Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,nDodoma

Matumizi sahihi na salama ya mifumo ya kieletroniki Serikalini, yametajwa kuwa suluhisho la kudumu katika kuziba mianya ya upotevu wa rasilimali za serikali ikiwemo mapato yatokanayo na vyanzo mbalimbali nchini.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati akipokea na kuzindua Mfumo wa Kieletroni wa Kuratibu Ununuzi wa Mafuta Serikalini, ujulikanao kama ‘GPSA Intergrated Management Information System’ (GIMIS), kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene.

Amesema kuwa, matumizi ya mifumo imara ya kielektroniki yanasaidia kuondoa mianya ya upotevu wa rasilimali za Serikali na kudhibiti watumishi wasio waadilifu, kwa kuwa malipo yote ya serikali yatalipwa kupitia njia sahihi na salama katika taasisi husika.

“Tukifanya kazi kupitia mifumo ya kielektroniki tunapunguza makosa mengi ya kibinadamu, hivyo matumizi sahihi ya mifumo hii yatatuwezesha kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wetu ikiwa ni pamoja na eneo la ukusanyaji wa mapato mbalimbali ya serikali”, alifafanua Dkt.Mwigulu.

Akieleza kuhusu mfumo huo Dkt. Mwigulu amesema kuwa, mfumo wa GIMIS unatumiwa na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), ambapo kwa sasa majukumu yote ya Wakala yanatekelezwa kupitia mfumo huo ambao umesaida kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha, Dkt. Mwigulu ameelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kuhakikisha inaunganisha mfumo wa Manunuzi Kielektroni (NeST) na mfumo wa GIMIS kwa kuwa, mfumo huo unatumiwa na Wizara, Mashirika ya Umma, Wakala, Ofisi za Mikoa na Halmashauri za Wilaya nchini katika kupata huduma za GPSA.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alisema kuwa, lengo la mfumo huo ni kurahisisha utendaji kazi wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), katika uuzaji wa mafuta Serikalini, ili kuweka uwazi na kutunza kumbukumbu za matumizi ya mafuta katika kila taasisi ya umma.

Amesema kuwa, hadi sasa zaidi ya taasisi nunuzi 7070 zinatumia mfumo huo ambapo, taarifa za matumizi ya mafuta kwa kila taasisi zinatunzwa katika mfumo huo na kusaidia katika uandaaji na usimamizi wa mipango ya bajeti ya ofisi, pamoja na udhibiti wa matumizi sahihi ya mafuta kwa taasisi za umma.

“Lengo la mfumo huu ni kuhakikisha matumizi sahihi ya mafuta kwa taasisi za umma na kuokoa fedha zilizokuwa zikipotea kutokana na kutokuwepo kwa kumbukumbu sahihi za matumizi ya mafuta”, alisisitiza.

Ameongeza kuwa, kupitia mfumo huo, Serikali inaweza kufahamu kiasi cha mafuta yaliyotumika na yaliyobaki, magari yaliyopatiwa mafuta, muda, mahali na tarehe na hivyo kuziwezesha taasisi husika kuweza kudhibiti matumizi ya mafuta ikiwa ni pamoja na kuondoa udanganyifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watumishi wasiokuwa waadilifu.

Aidha, katika utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuunganisha mifumo ya TEHAMA Serikalini, Simbachawene amesema kuwa, Mfumo huo umekwishaunganishwa kwenye mfumo mkuu wa Serikali wa kuwezesha mifumo kubadilishana taarifa (GovESB).

Ameongeza kuwa tayari mfumo huo umeshaanza kubadilishana taarifa na mifumo ya baadhi ya Taasisi za Umma kama vile mfumo wa kukusanya mapato ya Serikali (GePG) pamoja na mfumo wa Usimamizi wa Rasilimali za Taasisi (ERMS).

Mfumo wa GIMIS umesanifiwa na kujengwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).

By Jamhuri