Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mohamed Mchengerwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wamekutana katika Kikao Maalum lengo ni kujadili utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kuhusu Ushirikishwaji wa Halmashauri katika kugharamia Miradi na shughuli za Ulinzi na Usalama.

Agizo hilo lilitolewa Septemba 4, mwaka huu wakati wa Hafla ya Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilichohusisha viongozi wa juu wa wizaza zote mbili pamoja na wataalamu kutoka Jeshi la Polisi na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema wamejipanga na fedha zimeshaingia na tayari askari wako mafunzoni kwa ngazi ya nyota moja na wakitoka watakua tayari kwenda kwenye kata zote nchini.

“Kama mnavyofajamu malengo ya Mhe. Rais ni kupeleka Serikali kwa wananchi, sasa kwa kutumia dhana hiyo sisi tunalipeleka Jeshi la Polisi, kumekua na malalamiko mengi ya wananchi wakati mwingine ya kubambikiwa kesi, lakini yakiwepo mahusiano mazuri itasaidia kupata taarifa mbalimbali za uhalifu’

Katika kutimiza azma hiyo Mhe. Rais ametupatia fedha za kupandisha vyeo askari kwa ngazi ya nyota moja na hivi zaidi ya askari mia mbili wanaendelea na mafunzo na tutawatawanya katika kata zote, lakini pia ametoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa pikipiki ambazo zitaenda kwa askari kata hao” alisema Masauni

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amesema ni muhimu kufanya kazi na kumsaidia Mhe. Rais na maelekezo yanayotolewa na Amiri Jeshi Mkuu ni muhimu kutekelezwa ili dhana ya kupeleka ulinzi na usalama kwa wananchi iweze kutendeka.

“Wizara yetu hii ni wizara yake mwenyewe Rais, kwahiyo akitoa maelekezo sisi tunaanza utekelezaji mara moja leo tumeshapata taarifa hii muhimu na baada ya hapa Makatibu Wakuu na timu za wataalamu kutoka pande zote mbili watakaa kujadili na kuona tunaenda vipi mbele ili kukidhi vile vigezo ambavyo Mhe. Rais anavitaka.’”Alisema Mchengerwa..

By Jamhuri