Na Dk Ruben Lumbagala, JamhuriMedia

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametimiza miaka mitatu ya uongozi wake tangu alipoapishwa rasmi Machi 19, 2021 kuwa Rais wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.

Kufuatia kuapishwa kwake, Rais Samia aliyekuwa Makamu wa Rais wa wakati huo, akashika usukani wa kuwa Rais kamili kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kuendeleza gurudumu la maendeleo ya nchi.

Kimsingi, tangu Rais Samia aingie madarakani, amefanya mengi mazuri huku akigusa nyanja zote za maisha yaani kijamii, kiuchumi na kisiasa. Makala haya yanaangazia nyanja ya kisiasa ambapo Rais Samia ameitendea haki sana na huku akithibitisha kwa vitendo bila kuacha shaka ya aina yeyote kuwa yeye ni mwanademokrasia wa kweli kuanzia maneno hadi vitendo.

Na hii inatokana na ukweli kuwa Rais Samia anaelewa vyema umuhimu wa demokrasia katika kufanikisha agenda ya kuwaletea wananchi maendeleo. Ni katika demokrasia hiyo ambapo chama tawala kinakumbushwa vyema kuhusu uwajibikaji kupitia sauti zinazopazwa na vyama vya upinzani na hatimaye kujirekebisha na kufanya vyema zaidi kwa manufaa ya wananchi.

Chama tawala, yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina nafasi ya kufanya vyema zaidi kupitia hoja zinapoibuliwa na vyama na upinzani, na hivyo kunufaika zaidi kwa kufanyia kazi hoja hizo na hatimaye kuendelea kuongoza nchi kwani kufanyia kazi mawazo yanayotolewa na wapinzani, kunasaidia kutatua kero vinazogusa maisha ya wananchi.

Januari 3, 2023, Rais Samia akizungumza na viongozi wakuu wa vyama vya siasa vya upinzani Tanzania, alitangaza kufuta zuio na hatimaye kuruhusu tena mikutano ya hadhara.

Akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema: “Nianze na la mikutano ya hadhara, hii ni haki kwa sheria zetu. Ni haki ya vyama kufanya mikutano yao ya hadhara na kwa bahati taarifa zote mbili zimeibuka kama ni jambo muhimu sana. Uwepo wangu leo mbele yenu ni kuja kufanya ruhusa, kuja kutangaza lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoka.”

Ikumbukwe pia kuwa uhai wa vyama vya siasa ni pamoja na kuendesha shughuli za kisiasa kila siku ambapo mikutano ya kisiasa ni jukwaa muhimu la kujinadani na kuzungumzia masuala muhimu ya kitaifa ili kutafuta majibu ya pamoja kwa ustawi wa maendeleo ya wananchi.

Kutokana na zuio lililokuwepo, lilikwamisha vyama vya siasa kufanya shughuli zake kwa uhuru, na ndiyo maana Rais Samia akaondoa zuio hilo ili kutoa uwanja sawa wa siasa za ushindani kati ya chama tawala na vyama vya upinzani.

Lakini tuwe tunakumbuka kwamba zuio la mikutano lililowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano lilikuwa na sababu pia hata kama pengine zilionekana kama zinaminya demokrasia lakini zina mafunzo yake kwetu kama Watanzania.

Huko nyuma ilianza kuonekana kama nchi iko kwenye kampeni za uchaguzi muda wote! Yaani tunamaliza leo uchaguzi na kesho watu wanaanza mikutano isiyokwisha kiasi cha kutoipa utulivu serikali iliyochaguliwa na wananchi. Pia unajiuliza, wanaoandamana na kujaa kwenye mikutano, wanafanya kazi ya kuzalisha saa ngapi?

Pia kulijitokeza mtindo wa wanasiasa kuokota skendo za viongozi walioko madarakani kwenye korido, zisizo na ushahidi wowote na kuzifanya ajenda kwenye mikutano yao na baadhi ya vyombo vya habari kuzibeba zilivyo bila kuzitafutia usahihi. Ndio maana baadhi ya wanasiasa wa upinzani walijikuta mahakamani na wengine kukosa ushahidi wa madai yao huku pia baadhi ya magazeti yakifungiwa.

Lakini magazeti hayo yamefunguliwa na Samia na pia zimefanyika juhudi katika uongozi wa Rais Samia katika mazungumzo ya kutafuta maridhiano na kuachiwa kwa wanasiasa na vyombo vya sheria isipokuwa wale ambao kesi zao ni za jinai zaidi.

Pamoja na kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara ya kisiasa, haya ni mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa sambamba na wanasiasa kutumia lugha zenye staha kwenye majukwaa. Ilielezwa pia kwamba kama ilivyo nchi zilizoendelea kwenye demokrasia kama Marekani, baada ya uchaguzi, siasa zinahamia bungeni na kuwaacha wananchi wafanye kazi. Hilo ni jambo pia linalopaswa kuendelea kutufikirisha.

Kuondolewa kwa zuio la mikutano ya kisiasa kunaweka mazingira mazuri ya kuufanya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka huu 2024 na ule mkuu wa mwakani 2025 kuwa chaguzi huru na wa haki kwani vyama vyote (tawala na upinzani) vimepewa fursa sawa za kunadi sera zao kwa wananchi, na yule mwenye hoja zenye mashiko, zinazogusa maisha ya wananchi basi atapata fursa ya kuongoza na kuwatumikia wananchi kupitia sanduku la kura.

Mara kadhaa, Rais Samia amesema yeye ni muumini wa kukosolewa, hivyo vyama vya upinzani viikosoe serikali kikamilifu kwa kutumia lugha za staha na kwa kuheshimu mila, desturi, sheria, kanuni na miongozo ya nchi yetu kwani kukosolewa kunaipa serikali nafasi ya kujua changamoto zilizopo kwa ajili ya kufanyia kazi.

Katika hafla hiyo na viongozi wa vyama vya upinzani, Rais Samia alisema, “Wajibu wenu ni kufuata sheria zinavyosema, ni kufuata kanuni zinavyosema ndiyo wajibu wenu. Lakini kama waungwana wastarabu niwaombe sana, tunatoa ruhusa ya vyama vya siasa twendeni tukafanye siasa za kistaarabu, za kupevuka. Tukafanye siasa za kujenga na si kubomoa, kurudi nyuma.”

Saasa vyama vya siasa vimepata uwanja sawa wa kufanya siasa za ushindani kwa kutekeleza kwa vitendo haki ya kuandama ili kufikisha ujumbe mbalimbali. Mathalani, chama kikuu cha upinzani, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimefanya maandamano katika miji mbalibali kama vile Dar es Salaam, Arusha na Mwanza na kinaendelea na mipango ya kufanya maandamano katika miji mingine ili kufikisha ujumbe kwa serikali, huku jeshi la polisi likiilinda mikutano hiyo kikamilifu.

Vilevile, uhuru wa kujieleza kwa wananchi na kwa wanasiasa kwa ujumla ni nyenzo muhimu katika uwanja wa siasa. Uhuru wa kujieleza na kukosoa umepewa msukumo mkubwa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia kwani ni katika kujieleza na kukosoa kistaarabu na kiungwana, ndiko kunapotoka mawazo mazuri ya kujenga nchi yetu kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Wananchi wa aina zote waliosoma na wasiosoma, wanayo mawazo mazuri ambayo kama yakisikika na kufanyiwa kazi, yatachangia maendeleo ya nchi kwa kiasi kikubwa sana. Wanachama na viongozi wa vyama vya siasa nchini, wamehakikishiwa milango iko wazi wakati na muda wowote kushauri na kutoa maoni na mawazo yao ili serikali iweze kufanyia kazi kwa manufaa ya nchi.

Pia, Rais Samia amejitahidi sana kuweka mazingira wezeshi ya siasa za ushindani kupitia falsafa yake ya R4 yaani maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya. Wanasiasa wanapokuwa wameridhiana kwa pamoja na kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikiathiri mshikamano na umoja wao, ni dhahiri siasa za ushindani zitafanyika vyema.

Rais Samia mara kadhaa amefanya vikao na viongozi wa vyama vya siasa ili kujenga maridhiano, huku ustahimilivu ukihitajika sana katika kusubiria hoja zinazotolewa kufanyiwa kazi na serikali. Mageuzi katika sheria mbalilmbali yamefanyika ili kufanikisha azma ya serikali kujenga upya nchi ili kufikia maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na baadaye.

Lakini pia niwaguse wanasiasa, hususani wa upinzani kutumia haki yao ya kuzungumza kwa kuleta sera mbadala na suluhusho la matatizo yetu. Mfano, wanapolalamikia ugumu wa maisha au upungufu wa sukari, waeleze pia suluhusho la hilo.

Lakini pia watumie lugha zenye heshima na staha hasa wanapokuwa wanataja majina ya viongozi wetu wakuu. Kama kuna makosa, wawe na ushahidi huku wakitilia maanani kwamba hawa viongozi wetu ni binadamu wenye mapungufu, si malaika.

Kwa mafundisho ya Uislamu, Mtume Muhammad (SAW), aliwahi kuwaambia maswahaba zake kwamba kiongozi yeyote wa umma hasemwi kwa maneno yenye kukera mbele ya anaowaongoza hata akiwa ni dhalimu na kinachosemwa ni kweli bali hunasihiwa kwa maneno yenye staha. Mtume akafundisha kwamba hata baba ni kiongozi wa familia, ukienda kumdhalilisha mbele ya familia yake hata kama wewe ndiye mwenye haki, basi wewe ndiye unakuwa kwenye makosa.

Nihitimishe makala haya, kwa kukutakia afya nyema Rais Samia katika safari yako ya kuwatumikia wananchi ambao wana imani kubwa na wewe kuwa utasaidia kutatua kero zao na pia utasaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao ili wazidi kufurahia uongozi wako unaojali maisha ya wananchi wa aina zote.

Mungu ibariki Tanzania na watu wake wote.

Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma: Maoni: 0620 800 462

By Jamhuri