Ijumaa hii ya tarehe 9 Disemba, Watanzania penye majaliwa tutaungana pamoja kuadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara). Siku ya kukumbuka kushushwa bendera ya kikoloni ya Waingereza na kupandishwa bendera ya Uhuru ya taifa jipya la Watanganyika.

Ni siku ambayo wazazi na ndugu zetu walivua majoho na fikra za utawala wa kikoloni na kuvaa makoti na fikra ya utawala huru wa Waafrika ambao kwa karne nyingi walionewa na kuteswa kutokana na unyonge wao.

Disemba 9, 1961 ni siku ambayo haitasahaulika kwa Mtanganyika ye yote wala kwa Mtanzania kwa sababu ni siku ya Ukombozi. Ukombozi wa fikra za kiuchumi, kiutamaduni na kiulinzi. Fikra hizo njema leo zimeufikisha miaka 55 ya Uhuru kwa usalama salimini. Amin.

Katika miaka 55 ya uhuru wetu, tumepata mafanikio na changamoto nyingi katika siasa, uchumi, ulinzi na utamaduni. Viongozi waasisi wa taifa hili walijitahidi na kufaulu mno kujenga umoja na mshikamano imara na madhubuti kitaifa.

Katika mambo ya siasa tumeweza kutoa elimu ya siasa kwa wananchi na kujipanga katika kutoa na kujibu hoja za kisiasa. Ndani ya miaka hiyo, Nchi imeendeshwa katika mfumo wa siasa wa chama kimoja na mfumo wa siasa wa vyama vingi.

Katika mifumo hiyo bado hatujaiva katika kuvumiliana, kuheshimiana wala kujadiliana kisiasa kwa kuweka hoja za nguvu na badala yake tunaweka nguvu ya hoja na hatima yake tunabaki katika uharakati na kupigana vikumbo na kujengeana chuki. Tujirekebishe.

Uchumi wetu bado haujawa wa kujitegemea. Uwezo wetu wa kuendesha rasilimali zetu una mashaka kutokana na elimu tuitoayo yenye dalili ya undumila kuwili (double standards). Hatujafanikiwa katika kuelimishana umuhimu wa kulipa kodi. Taifa halijawa na mfumo wa kiuchumi wa kitaifa unaojulikana.

Pamoja na kasoro hizo na nyinginezo tumefanikiwa kiasi kuratibu na kujenga taratibu na msimamo wa kuendesha rasilimali wenyewe. Juhudi na maarifa zaidi zinahitajika kuwekwa kwenye uchumi tuondokane na umaskini.

Mshikamano na umoja wa wananchi umesaidia sana kuimarisha usalama na ulinzi wetu. Uwelewano wetu umesaidia vyombo vya Ulinzi na Usalama kuwa na lugha moja ya kitaifa ya kudumisha amani na utulivu.

Ni busara kuangalia masuala ya siasa, uchumi, ulinzi na usalama yanavyosimikwa na dhana kuu ya Utamaduni. Utamaduni wetu unapoeleweka na kuzingatiwa ipasavyo, masuala hayo huwa hayana taabu kwa sababu utamaduni ndiyo mfumo mzima wa maisha ya binadamu.

Ni mfumo unaomlea na kumjenga binadamu katika kuishi; ndiyo siasa. Kupata pato lake la siku; ndiyo uchumi. Kufikiri, kupanga na kutekeleza mambo; ndiyo ulinzi na usalama. Mambo hayo pamoja na michezo, ngoma, elimu na lugha ni vielelezo vya utamaduni.

Miaka mitano baada ya Uhuru wa Tanganyika, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliliamsha na kulielimisha taifa hili maana na muhimu wa kulinda na kuenzi utamaduni wa taifa. Nasikitika elimu na mwamsho huo haukupata mshindo wa kulindwa na kuenziwa vilivyo.

Ni nani ni mkulima, mfanyakazi, msanii, mlezi na muelimishaji, mchezaji na mfundaji, mlinzi wa shilingi yetu, mheshimu na mpenda lugha yetu na ni nani mlinzi wa taifa letu. Ukweli ni wewe na mimi wa kutambua hayo na kuelewa pasi na mashaka kuwa “Titi la mama ni tamu hata kama ni la mbwa.”

Ndani ya miaka 55 tumepoteza utamaduni wetu. Leo kuanzia kwa viongozi wetu wa nchi, vyombo mbalimbali vya jamii na wananchi tunalia na kulalama kuhusu siasa, uchumi, maadili na imani zetu zimeporomoka na haziko sawa. Sababu tumetupa utamaduni wetu.

Kwa hiyo huu si wakati tena wa kulia wala wa kiongozi kuwa mtawala. Ni wasaa kuwa na uongozi wa pamoja uliojaa ukweli na haki. Kwa makusudi turudi kwenye utamaduni wetu tupate kujenga na kuongoza nchi kwa miaka 55 mingine ijayo na iliyo tambalale.

By Jamhuri