Desemba 6, 2015 Gazeti la JAMHURI lilitimiza miaka minne tangu lilipoanzishwa tarehe kama hiyo mwaka 2011.

Wahenga walisema penye nia pana njia, na mgaa gaa na upwa hali wali mkavu! Kudumu kwenye soko lenye ushindani mkubwa wa vyombo vya habari kama ulivyo hapa nchini, si kazi ndogo.

Kwa ujasiri mkubwa tulianzisha Gazeti la JAMHURI tukiamini kuwa woga ndiyo silaha dhaifu kuliko silaha zote kwenye uwanja wa mapambano, yawe ya maisha au ya vita. Tulianzisha Gazeti hili tukiwa na dhamira kadhaa, lakini moja ilikuwa kuhakikisha tunapata uwanja mpana wa kitaaluma wa kulitumikia Taifa letu katika suala zima la kupasha, burudisha na kuelimisha.

Si hivyo tu, bali dhamira nyingine ilikuwa kupanua wigo wa ajira na kuondoa kasumba miongoni mwa Watanzania kuwa wazalendo, na hasa vijana wasiokuwa na historia ya kutoka kwenye familia zenye ukwasi, hawawezi kufanya mambo mazuri na makubwa kwa manufaa yao na kwa jamii nzima.

Kwa ujasiri mkubwa tumeweza kuwathibitishia Watanzania kuwa mtu au watu wenye dhamira njema ya kimaendeleo wakiungana na kuwa na lengo moja wanaweza kufanikiwa. Dhana ya kwamba kila chombo cha habari kinaanzishwa na matajiri au wanasiasa, ni dhana mbaya inayolenga kuwakatisha tamaa vijana. Sisi kwa umoja wetu tumethibitisha pasi na shaka kuwa kujitegemea kunawezekana kabisa.

Wakati tukiendelea na safari yetu ya kuuanza mwaka wa tano, hatuna budi kwa moyo wa dhati kabisa kuwashukuru wasomaji, watangazaji na wote wenye nia njema waliotusaidia kwa hali na mali.

Msaada wao umekuwa mkubwa kiasi kwamba leo tunaweza kutamba kuwa tupo miongoni mwa kampuni za wazalendo zinazotekeleza majukumu yake kwa ustadi mkubwa. Hata hivyo, changamoto kubwa ya uendeshaji Gazeti tumeipata kwenye fedha za kujiendesha. Suala la matangazo ni muhimu sana. Tunaomba watangazaji wasitubague.

Tahariri yetu ya kwanza tulieleza dhamira zetu zilizotusukuma kuanzisha Gazeti la JAMHURI. Tuliahidi kufanya kazi yetu ya uandishi kwa weledi huku tukiweka mbele maslahi ya Tanzania na Watanzania.

Kweli, kwa kipindi hiki tumefanikiwa kufanya kazi kubwa, tumepata tuzo kadhaa za Umahiri wa Uandishi wa Habari kutoka taasisi zinazotambulika ndani na nje ya nchi; na kwa kweli tulijitahidi kuyalinda maslahi ya nchi yetu kadri tulivyoweza.

Pamoja na mafanikio hayo, tunashindwa kujizuia kusema wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Nne haikuwa na ushirikiano wa dhati. Ama ilishindwa, au ilipuuza kabisa kuyafanyia kazi mambo mengi tuliyoyaibua tukiwa na ushaidi wa kutosha.

Kwa mfano, uuzaji wa Hifadhi za Taifa, orodha ya matapeli kwenye biashara ya madini, orodha ya wauza dawa za kulevya, wizi uliopindukia katika Wizara kama ya Maliasili na Utalii, ufujaji wa fedha za umma kupitia mikutano kama ya Smart Partnership, orodha ya majangili; magenge ya wapora ardhi, ukiukwaji wa haki za binadamu, uonevu kwa raia na mambo mengine mengi sana. Tunaamini Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, itakuwa sikivu na haitasita kuyafanyia kazi mambo yatakayoibuliwa na vyombo vya habari.

Tunawashukuru mno wasomaji na watangazaji wetu wote. Daima sisi JAMHURI Tunaanzia Wanapoishia Wengine. Endeleeni kutuunga mkono. Mungu awabariki sana.

1476 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!