Ukurasa wa 12 wa gazeti hili tumechapisha majina ya mawaziri wapya pamoja na wizara watakazoongoza. Pia wamo naibu mawaziri katika wizara kadhaa.

Mawazari na naibu mawaziri hao walitangazwa Alhamisi iliyopita. Siku hiyo walitangazwa jumla ya 30 huku wengine Rais Dk. John Magufuli akiwaweka kiporo.

Sherehe za kuwaapisha mawaziri hao zilifanyika Jumamosi mbele waandishi wa habari pamoja na viongozi wengine wa kitaifa wakiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, pamoja na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.

Hakuna ubishi kwamba Watanzania na hata watu wengine wa nchi wanaofuatilia siasa za Tanzania, walikuwa wakisubiria kwa hamu ya kujua Baraza la kwanza la Rais wa Awamu ya Tano.

Macho na masikio ya Watanzania hakika yameelekezwa kwa wasaidizi hao wa Rais ambaye Serikali yake imejipambanua kupambana na ufisadi na majukumu mengine mazito ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Katika orodha hiyo tuliyoichapisha ni dhahiri  kuwa Rais amewatambua na kuwaamini kuwa watatekeleza majukumu yao kwa kiwango kikubwa, ni kutokana na weledi.

Sura zao na taarifa zao za awali zinaonesha kwamba wengi hawana historia ya kashfa mbalimbali zilizothibitishwa hivyo ni imani ya gazeti hili na Watanzania kwamba viongozi hao watachapa kazi na kujiwekea alama nzuri mbele ya jamii huko tuendako.

JAMHURI inawapongeza wateule hao waliokula kiapo ikimiani kwamba watachapa kazi kama ilivyo kaulimbiu ya Rais Magufuli badala ya kujenga dhana kwamba wamepata “ulaji”.

Tumefurahishwa na watu kuingia kazini Jumamosi na wengine kuanza kushughulika muda mfupi tu baada ya kuapa. Tuna imani kwamba kasi hiyo itaendelea kuhitimisha dhana ya ‘Hapa kazi tu’, badala ya kujineemesha.

Mawaziri hawa hawana budi kutambua kwamba tayari Rais Magufuli na wasaidizi wake wa mwanzo walianza kazi nzuri yenye kuonesha mafanikio. Waendelee hapo.

Kabla ya mawaziri hawajateuliwa, fedha nyingi zinazokadiriwa kufikia bilioni 10.6/- zimeokolewa katika operesheni ya kuwabana wakwepa kodi katika Bandari ya Dar es Salaam, na zaidi ya watuhumiwa 40 tayari wametiwa mbaroni wakifanyiwa uchunguzi. 

Kwa hali hiyo ni imani ya gazeti JAMHURI kwamba mawaziri hao watakuwa na majukumu makubwa ya kuhakikisha vita dhidi ya maadui wakubwa waliotangazwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, rushwa, ufisadi, ubadhirifu wa aina yoyote vitakuwa ajenda.

Hakuna ubishi kwamba kama mapambano hayo yatakolezwa vema, mafanikio yake yataonekana na Watanzania watafurahjia keki ya Taifa kuliwa na kila mmoja.

Sasa kazi inabaki kwao kusimamia harakati zote za kuminya na kuziba mianya ya rushwa na kulipa mapato ya Serikali kama walivyoanza timu ya watu watatu mara baada ya kuingia Ikulu.

JAMHURI ina imani na Serikali ya Magufuli na timu yake katika kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni na pale alipokuwa akihutubia bungeni ili kuipeleka nchi mbele kiuchumi.

1153 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!