Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilitenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 50 katika bajeti ya maendeleo kwa ajili ya ununuzi wa Rada za hali ya hewa, kununua vifaa vya hali ya hali ya hewa, ukarabati wa vituo vya hali ya hewa pamoja na ujenzi wa Kituo cha Hali ya Hewa cha Kanda ya Mashariki.

Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA),imeendelea na uboreshaji wa miundombinu ya vifaa vya hali ya hewa kuendana na teknolojia na matakwa ya kimataifa ikiwemo kuondoa vifaa vyote vinavyotumia zebaki kwa kununua vifaa 15 vya kidigitali vya kupima mgandamizo wa hewa na vifaa 25 vya kidigitali vya kupima joto hewa.

Katika kuboresha huduma za usalama katika usafiri wa anga , Mamlaka imenunua vifaa vya kisasa vya hali ya hewa vitakavyofungwa katika njia ya kuruka na kutua ndege katika viwanja vya ndege vya Abedi Karume-Zanzibar, JNIA-Dar es Salaam, KIA-Kilimanjaro na Songwe.

Mamlaka ilinunua seti tano (5) za vifaa vya utambuzi wa matukio ya radi (Lighting detectors) ambavyo vimefungwa katika maeneo ya Musoma, Mwanza, Bukoba, Tabora na Kibondo mkoani Kigoma na Mamlaka imeendelea na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya hali ya hewa ikiwemo mitambo sita (2) ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe inayohamishika (mobile Automatic Weather Stations).

Kuongezeka kwa usahihi wa utabiri kumetokana na jitihada za serikali kuwekeza katika kusomesha wataalam wa hali ya hewa, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kuandaa utabiri.

Katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kwa ujumla vimeongezeka na kufikia asilimia 88.5, ambapo katika msimu wa mvua za Vuli 2022, viwango vya usahihi vilikuwa asilimia 94.1.

Viwango hivi ni juu ya kiwango cha usahihi wa utabiri kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) cha asilimia 70. Ongezeko hili la usahihi wa utabiri unazifanya huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini kuwa za uhakika na kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta zote za kiuchumi na kijamii nchini zinazotegemea hali ya hewa.

Kuongezeka kwa usahihi wa utabiri kumetokana na jitihada za serikali kuwekeza katika kusomesha wataalam wa hali ya hewa, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kuandaa utabiri pamoja na kuongezeka kwa mtandao wa vituo vya kupima hali ya hewa.

Aidha, Mamlaka imeendelea kutoa utabiri wa msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa usahihi na ubora hivyo kuchangia kupunguza athari kwa watu na mali zao.

Mfano mnamo Oktoba 2021 Mamlaka ilitoa utabiri wa msimu wa mvua za Vuli kuwa chini ya wastani.Utabiri huo uliziwezesha Mamlaka mbalimbali kufanya maamuzi stahiki na kusaidia kuepusha madhara makubwa ambayo yangeweza kutokea.

Mamlaka imeendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) katika kutekeleza majukumu ya sekta ya hali ya hewa kwa shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwemo kufuatlia mabadiliko ya hali ya hewa yanayopelekea mabadiliko ya tabia nchi.

Vituo vya kupima uchafuzi wa hewa (air pollution monitoring 20 vilinunuliwa na kufungwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuona kwa kiasi gani shughuli za kibinadamu zinavyoharibu mazingira. Taarifa za hali ya hewa pia zimekuwa zikitumika katika kufanya upembuzi yakinifu wa athari za miradi katika mazingira (Environment Impact Assessment) na hivyo kusaidia katika utunzaji wa mazingira.

Mamlaka imetumia fursa ya kukua kwa TEHAMA kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji wa huduma na pia kurahisisha usambazaji wa taarifa za hali ya hewa;

Mamlaka ilinunua vifaa na mitambo mbalimbali ya kupima hali ya hewa ambayo utendaji wake umerahisishwa kwa kutumia TEHAMA na hivyo kuweza kupima na kutuma taarifa za hali ya hewa katika Kituo Kikuu na Utabiri (CFO) vyenyewe;

Ubunifu wa watumishi wa TMA katika TEHAMA umefanikisha kuundwa kwa mifumo mbalimbali iliyorahisisha shughuli za uendeshaji na utoaji wa huduma. Baadhi ya mifumo hii ni “Meteorological Aviation Information system (MAIS)” ambao imeendelea kuboreshwa na unatumika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa usafiri wa anga.

Pia “Marine Meteorological Information System (MMIS) ambao unatumika katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu pamoja na “Digital Meteorological Observatory (DMO)”, mfumo ambao unatumika katika kurekodi taarifa za uangazi, kuzituma Kituo Kikuu cha Utabiri wa hali ya hewa.

Mifumo hii ya TEHAMA pia imeiwezesha mamlaka kutoa huduma mahsusi kwa sekta mbalimbali zikiwemo za madini, usafiri wa barabara, ujenzi na utalii.

Mifumo mingine iliyobuniwa na wataalam wa Mamlaka ni ile ya mawasiliano ya data kutoka vituoni hadi Kituo Kikuu cha Utabiri na usajili wa vituo vya hali ya hewa na “Regional Specialized Meterorological Center- Dar es Salaam-RSMC Portal” kwa ajili ya Kituo cha Kanda cha kutoa mwongozo wa utabiri kwa Nchi za Ukanda wa Ziwa Victoria;

Utekelezaji wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania

Kanuni za Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya mwaka 2019 zimekamilika katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na hivyo kuimarisha shughuli za udhibiti, uratibu na utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini pamoja na kupatikana kwa vyanzo vipya vya mapato. Ukusanyaji wa mapato utaiwezesha Mamlaka kupunguza gharama kubwa za uendeshaji kutoka serikalini sambamba na kuendeleza uboreshaji wa huduma za hali ya hewa nchini.

Katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mamlaka imefanikiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa kukarabati vituo saba (7) vya hali ya hewa vilivyopo katika mikoa ya Singida, Songwe, Mpanda, Shinyanga, Songea, Mahenge na Tabora pamoja na nyumba tatu (3 ) za wafanyakazi. Uboreshaji wa miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kilichopo Kigoma ulifanyika.

Maboresho hayo yanaenda sambamba na kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa Mamlaka kupitia mafunzo mbalimbali ya muda mrefu na muda mfupi ndani na nje ya nchi .

Utekelezaji wa Mfumo wa Udhibiti wa Ubora wa Huduma
Mamlaka imeendelea kukidhi Viwango vya Ubora vya Kimataifa katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga na hivyo anga la Tanzania kuendelea kuaminika kuwa salama.

Katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mamlaka ilifanyiwa ukaguzi wa kimataifa na Kampuni ya Certech ya Canada juu ya utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa ubora wa huduma “Quality Management Systems(QMS)” kwa mwaka 2021 na 2022 ambapo ukaguzi wa mwaka 2022 ulifanyika kuanzia tarehe 14 hadi 21 Januari 2023.

Katika kaguzi hizo ubora wa huduma zinazotolewa na Mamlaka katika seekta ya usafiri na usalama wa anga zilionekana kukidhi mahitaji ya wadau, jambo ambalo liliwezesha Mamlaka kuendelea kushikilia cheti cha ubora wa huduma tajwa cha ISO 9001:2015.

Kielelezo 7: Cheti cha Ubora (ISO) kwa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga ambacho Mamlaka ilipata baada ya ukaguzi wa mwaka 2022 uliofanyika kuanzia tarehe 14 hadi 21 Januari 2023.

Kuiwakilisha Nchi Kimataifa Katika Masuala ya Hali ya Hewa

TMA imefanikiwa kutekeleza vyema jukumu lake la kuiwakilisha nchi katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa. Wataalamu mbalimbali wa Mamlaka wameendelea kutekeleza majukumu yao katika Vikosi kazi mbalimbali vya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

TMA ilitekeleza vizuri dhamana ilizopewa kikanda na kimataifa na kufanikiwa kuitangaza vizuri TMA na Tanzania kimataifa. Wataalamu kumi na moja (11) wa TMA walioteuliwa kuhudumu katika vikosi kazi mbalimbali vya Kamisheni za WMO walishiriki vyema na kutoa mchango wa kitaalamu katika shughuli za vikosi kazi hivyo. Kutokana na ushiriki mzuri, TMA iliendelea kuaminiwa ambapo baadhi ya wataalamu walipewa majukumu ya uongozi.

Dkt. Kabelwa ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati ya WMO ya Uchakataji wa Data na Utabiri wa Hali ya Hewa “Standing Committee on Data Processing for Applied Earth System Modelling and Prediction (SC-ESMP)”. Aidha, Dkt. Pascal Waniha, ambaye ni Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Ufundi katika Mamlaka aliteuliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza wa kikosi kazi cha utekelezaji wa programu ya WMO “Task Team on Global Basic Observing Network (TT-GBON)”.

ii. TMA ilishiriki vizuri katika kutoa mchango wa kitaalamu unaohusu sayansi ya hali ya hewa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi ambao ulichangia katika maamuzi yaliyotolewa kwa manufaa ya nchi yetu. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a alishiriki kwa mafanikio katika Mikutano ya Umoja wa Mataifa ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na tabianchi, ikiwa ni pamoja na Mkutano wa 27 “Twenty-seventh session of the United Nations Framework Framework Convention on Climate Change Conference of the Parties (UNFCCC-COP-27)” uliofanyika Sharm El-Sheikh, Misri kuanzia tarehe 06 hadi 18 Novemba 2022.

Katika Mkutano huo, Dkt. Ladislaus Chang’a aliongoza vikao vya Kamati ya Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia nchi ya Ushauri katika masuala ya teknolojia “Subsidiary Body for Scientific and Technological Advice (SABSTA-57)” ambavyo vilikuwa ni sehemu ya majadiliano katika Mkutano wa COP-27. Ushiriki mzuri wa TMA uliwezesha Tanzania kuteuliwa kuwa miongoni mwa nchi zitakazonufaika na mpango wa WMO wa kuboresha uangazi wa hali ya hewa wa “Systematic Observation Funding Security (SOFF)”.

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilikuwa mwenyeji wa kongamano la 15 la watumiaji kutoka Bara la Afrika wa data na huduma zitolewazo na Shirika la Satelati za hali ya hewa la Umoja wa Ulaya “The 15th EUMETSAT User Forum in Africa (15th EUFA)”.

Kongamano hilo lilifanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania kuanzia tarehe 13 hadi 16 Septemba, 2022 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere “Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC)”.

Kongamano hilo lilifanyika kwa mafanikio na kuitangaza TMA na Tanzania kimataifa katika nyanja mbalimbali kama vile vivutio vya utalii na Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa cha Kigoma. Pia ukarimu uliooneshwa kwa wageni kupitia huduma mbalimbali walizopewa na maeneo mbalimbali waliyotembelea yaliiletea sifa nzuri nchi yetu na kuchangia katika uchumi wa nchi kupitia huduma walizotumia washiriki wa mkutano.

Hatua hiyo itachangia kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi za bara la Afrika na Bara la Ulaya.

Mashirikiano ya Tanzania na nchi mojamoja katika huduma za hali ya hewa kupitia Tume za Kudumu za Pamoja “Joint Permanent Commission (JPC) yaliimarika zaidi. Katika kipindi cha uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mamlaka ilishiriki katika mikutano na mawasiliano mbalimbali yaliyohusisha JPC na nchi saba (7) ambazo ni Uganda, Msumbiji, Malawi, Afrika ya Kusini, Oman, Irani, na Rwanda.

Tafiti za kisayansi na ushirikiano na taasisi nyingine.

Mamlaka imeendelea kushirikiana na taasisi nyingine katika kufanya tafiti mbalimbali katika masuala ya hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, ambapo katika kipindi cha miaaka miwili ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, jumla ya machapisho ya utafiti manne (4) yaliandaliwa na kuchapishwa katika majarida ya kimataifa ya sayansi. Wataalamu watano (5) kutoka Zanzibar walishiriki katika tafiti hizo. Tafiti hizi zimechangia katika kuboresha huduma zinanzotolewa na Mamlaka.

Mafanikio haya kwa kiasi kikubwa yamepatikana kutokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya kuipatia Mamlaka vitendea kazi muhimu ikiwemo Rada na vifaa vya hali ya hewa kupitia bajeti ya maendeleo, kupatiwa fedha za kufanikisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa na pia kupatiwa wafanyakazi wapya.

Mafanikio haya yameifanya TMA kuweza kutimiza majukumu yake ya utoaji wa huduma, uratibu na udhibiti wa shughuli za hali ya hewa nchini kama ilivyoelekezwa katika Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 na pia kutimiza jukumu muhimu la kuiwakilisha Nchi kimataifa kwenye masuala ya hali ya hewa.

Aidha, Mamlaka inatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kufuatilia na kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA kwa ajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya Taifa letu. Taarifa hizi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA ni rasmi, zimeboreshwa na zinakidhi viwango vya kimataifa.

By Jamhuri