Mgonjwa wa Marburg aruhusiwa,hakuna maambukizi mapya

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema wamemruhusu mgonjwa mmoja (26) kati ya wagonjwa watatu waliolazwa katika vituo maalum vilivyotengwa kwaajili ya wagonjwa wa marburg baada ya kujiridhisha na hali yake kwa kumfanyia vipimo zaidi ya mara tatu vya ugonjwa huo.

Pia amesema Tanzania ni salama na inaendelea kuchukua hatua ya kudhibiti ugonjwa huo ambapo hadi sasa hakuna visa vipya vya maambukizi wala vifo tangu ulipotangazwa machi 21,mwaka huu katika kata mbili za Maruku na Kanyangereko Bukoba vijijini mkoani Kagera zilizoathirika.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari,Waziri huyi Ummy, alisema wagonjwa hao wawili waliobaki wanaendelea na matibabu huku mgonjwa mmoja kati yao ni mtumishi wa afya na hadi sasa hali zao zinaendelea vizuri.

Ummy alisema jumla ya watu 212 waliotangamana na wagonjwa hao wamebainishwa kati yao watu 35 tayari wamemaliza siku 21 za uangalizi bila kuonesha dalili zozote za ugonjwa huo na hivyo kuwaruhusu kutoka katika karantine na kurejea kwenye familia na shughuli zao.

”Hii ni ishara nzuri kwetu ,wizara ya afya,serikali na taifa kwa ujumla kwa kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Marburg nchini kwa wakati ila bado tunahimiza wananchi hasa wa mkoa wa Kagera kuendelea kuchukua tahadhari ,kudhibiti ugonjwa na kuzuia maambukizi mapya katika jamii,”alisema na kuongeza

”Tangu tulipotangaza uwepo wa ugonjwa huu,kutokea machi 21,2023 jumla ya visa nane na kati yao watu watano wamefariki ni jambo la kumshukuru Mungu kuwa hatujapata wagonjwa wapya,wala vifo,”alisema Ummy.

Alisisitiza endapo kutakuwa na mtu yeyote kwenye jamii mwenye dalili za homa kali,kutapika ,kuharisha ,kutoka damu na mwili kuishiwa kuhakikisha wanatoa taarifa kwa haraka kwa kupiga simu 199 bila gharama na kuepuka kumgusa mgonjwa au majimaji ya mwili wake.

”Tuendelee kuzingatia unawaji wa mikono kwa maji tiririka na sabuni ,kuosha matunda na kula chakula kilichopikwa kikamilifu,”alisema na kuongeza

”Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO),hata mgonjwa wa mwisho kupona atakaporuhusiwa hatuna budi kuendelea kuchukua tahadhari hadi tutakapojiridhisha kwamba ugonjwa umeisha,”alisisitiza.

Ummy aliwahakikishia watanzania na jamii ya Kimataifa kuwa Bukoba ni salama,Kagera ni salama na Tanzania ni salama hivyo watu waendelee na shughuli zao bila hofu yoyote, na kuendelea kuwatoa hofu kuwa ugonjwa huo ulioathiri sehemu ndogo ya mkoa wa Kagera utaisha ndani ya siku chake kwa kuzingatia miongozo ya Shirika la Afya Duniani.