na mazingira haya, JAMHURI limeelezwa kuwa iwapo serikali itayapokea mawazo ya Mbunge wa Jimbo la Sengerema na nchi nzima kuyafanyia kazi, huenda wananchi wakawa wamepata ukombozi wao kama wadau wakubwa wa ushirika.

Haya ni baadhi ya majengo ya Kiwanda cha kuchambua Pamba cha Buyagu Ginery Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza Picha na Antony Sollo