Wiki iliyopita Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limepata mkopo wa wastani wa Sh bilioni 165. Shirika limeupata mkopo huu kutoka benki na mashirika tisa ya fedha. Mashirika na benki zilizotoa mkopo huu na kiasi cha fedha walizotoa kwenye mabano ni CRDB Bank (Sh 35 bilioni), ECO Bank (Sh 20 bilioni), ABC (Sh 4 bilioni), NMB (Sh 26 bilioni), CBA (Sh 24 bilioni), TIB (Sh 22 bilioni), Azania (Sh 7 bilioni), Local Authorities Pension Fund-LAPF (Sh 15 bilioni) na Shelter Africa Company (Sh 22 bilioni).

 

Kiasi hiki cha fedha kitatumiwa katika mpango wa ujenzi wa nyumba 15,000 kati ya sasa na mwaka 2015. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema Sh bilioni 23 kati ya hizo zitatumika kwa ajili ya kujenga nyumba za gharama ndogo na kuwawezesha wananchi wengi kumiliki nyumba.

 

Katika hili sisi tunaona wala hakuna sababu ya kuuma au kuumba maneno. Tunataka sifa za pekee zimwendee Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, ambaye amekuwa na ubunifu wa hali ya juu kufanikisha mpango wa aina hii. Itakumbukwa kuwa Mchechu alipoingia NHC alikutana na vikwazo vingi. Alikuta shirika lina madeni mengi kwa kiwango cha kutokopesheka na alikuta lina wateja ambao wengi walikuwa wadaiwa sugu.

 

Ni kweli kwamba hadi sasa bado wapo wateja wanaodaiwa na NHC lakini kwa utaratibu uliofanywa na shirika wa kukusanya madeni, walio wengi wamelipa madeni yao. Ni hali hii iliyoliwezesha shirika hili kukopesheka. Mbali na mkopo huu, mwaka uliopita NHC ilifanikisha mpango wa benki nyingi kati ya hizo kuingia mkataba wa kuwakopesha wateja wenye nia ya kununua nyumba zinazojengwa na shirika hilo.

 

Chini ya mpango huu, benki inawalipa NHC kisha mteja anakabidhi benki hati ya nyumba anayonunua na yeye anaanza kulipa kidogo kidogo hadi anapomaliza mkopo anakabidhiwa hati ya nyumba. Utaratibu huu unatumika kwa kiasi kikubwa katika nchi zilizoendelea. Unamwezesha mfanyakazi wa kawaida kumiliki nyumba baada ya kulipa kidogo kidogo kwa miaka kati ya 15 hadi 20 ya utumishi wake.

 

Sisi tunasema ubunifu aliouonyesha Mchechu unapaswa kuigwa na wakurugenzi wengine. Hivi leo kuna sababu gani ya msingi kwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Shirika la Reli Tazania (TRL) au Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kuwa hoi kiasi kile? Wateja wapo, mizigo ipo, lakini kisichokuwapo ni uongozi bora. Moja ya mashirika haya tunaamini yakishilikiwa na mtu kama Mchechu, yataanza kutengeneza faida ndani ya nusu saa. Tunasema hongera Mchechu na wakurugenzi wengine igeni mazuri yake.

 

By Jamhuri