Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media.

Beki wa Mtibwa Sugar, Iddy Moby Mfaume amefariki dunia jana jioni Machi 05, 2023 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Thobias Kifaru amethibithisha kutokea kifo cha mchezaji huyo ambapo alitaja chanzo cha kifo chake kuwa ni mshituko.

“Jana alipata mshituko kidogo, tukampeleka hospitali ya kiwanda cha Sukari Mtibwa hapa Manungu lakini wakatuelekeza tumpeleke Hospitali ya ‘Misheni’ tukampeleka kwa uchunguzi zaidi lakini nao wakatuambia anahitaji vipimo vikubwa.

Baada ya hapo ndipo tukampeleka Benjamin Dodoma na kufika saa 7 usiku, akapokelewa vizuri na vipimo mbali mbali vikaendelea na leo jioni ametutoka na sasa tunafanya taratibu za mazishi.”amesema kafuru

Kwa mujibu wa daktari wa Hospitali ya Kampuni ya Mtibwa Sugar, Khalid Sabuni, Mobby alipata tatizo la kiafya Machi 4, 2023 mkoani Morogoro wakati akiwa katika mazoezi binafsi ya kutembea kuelekea mchezo wao wa ASFC dhidi ya KMC.

“Akiwa anaelekea uwanjani, alianza kupata tatizo la kuumwa kichwa, kisha alisikia kizunguzungu na kutaka kuanguka lakini alipiga magoti,”amesema Dkt. Sabuni

Dkt. Sabuni amesema, Mobby alipelekwa katika hospitali hiyo ya kampuni, na kisha hospitali ya Bwagala kwa ajili ya matibabu zaidi lakini ilipofika usiku hali ilikuwa mbaya na hivyo kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma.

“alifika Dodoma usiku lakini kufikia mchana wa leo akawa amefariki.” alisema Dkt. Sabuni.

Iddy alisajiliwa Mtibwa Sugar msimu huu akitokea Ruvu Shooting lakini aliwahi pia kuzichezea timu za Geita Gold, Polisi Tanzania, na Mwadui FC kwa nyakati tofauti na pia aliwahi kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

By Jamhuri