Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini mkoani Kagera Dkt. Jasson Rweikiza Jana Jumanne Mei 14, 2024 amesimama Bungeni Jijini Dodoma kuhoji Wizara ya Maji kwanini mradi mkubwa wa maji wa Kemondo- Maruku umechelewa kuanza huku akihoji kulipwa kwa madeni ya wakandarasi ili mradi ukamilike na wananchi wake wa Jimbo la Bukoba Vijijini waanze kunufaika na maji kwenye mradi huo.

Akijibu swali la Mbunge Rweikiza, Naibu Waziri wa Maji Kundo Mathew amesema:-

“Serikali inaendelea kutekeleza miradi wa maji wa Kemondo- Maruku unaotekelezwa kwa awamu 3 ambapo awamu ya kwanza umefikia wastani wa asilimia 95 na utakamilika mwezi Juni na kunufaisha Vijiji 5 vya Rwagati, Kanazi, Katoju, Buganguzi na Minazi.

Awamu ya pili ya mradi imeanza utekelezaji na imefikia asilimia 67 na unatarajia kukamilika Septemba 2024 na kunufaisha Vijiji vya Mutayabega, Bulinda, Mulahya na Maruku na awamu ya 3 itahusisha ujenzi wa miundombinu na usambazaji maji katika Vijiji vya Kata mbili za Muhutwe na Kanyengereko na itaanza baada ya awamu ya pili kukamilika

“Kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kulisababishwa na kuchelewa kwa pampu za kusukuma maji kutoka Uturuki ambapo kwasasa zimepokelewa na kazi ya ufungaji inaendelea.” amesema Naibu Waziri wa Maji.

Mbunge Rweikiza aliongeza maswali mawili ya nyongeza ambayo ilikua ni kuhoji kuhusu lini serikali italipa madeni ya zaidi ya Bilioni 3 katika awamu ya kwanza ya mradi yaliyosababisha mradi kuchelewa pamoja na kuuliza awamu ya pili ya kupeleka maji Maruku na Kanyengereko mkandarasi alifukuzwa kwa kushindwa kazi, akahoji ni lini mkandarasi wa pili ataletwa ili kazi iendelee?

Maswali hayo yote mawili yanajibiwa na Naibu Waziri wa Maji:-

“Serikali inatambua kwamba kuna madai ya mkandarasi na tayali Wizara ya Maji tumeshawasilisha kwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo. Swali la pili ni kweli mkandarasi aliyekuwepo hakuweza kufanya mradi kwa ubora unaotakiwa na kuwa nje ya muda na serikali tumeuingiza sasa mradi huu kwenye Bajeti ya 2024/25 na hatua za manunuzi zikikamilika basi mkandarasi atapatikana na kazi ya ujenzi wa mradi itaendelea.

Aidha, Naibu Waziri wa Maji alimpongeza sana Mbunge Rweikiza kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kuomba hii miradi mbele ya Rais na Rais akaridhia kuanzishwa kwa miradi hii.

By Jamhuri