Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi kukumbushana misingi ya uongozi na taratibu za utendaji kazi Serikalini kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo.


Rais Samia amesema hayo leo wakati akifungua Mkutano wa Faragha (Retreat) wa Mawaziri na Makatibu Wakuu uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa (AICC)


Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa Viongozi hao kuwa na uelewa wa pamoja wa mtazamo na mwelekeo wa Serikali juu ya masuala mbalimbali.


Vile vile, Rais Samia amewataka VĂ­ongozi hao kutumia Mkutano huo kukumbushana na kuelekezana juu ya kutimiza ipasavyo wajibu walionao na dhamana walioibeba ya kuwatumikia wananchi.

Viongozi mbalimbali wakiwemo, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Watoa Mada wakiwa kwenye Mkutano wa Faragha uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) tarehe 02 Machi, 2023.


Rais Samia pia amesema umakini na umahiri unahitajika kwa Viongozi katika kutumia na kusimamia rasilimali watu, vifaa na fedha za umma pamoja na kuwa na mipango na mikakati thabiti ya kutekeleza na kusimamia majukumu yao.


Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka Viongozi hao kuyasemea mafanikio ya Serikali yaliyopatikana na kuwa wepesi kusahihisha kwa wakati upotoshaji unaofanywa dhidi ya Serikali kupitia watumishi na vitengo vya Habari vya wizarani.


Mkutano huo ambao unafanyika kwa mara ya kwanza tangu Rais Samia aingie madarakani, una lengo la kuwakumbusha Viongozi kuhusu dhana ya uongozi na sifa za kiongozi bora na utaratibu wa utoaji wa maamuzi ya kisera ndani ya Serikali.

Viongozi mbalimbali wakiwemo, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Watoa Mada wakiwa kwenye Mkutano wa Faragha uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) tarehe 02 Machi, 2023.

By Jamhuri