EU yaridhishwa na utekelezaji miradi

Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA

Umoja wa Ulaya (EU) umeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi wa kilimo wa AGRI-CONNECT inaoufadhili.

Huu ni mradi ulioanzishwa mwaka 2020, unaolenga kusaidia kukuza kilimo katika mikoa sita ya Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo EU imetoa Euro milioni 100 sawa na zaidi ya Sh bilioni 250 za Tanzania.

Mradi huo unahusisha uboreshaji wa kilimo cha mazao ya chai, kahawa, mboga na matunda na umehusisha wadau mbalimbali kama Serikali ya Tanzania, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), wakulima, wasindikaji, wajasiriamali wadogo na wauzaji wa pembejeo.

Pia unahusisha uboreshaji wa miundombinu ya barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA), ili zipitike kwa urahisi wakati wote wakulima, wafanyabiashara, wasindikaji na wajasiriamali wafikishe bidhaa zao katika masoko kwa wakati na kuzuia upotevu na uharibifu wa mazao.

Akizungumza hivi karibuni jijini Mbeya baada ya ukaguzi wa miradi kadhaa uliofanywa kwa pamoja na maofisa wa EU, viongozi wa serikali, wawakilishi wa mashirika yasiyo kiserikali na wadau mbalimbali, Ofisa Ushirikiano wa Kimataifa wa EU kwa nchi za Afrika Mashariki, Anna Costantini, amesema kuwa wameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi wa AGRI-CONNECT katika maeneo mbalimbali waliyotembelea.

“Kwa kweli tumefurahishwa sana na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi, pamoja na kwamba wakati tunaanza tulikuwa na changamoto kubwa hasa katika kuwaunganisha wadau wote muhimu,” amesema na kuongeza:

“Lengo la kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao pia limeonyesha matokeo chanya katika maeneo yote tuliyotembelea na ni matumaini yetu kuwa mradi huu utakapofikia ukomo utakuwa umewanufaisha walengwa wote, hasa wanawake na vijana.”

Ofisa huyo wa EU amesema hali ya uzalishaji, lishe, upatikanaji wa masoko na elimu ya kilimo ni viashiria vya mafanikio ya mradi huo.

Mkurugenzi wa Mradi wa KIBOWAVI Daniel Kalimbiya

Anna anasema Tanzania ni moja wa washirika muhimu sana katika sekta ya uchumi na jamii na kuahidi kuwa umoja huo wa Ulaya utaendelea kushirikiana katika miradi mingine kama ya uboreshaji wa miji, mazingira na jinsia katika siku za usoni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la HELVETS-Tanzania ambalo ni mdau muhimu wa mradi huo, Daniel Kalimbiya, amesema mradi umefanikiwa kuwajengea uwezo wakulima katika mbinu bora za kilimo, kilimo cha kiekolojia, elimu ya lishe na upatikanaji wa fedha na kukidhi viwango vya ubora wa mazao.

HELVETAS-Tanzania ni NGO inayotekeleza mradi wa Kilimo Bora kwa Wanawake na Vijana (KIBOWAVI) katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Katavi wenye thamani ya Euro milioni 5, sawa na Sh bilioni 14.

“Na hii imesababisha kuongeza uzalishaji na tija kwa kulima kibiashara, kuongeza kipato, kuboresha afya zao na uunganishwaji wa masoko ya mazao yaliyozalishwa na yaliyoongezwa thamani,” anasema.

Mkurugenzi huyo anasema aidha mradi umewafikia zaidi ya kaya 21,300 (sawa na wanufaika zaidi ya 100,000) kupitia vikundi 650 vya wakulima wa mazao ya bustani katika mikoa tajwa na wengine nje ya mikoa husika.

Anasema pia mradi umefanikiwa kuongeza kipato kwa zaidi ya asilimia 40 kwa wakulima kwa ujumla, pia kupunguza kiwango cha upotevu wa mazao ya bustani baada ya kuvunwa kwa kuwajengea uwezo wazalishaji, kuhamasisha utumiaji wa teknolojia za uhifadhi, ukaushaji na utumiaji wa miundombinu ya viwanda vya kisasa vya kuchakata mazao ya bustani na utumiaji wa masoko ya kisasa na kupunguza upotevu wa mazao kwa asilimia 30.

“Mradi umejenga miundombinu ya masoko ya Rungwe, Busokelo, maghala ya kuhifadhi na kuuzia vitunguu na hiriki katika wilaya za Mbarali na Ileje, ujenzi wa viwanda vya usindikaji wa mazao ya bustani katika mikoa ya Mbeya na Katavi.

“Aidha, mradi umejenga vituo 11 vya mafunzo vya wakulima katika halmashauri 11 za mikoa ya Mbeya, Songwe na Katavi,” anasema mkurugenzi huyo.

Kalimbiya anaongeza kuwa mradi umefanikiwa kuwaunganisha wakulima na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa mboga, matunda na viungo na kuimarisha uhusiano wa kibiashara.

Wadau hao ni wauzaji wa pembejeo, wanunuzi, wauzaji wa zana za kilimo na umwagiliaji na wafanyabiashara wa mazao ndani na nje ya nchi.

“Pia elimu ya jinsi na jinsia imesaidia kujitambua kwa wanawake, vijana na wanaume kuweza kushiriki na kushirikishana kikamilifu katika shughuli za maendeleo, ikiwamo kupanga na kuamua katika kaya, kufanya kazi kwa pamoja bila kubagua kuwa hii ni kazi ya jinsia fulani na akina baba kuwaruhusu akina mama kushiriki shughuli za mradi kupitia vikundi, akina mama na vijana sasa wanajiamini na kujieleza mbele ya hadhara,” anasema.

Anahitimisha kuwa elimu hiyo ya jinsi na jinsia imesaidia kuimarisha uhusiano kati ya baba na mama, hivyo kuongeza amani na utulivu katika familia.