Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Afrika haiwezi kuendelea kubaki kuwa soko la teknolojia zinazozalishwa kwingine, bali inapaswa kujenga uwezo wa kuzalisha teknolojia na bunifu zake, kukuza vipaji na kujipambanua kuwa kitovu chenye ushindani katika ubunifu na uwekezaji.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 29 Septemba 2026, wakati akifungua Maonesho ya Teknolojia na Akili Unde (Tech and AI Expo Zanzibar 2026), katika Hoteli ya Golden Tulip Airport, Zanzibar, sambamba na uzinduzi wa Sera ya Kidijitali ya Zanzibar 2026 (Zanzibar Digital Policy 2026), inayolenga kutoa mwelekeo wa mageuzi ya kidijitali Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi amesema mageuzi ya teknolojia yanatoa fursa kubwa kwa Afrika kukabiliana na changamoto za maendeleo, kuboresha huduma za umma, kupanua upatikanaji wa elimu na afya, kuongeza uzalishaji, kuimarisha biashara na kufungua fursa mpya za ajira.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejizatiti kuendeleza mageuzi ya kidijitali kwa kuwekeza katika miundombinu na mazingira yatakayowezesha wananchi, biashara na taasisi kutumia teknolojia kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Dkt. Mwinyi amesema Serikali inalenga kuunganisha kaya 100,000 na huduma za intaneti za uhakika kupitia mfumo wa Fibre-to-the-Home ndani ya miaka mitatu, sambamba na kuimarisha mawasiliano kupitia nyaya za chini ya bahari (Submarine Cable) na kuendeleza miundombinu ya vituo vya data (Data Center).
Akizungumzia Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), Rais Dkt. Mwinyi amesema teknolojia hiyo ina uwezo mkubwa wa kuongeza tija katika kilimo, afya, elimu, utalii, huduma za Serikali na biashara, lakini mafanikio yake yanahitaji miundombinu imara, taarifa sahihi na za kuaminika, wataalamu wenye ujuzi, usimamizi wenye uwajibikaji pamoja na imani ya wananchi katika matumizi ya teknolojia hiyo.
Amesema Serikali inaandaa Mfumo Mkakati wa Akili Unde (AI Strategy Framework) utakaoongoza matumizi salama na yenye uwajibikaji wa teknolojia hiyo katika uchumi na huduma za umma, huku ukizingatia faragha, usalama na haki za msingi za wananchi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inaendeleza hatua za kuweka mfumo bora wa kisheria na kisera kwa kampuni changa, wabunifu na wawekezaji wa teknolojia, pamoja na kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi na uwajibikaji katika mazingira ya kidijitali.
Amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano katika miundombinu ya kidijitali, usalama wa mtandao, usimamizi wa taarifa, utafiti, ubunifu na uhamishaji wa teknolojia ili Afrika iwe na uwezo mkubwa zaidi wa kutatua changamoto zake.
Naye Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga, amesema Serikali inalenga kujenga mazingira yatakayowawezesha vijana kutumia teknolojia na ubunifu kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali na kutengeneza bidhaa na huduma zenye uwezo wa kushindana katika masoko mbalimbali.
Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi ameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano wa Kimkakati (MoU) baina ya Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar na Huawei Technologies Tanzania Limited, iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Fatuma Mbarouk Khamis, pamoja na Bw. Tiger Liu kwa niaba ya Huawei.
Maonesho hayo yamewakutanisha watunga sera, viongozi wa sekta ya teknolojia, wataalamu wa Akili Unde, wawekezaji, watafiti, kampuni changa, washirika wa maendeleo na vijana wabunifu kutoka nchi mbalimbali, kwa lengo la kubadilishana maarifa, kuimarisha ushirikiano na kujadili nafasi ya teknolojia katika kuharakisha maendeleo ya Afrika.












