Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam.
Madereva wa mabasi ya masafa marefu na malori katika baadhi ya mikoa nchini wameendelea kugoma leo Septemba 29, 2026 wakipinga wanachodai kuwa ni faini kubwa,kukatwa pointi kwenye leseni, kufungiwa leseni pamoja na kulazimishwa kurejea shuleni baada ya kurejeshewa leseni.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya mabasi kusitisha safari katika vituo mbalimbali vya mabasi nchini huku abiria wakikumbana na usumbufu na kulazimika kusubiri kwa muda mrefu au kurejea nyumbani.
Katika Kituo cha Mabasi Msamvu mkoani Morogoro mabasi yaliyokuwa yamepangwa kuanza safari saa 12:00 asubuhi kwenda mikoa mbalimbali hayakuanza kupakia abiria. Mabasi yaliyoonekana kuondoka kituoni hapo ni yale yaliyokuwa yamewasili kutoka safari za masafa marefu na kumalizia safari Msamvu.
Baadhi ya madereva na wafanyakazi waliokutwa kituoni hapo walikataa kuzungumza na waandishi wa habari huku waliozungumza kwa masharti ya kutorekodiwa wakisema walilazimika kuwaruhusu baadhi ya abiria waliokuwa wakitarajia kusafiri kurejea nyumbani wakihofia magari yao kushambuliwa endapo wangeendelea na safari.
Walisema wao ndio wenye dhamana ya magari wanayoendesha pamoja na usalama wao na mali zilizokabidhiwa kwao.
Madereva hao wanadai kuwa moja ya sababu kuu za mgomo ni mfumo wa pointi unaohusishwa na leseni zao pamoja na faini wanazodai kutozwa na askari wa Usalama Barabarani.
Kwa mujibu wa madereva hao baadhi ya makosa yanaweza kusababisha dereva kutozwa faini inayofikia hadi Sh1 milioni huku hatua nyingine zikihusisha kusimamishwa leseni, kupunguziwa pointi na hatimaye kupokonywa leseni.
Wamedai kuwa baada ya kurejeshewa leseni baadhi yao hutakiwa kurejea shuleni kabla ya kuruhusiwa kuendelea na kazi hali wanayosema inawaathiri kiuchumi kwa kuwa bila leseni hawawezi kuendelea na majukumu yao ya kikazi na kifamilia.

Hali kama hiyo imetokea pia katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Mbezi jijini Dar es Salaam ambako madereva wa mabasi yaendayo mikoani wameripotiwa kusitisha safari huku abiria wakikaa muda mrefu kituoni wakisubiri hatma ya safari zao.
Katika Stendi ya Mabasi ya Magufuli jijini Dar es Salaam baadhi ya madereva wameeleza kuwa wamechoshwa na faini wanazodai kuwa ni limbikizi, kukatwa pointi, kufungiwa leseni pamoja na kurejeshwa darasani.
Mmoja wa madereva aliomba Serikali kuingilia kati suala hilo akisema mfumo huo unaathiri maslahi ya madereva na shughuli za usafirishaji nchini.
Kwa upande wake Meneja wa Stendi ya Mabasi ya Magufuli, Isack Kasebo amesema kinachoendelea ni mgomo, huku akieleza kuwa hajafahamu chanzo chake wala anayesimamia mgomo huo.
Mkoani Dodoma, mabasi yaliyokuwa yakitoa huduma kutoka Stendi ya Nanenane kwenda mikoa mbalimbali yalisitisha safari asubuhi ya leo.
Baadhi ya madereva wameeleza kuwa malalamiko yao yanahusu kukamatwa kwa magari kwa madai ya kukiuka sheria za barabarani, kufungiwa leseni kwa kile wanachodai kufanyika kinyume cha utaratibu, pamoja na madai dhidi ya baadhi ya askari wa usalama barabarani.
Baadhi ya abiria wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro huo, wakisema kusitishwa kwa safari kumevuruga mipango yao ya kusafiri na kuendelea na shughuli zao.
Mkoani Mara, madereva wa mabasi yaendayo mikoani na wilayani pia wamesitisha safari, huku baadhi yao wakikataa kuzungumza na waandishi wa habari kwa madai ya kuhofia usalama wao.
Wakati huo huo mkoani Mbeya, Mkuu wa Mkoa Jumanne Sagini akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa SACP Benjamin Kuzaga, amefanya mazungumzo na madereva katika jitihada za kumaliza mgomo huo.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamewataka madereva kuendelea na safari huku wakieleza kuwa malalamiko yao yanaweza kushughulikiwa.
Hata hivyo madereva wameendelea kusisitiza madai yao wakieleza kuwa wanahitaji suala la kukatwa pointi kwenye leseni zao lishughulikiwe kabla ya kurejea kazini.
Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya SSP Notika Kilewa, pia amewataka madereva kusitisha mgomo na kuendelea na safari akieleza kuwa katika baadhi ya mikoa huduma za usafiri zinaendelea.
Akizungumza leo Septemba 29, 2026, SSP Kilewa amesema madereva wanapaswa kurejea kazini ili huduma za usafiri ziendelee huku madereva wakieleza kuwa bado wanaendelea na vikao vyao vya ndani kujadili suala hilo na kwamba wataendelea na safari baada ya kufikia muafaka.

Hata hivyo wakati mazungumzo yakiendelea katika baadhi ya maeneo Jeshi la Polisi Tanzania limetoa onyo kwa mtu au kundi lolote linalohamasisha au kushiriki katika vitendo vya kuzuia mabasi na malori kuendelea na safari.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne Septemba 29, 2026 Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania, CP Awadh Juma amesema ni kosa kisheria kumzuia dereva kutoa huduma au kufanya vitendo vya hujuma dhidi ya vyombo vya usafiri na abiria.
CP Awadh amesema Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kuzuia magari au kufanya kitendo chochote kinachokiuka sheria dhidi ya mabasi, malori, madereva au abiria.
Aidha, amezungumzia taarifa zinazohusu mfumo wa alama kwenye leseni za madereva, akisema mfumo huo bado haujaanza kutumika na kuwaonya wananchi na madereva kutokubali kuongozwa na taarifa anazoeleza kuwa ni propaganda zinazozagaa mitandaoni.
Amesema usalama umeimarishwa na kuwataka wamiliki wa magari pamoja na madereva kuendelea kutoa huduma bila hofu.
Pamoja na kauli hiyo ya Polisi, mgomo huo umeendelea kuathiri usafiri katika baadhi ya vituo na mikoa, huku jitihada za mamlaka za kuwarudisha madereva kazini zikiendelea.
Abiria ndio wanaoendelea kuwa waathirika wa moja kwa moja wa hali hiyo, kutokana na kusitishwa kwa safari na kutokuwa na uhakika wa muda ambao huduma za usafiri zitaanza tena kwa utaratibu wa kawaida.



