Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa watanzania kuilinda na kuitunza miradi ya miundombinu ya afya na elimu iliyojengwa na Serikali ili inufaishe kikazi cha sasa na kijacho.

Mchengerwa wito huo kwa watanzania, alipokuwa akizungumza na wananchi  wa Kijiji cha Nyamwage Kata ya Mbwara wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani rufiji pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma walio katika Sekretarieti za mikoa na Serikali za Mitaa.

“Watanzania wenzangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kutekeleza ujenzi wa miradi ya miundombinu ya afya na elimu katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo niwaombe tuilinde na kuitunza kwa manufaa yetu na kikazi kijacho,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mchengerwa amemtaka kila mtanzania kuwa mlinzi wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa nchini kwa kutoa taarifa za ubadhilifu wa fedha ili iwe na tija kwa jamii na maendeleo ya taifa.

Akizungumzia kiasi cha fedha kilichopokelewa katika Hamashauri ya Wilaya ya Rufiji, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Abdul Chobo amesema halmashauri yake ilipokea shilingi milioni 180 kwa ajili ya ukarabati wa  shule kongwe na ujenzi unaendelea vizuri ili wanafunzi wawe na mazingira rafiki ya kupata elimu bora.

Sanjari na hilo, Chobo amesema Halmashauri yake ilipokea zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu sita hivyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwawezesha walimu kupata makazi bora.

Ameongeza kuwa, walipokea fedha za Mradi wa BOOST kiasi cha shilingi milioni 916 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu, ambazo zimetatua changamoto ya msongamano wa wanafunzi darasani, wanafunzi kukaa chini na upungufu wa madarasa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyamwage Kata ya Mbwara wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani rufiji pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo.

Sehemu ya wananchi wa Kijiji cha Nyamwage Kata ya Mbwara wakimsikuliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani rufiji pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo.

Mwenyekiti wa Hamashauri ya Wilaya ya Rufiji, Mhe. Abdul Chobo akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyamwage Kata ya Mbwara wakati wa  ziara ya kikazi ya Mhe. Mchengerwa iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma katika Halmashauri hiyo ya Wilaya

Mwonekano wa Shule ya Msingi Bungu iliyojengwa kupitia fedha za mradi wa BOOST kwa lengo la kuboresha miundombinu ya elimu katika shule hiyo iliyopo Wilayani Kibiti

By Jamhuri