Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Ifuatayo ni mada iliyotolewa na Mwandishi wa Habari Mwandamizi, Aboubakary Liongo, katika maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa lililofanyika Aprili 9, 2022 Chuo cha Uongozi Kibaha.

Ndugu zangu, wakati tunaadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ni vema tutumie fursa hii kutafakari mambo gani ya msingi ambayo Mwalimu aliyatilia mkazo na kuyasimamia kama dira yake kuu wakati wote wa uongozi wake. 

Na katika muktadha wa mjadala wetu huu wa leo, mimi ningependa kueleza kidogo juu ya mambo makuu matano ambayo naamini ndiyo alama alizotuachia. 

Katika kufanya hivyo, nitajaribu kulinganisha mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika maeneo hayo matano na namna serikali iliyopo madarakani ya Awamu ya Sita inavyoyaishi.

  1. 1. Kupinga ukabila, udini

Jambo la kwanza ambalo ningependa kusema ni suala la ukabila na udini. Mwalimu Nyerere alilijenga taifa letu kwa fikra pana sana na moja ya mambo ambayo aliyapinga waziwazi na kuhakikisha hayatokei nchini ni kuendekeza ukabila na udini miongoni mwa Watanzania. 

Katika hotuba zake nyingi alikuwa akikemea dhana yoyote ya kujaribu kutambuana kwa makabila yetu au dini zetu. Alijua kwa sababu yoyote ile kuruhusu watu kujitambua kwa makabila yao badala ya utaifa wao ni kupandikiza mbegu ya ubaguzi ambayo ikimea ni vigumu kuing’oa. 

Alikuwa akitoa mifano ya nchi jirani ambao hawakuwa wameona athari ya jambo hilo mapema na mpaka sasa dhambi hii ya ubaguzi wa kikabila inawatafuna katika nyanja zote za maisha ya kila siku. 

Katika kuhakikisha anaweka imara misingi ya kukomesha ukabila, Mwalimu Nyerere aliweka mkazo katika matumizi ya lugha ya Kiswahili na kwa makusudi akaipitisha kuwa lugha rasmi ya Watanzania. 

Na zaidi akahakikisha katiba yetu inasema waziwazi kuwa serikali yetu haina dini.

Lugha ya Kiswahili imeendelea kutuunganisha Watanzania wote mpaka leo bila kujali makabila yetu. Ni vigumu sana kumkuta Mtanzania aliyepo nchini, iwe mjini au kijijini asijue kuzungumza Kiswahili. 

Watanzania wanaongea Kiswahili kwanza, kisha lugha zao za asili baadaye. Kiswahili kinaendelea kuwa lugha kubwa inayokua na kutambulika duniani kwa sababu ya Mwalimu Nyerere kujenga misingi imara ya lugha hii.

Na zaidi katika kukemea ukabila na udini, Mwalimu alikuwa akisema waziwazi kuwa kabila au dini ya mtu haiwezi kuwa sifa ya kuchaguliwa katika uongozi. Alisisitiza viongozi wachaguliwe kwa sifa za uwezo wa uongozi na si kwa makabila au dini zao.

Hii kwa hakika ilisaidia sana kujenga taifa moja bila kujali kabila wala rangi zetu na ndiyo maana mpaka leo Tanzania bado ndiyo nchi yenye umoja, amani na upendo barani Afrika. Hata hapa tulipokaa hatujuani makabila lakini tu ndugu, na dini kwetu si tatizo kabisa.

Serikali ya Awamu ya Sita, ukabila, udini

Tunaona kwa kweli tangu Awamu ya Sita imeingia madarakani inaendelea kuishi katika maono haya ya Baba wa Taifa. Bado inaendeleza dhana ya kupinga ukabila na udini na kujenga mshikamano wa kitaifa bila kuangalia makabila yetu wala dini zetu. 

Serikali hii inajitahidi kutibu majeraha yaliyotokana na wakati fulani hapo nyuma kuonekana kama dalili za kutokufuatwa kwa misingi aliyoiweka Mwalimu kwenye eneo hili la ukabila.

Rais amekuwa akiteua wasaidizi wake bila kufuata watu wa eneo fulani au dini fulani, walau sasa yale malalamiko ya kuwa watu wa eneo fulani au dini fulani ndio wenye kushika nafasi nyingi serikalini, yamepungua kwa kiasi kikubwa.

2.  Uongozi

Mwalimu alijenga misingi imara ya kupata viongozi wanaoweza kukidhi matarajio ya wananchi kwa kusimamia maadili ya uongozi. Hakuwa na mzaha katika suala la maadili ya uongozi.

Kama mnakumbuka katika moja ya hotuba zake kwenye Mkutano Mkuu wa CCM mwaka 1995, alisema Watanzania wanataka kiongozi bora na kiongozi bora hawezi kutoka nje ya CCM. 

Alisema hili akijua ile misingi ya kuandaa viongozi kwa kuzingatia miiko na maadili ya uongozi ambayo yeye na wenzake waliiweka ipo imara.

Mwalimu Nyerere aliamini kuwa heshima ya uongozi kwa umma inatokana na kuishi kwa kuzingatia maadili ya viongozi yaliyokuwa yamewekwa. 

Haikuwa rahisi wakati wa zama za Mwalimu kukuta mtu amechaguliwa uongozi pasipo kwanza kupikwa na kuelewa misingi ya uongozi ili aweze kuwatumikia Watanzania kwa kuifuata miiko hiyo. 

Rushwa ikiwa ni adui mkubwa ambaye Mwalimu Nyerere alikemea kwa nguvu zake zote, hasa miongoni mwa viongozi.

Serikali ya Awamu ya Sita na uongozi

Ni wazi kuwa katika miaka ya hivi karibuni tumeona kukengeuka kwa serikali zetu katika kusimamia hili. Tumeona baadhi ya watu ambao hawakuwa na sifa za uongozi wala maadili yake wakipewa madaraka; na matokeo yake wakaishia kuyafinyanga, wakageuka wala rushwa wakubwa, wababe, wanyanyasaji na uhuni wa kila aina kwa kutumia nafasi zao.

Lakini sasa tunaona Serikali ya Awamu ya Sita inalifanyia kazi jambo hili na tunashuhudia mageuzi kadhaa katika suala zima la uongozi, wale ambao hawana maadili ya uongozi wamewekwa pembeni na kazi hii kama kaulimbiu ya Rais inavyosema inaendelea.

3. Ujinga, maradhi na umaskini

Mwalimu aliamini kuwa ili tuendelee ni lazima tupambane na maadui wakubwa watatu; ujinga, maradhi na umaskini. 

Alifanikiwa sana kufuta ujinga. Mnakumbuka ule mpango wa elimu ya watu wazima. Tanzania ilisifiwa duniani kwa mafanikio hayo kiasi cha kupewa tuzo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Lakini inasikitisha kuwa bado safari ya kufuta ujinga haijaisha. Kwa mujibu wa takwimu za serikali za mwaka 2018, asilimia 20 ya Watanzania walikuwa hawajui kusoma na kuandika.

Tumeshindwa kumuenzi Mwalimu katika eneo hili. Hii ni mbaya sana kuwa na idadi hiyo ya watu wasiojua kusoma na kuandika katika zama hizi za sayansi na teknolojia. Huku ni kujipalilia umaskini.

Takwimu za NECTA za mwaka 2019 zinaonyesha ni asilimia 32 tu ya wanafunzi wa darasa la pili wanaoweza kusoma kwa ufasaha na kuelewa wanachokisoma! 

Hali hii ni lazima sote tuikatae kwa nguvu kwa sababu tunajenga taifa la watumwa. Ndiyo maana watoto wetu wanamaliza darasa la saba hawajui kusoma wala kuandika. Tunajenga taifa la namna gani?

Lakini ujinga si kutokujua kusoma na kuandika tu, ila ni pamoja na kutoa elimu inayoendana na mazingira na mahitaji ya zama tulizomo. Elimu inayotolewa hivi sasa ni lazima iendane na mabadiliko ya teknolojia duniani. 

Awamu ya Sita na mapambano dhidi ya ujinga, maradhi, umaskini

Katika kukabiliana na adui maradhi, serikali zote zilizopita kwa hakika zimekuwa zikijitahidi japo si kwa kiasi ambacho kinategemewa.

Lakini jambo muhimu ambalo Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua nalo ni kuweka kipaumbele katika sekta za kijamii; elimu, afya na maji. 

Hizi ni sekta muhimu sana katika kupambana na ujinga, maradhi na umaskini. Katika historia ya nchi yetu kwa mara ya kwanza tumeona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta hizi kupitia mkopo wa masharti nafuu wa Benki ya Dunia wa kukabiliana na madhara ya ugonjwa wa Uviko-19. 

Lakini hata kabla ya mkopo huu, katika hotuba yake ya kwanza bungeni baada ya kuapishwa, Rais Samia Suluhu Hassan alisema bayana kuwa kipaumbele sasa ni katika sekta za kijamii. 

Kwa hakika huu ni mtanzamo sahihi kwa maendealeo ya taifa hasa katika zama tulizonazo.  Tunaweza kusema kuwa ni bahati kubwa kwa Tanzania kumpata Rais mwanamke kwa sababu yeye anajua uchungu na madhila anayopata mjamzito.

Ninasema hivi kwa sababu waathirika wakubwa kabisa katika sekta ya afya ni wanawake na watoto.

Sasa Rais Samia hapa amekuwa pumzi mpya katika fikra na maono ya Mwalimu kupambana na adui maradhi ambayo yamekuwa yakisababisha idadi kubwa ya vifo vya kina mama na watoto chini ya umri wa miaka mitano vinavyoweza kuzuilika. 

Bado tuna tatizo kubwa katika eneo hili na tunahitaji kuendelea kuweka nguvu kubwa hapa. Kwa kuwa kikao cha bajeti kinaendelea Dodoma hivi sasa, hamu yetu ni kuona namna gani bajeti hii ya pili ya Awamu ya Sita itazibeba sekta hizi na kuweka uwekezaji mkubwa ili kuleta maendeleo kwa Watanzania.

Ni aibu sana kuona kuwa katika karne hii ya 21 bado shule zetu nyingi za msingi na sekondari hazina huduma ya maji safi wala vyoo vya kutosha! Hili ni lazima tulirekebishe haraka.

4. Uhuru wa kuzungumza na kukosoa

Mwalimu aliliandaa taifa hili mpaka siku ya mwisho wa uhai wake hapa duniani.

Alikuwa na kaulimbiu yake kuwa vijana ni taifa la kesho, akiwaanda kuwa viongozi na kuitetea nchi yao.

Katika moja ya hotuba zake, Mwalimu alisema: “Tunataka kuona vijana jeuri katika taifa hili, wenye kujiamini na wasio waoga, yaani wale ‘ndiyo bwana mkubwa’. 

“Tunataka kuona vijana wenye ujasiri wa kuhoji na kupiga vita mifumo ya kidhalimu, isiyoshabihiana na matakwa na matarajio ya jamii ya Watanzania.”  

Mwalimu pia aliwahi kusema: “Udikteta ni serikali ya mtu mmoja au kikundi cha watu wachache ambao wao huwa ndiyo sheria. Na anayepinga watakayo wao, basi huonyeshwa cha mtema kuni.”

Huko nyuma si mbali sana tumeshuhudia haya kama taifa, tukipoteza haiba na matumaini. Hakukuwa tena na vijana ambao Mwalimu aliwataka wawe jasiri wa kuhoji, na wale waliojaribu walikiona cha mtema kuni. 

Vijana wasomi wa Chuo Kikuu ambao huko nyuma walikuwa ni vinara wa mijadala yenye chachu ya kuhoji serikali yao na kujadili mustakabali wa nchi, wote walikuwa kimya.

Ukumbi ule wa Nkrumah pale UDSM palikuwa kitovu cha mijadala motomoto ya kuchemsha fikra kwa mustakabali wa taifa, lakini sasa pamekuwa dorooooo! 

Awamu ya Sita na uhuru wa kuzungumza, kukosoa

Serikali ya Awamu ya Sita imeliona hilo na inatembea mlemle kwenye maono ya Mwalimu. Minyororo imefunguliwa hivi sasa uhuru wa kuzungumza na kuhoji upo.

Rais mwenyewe amesema wazi kabisa anataka kuongoza taifa lenye uhuru wa kuhoji na kukosoa lakini kwa kufuata misingi na sheria zilizopo. Anatibu majeraha. Analiunganisha taifa kama Mwalimu alivyotaka.

Ameruhusu uhuru wa vyombo vya habari na hata vile vyombo vilivyokuwa vimefungiwa, vingine kibabe maana wengine walishinda kesi mahakamani na kuamriwa wafunguliwe, lakini bado waliendelea kufungiwa!  

Sasa vyote viko huru na michakato ya kubadili sheria kandamizi zinazokinzana na uhuru wa habari zinapitiwa upya kwa ushirikiano na wadau ili kuishi dhana hii muhimu katika falsafa ya Mwalimu Nyerere ya uhuru wa kuzungumza na kukosoa pasipo kutukanana wala kudhalilishana, bali kwa kuzingatia sheria na utu.

Niwakumbushe kauli aliyowahi kuitoa Mwalimu alipokuwa akizungumza na watumishi wa sekta ya umma: “Nawaambieni na mnisikilize kwa makini. Utii ukizidi sana unakuwa woga. Mara zote utii huzaa unafiki na kujipendekeza.”

Rais Samia yeye juzi tu hapa alisema: “Tunasifiwa kwamba ‘adjustments’ (marekebisho) tuliyofanya Awamu ya Tano yameleta heshima ndani ya utumishi wa umma. Heshima iliyokuzwa ni ya woga. Kwa sababu kulikuwa na Simba wa Yuda ambaye ilikuwa ukimgusa sharubu anakurarua. Heshima inayotakiwa iwe ya moyoni.”

Sote tunajua tulipotoka, kwa hiyo kauli ile ya Rais Samia ni kauli au mafunzo yaliyotolewa na Baba wa Taifa miongo kadhaa huko nyuma. Tusijenge taifa la waoga, hatuwezi kufika!

5. Uhusiano wa kimataifa

Sera ya nje ya Tanzania wakati wa utawala wa Mwalimu, Tanzania ilisifika kuwa nchi iliyosimamia haki duniani.

Tanzania ilikuwa na usemi mkubwa katika masuala ya kimataifa pamoja na kuyatetea mataifa ya ulimwengu wa tatu katika majukwaa hayo. 

Tanzania Ilikuwa na sauti yenye kuheshimika katika jumuiya ya nchi zisizofungama na upande wowote; yaani ‘Non-Aligned Movement – (NAM)’ na ndani ya Umoja wa Mataifa (UN). 

Mwalimu Nyerere, pamoja na wenzake kina Dk. Kwame Nkrumah wa Ghana, Rais Ahmed Sekou Toure wa Guinea na Modibo Keita wa Mali, walishirikiana na waasisi wengine wa jumuiya hiyo; Waziri Mkuu wa India, Jawaharlal Nehru, Rais Jamal Abdel Naser wa Misri, Ahmed Sukarno wa Indonesia na  Josip Broz Tito wa iliyokuwa Yugoslavia kuzitetea nchi za ulimwengu wa tatu na jumuiya hiyo kuwa ya pili yenye nguvu baada ya UN.  

Nje ya NAM tutakumbuka mchango wa Tanzania katika kupigania China kupewa kiti UN kilichokaliwa na Taiwan. 

Kazi hiyo kubwa ilifanywa na aliyekuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania UN, Dk. Salim Ahmed Salim.

Mwalimu pia alisimama kidete kama tujuavyo katika kupigania ukombozi wa Bara la Afrika na Tanzania ikajitolea kwa hali na mali kwa ajili ya ukombozi wa bara hili. 

Vyama vya ukombozi kama Frelimo cha Msumbiji, Swapo (Namibia), ANC na PAC (Afrika Kusini), Molinaco (visiwa vya Comoro), MPLA (Angola) na Zanu na Zapu (Zimbwe) na vingine vikiungwa mkono na Tanzania.

Mji wa Dar es Salaam ulikuwa makao makuu ya Kamati ya Ukombozi ya OAU. Kwa ujumla, Mwalimu aliifanya Tanzania kuwa Makka ya vyama vya wapigania uhuru barani Afrika.

Sera ya nje ya Tanzania chini ya uongozi wa Mwalimu pia ilisimama katika kupigania mfumo mpya wa uchumi duniani chini ya kile kilichojulikana kama Kamisheni ya Kusini na Kusini (South South Commission – SSC). 

Lengo lilikuwa nchi hizi ziwe na ushirikiano wa kiuchumi baina yao na kujiondoa katika ile hali ya uchumi wao kudhibitiwa na nchi kubwa za Magharibi. 

 Mwalimu akijulikana kuwa ni ‘mjamaa’ na Tanzania ilikuwa na uhusiano mzuri na mshikamano pamoja na nchi za kijamaa za Ulaya Mashariki, ambazo ndizo zilizosimama  katika kusaidia pia ukombozi wa Bara la Afrika.

Hapa ningependa pia kukumbusha uhusiano mzuri wa Tanzania na Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) na kiongozi wake, Yasser Arafat na Chama cha Ukombozi wa Sahara Magharibi (Polisario). 

Wakati Palestina ikikaliwa na Israel, Sahara Magharibi ilitawaliwa na kukaliwa kwa nguvu na Morocco. Hali hiyo inaendelea hadi leo. Ndipo nilipogusia awali kwamba Sera ya Tanzania wakati wa Mwalimu ilisimama katika kutetea haki na kupinga dhuluma. 

Awamu ya Sita na uhusiano wa kimataifa 

Tangu Rais Samia alipochukua nafasi kuwa Kiongozi Mkuu wa taifa kufuatia kifo cha Dk. John Magufuli Machi 2021, sera ya Tanzania kuelekea nchi za nje imebadilika sana na kwa sehemu kubwa imerudi katika nafasi yake kimataifa. 

Uhusiano na nchi jirani umeimarika sawa na ule na nchi za nje hasa wafadhili ambao wamerejesha imani kwa  Tanzania. Uongozi wake umefungua milango kwa Tanzania kuwa kivutio kwa wawekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi, ukiwamo utalii. 

Kitu kimoja ninachoona kimesaidia pamoja na hayo niliyoyataja, ni kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeona ile haja ya kutoka nje kuhudhuria mikutano ya kimataifa na kadhalika, kwani hiyo ni nafasi ya kuonana na viongozi wa nchi nyingine, kufahamiana na kuzungumza ana kwa ana kuhusu matatizo ya nchi, ushirikiano wa pamoja na masuala yanayoihusu dunia. 

Nimezungumza juu ya sera ya nje ya Tanzania wakati wa Mwalimu ambayo kama nilivyosema ile ilikuwa enzi nyingine katika siasa za dunia na ilikuwa ya kutukuka. 

Na sasa kuna sera ya nje ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia ambayo ninaamini kisiasa, imeanza kuirejesha nchi mahala pake kimataifa na kiuchumi. Pia imeanza kuwa ya mafanikio ikielekea kwenye uchumi wa kati. 

Heshima hiyo inapiga hodi kila mahali kote duniani. Hata hapa kwa jirani zetu Kenya jina la Rais Samia limekuwa ajenda kwenye kampeni zao za Uchaguzi Mkuu. 

Kila mwanamke anayegombea anataka kuwa kama Mama Samia wa Tanzania.

Kwa mara nyingine ninasema kwenye eneo hili la uhusiano wa kimataifa Rais Samia amekuwa pumzi mpya ya Tanzania. 

Ndugu zangu, nadhani kwa leo itoshe kuishia hapa. Ninaamini nimesema yale ambayo kwa hakika yanamuelezea Mwalimu Nyerere katika dhamira yake halisi na ni vema sasa tukaendelea kujadiliana umuhimu wa kuendelea kuyaenzi maono yake haya. 

Nawashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuyasema haya mbele ya hadhira hii muhimu na asanteni kwa kunisikiliza.

By Jamhuri