Na Lilian Lundo na Veronica Simba, JamhuriMedia

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tayari ameanza kazi ya kuunganisha umeme kwenye migodi midogo midogo wilayani Geita, ili kuwapunguzia gharama za kutumia mafuta ya Diesel wachimbaji wadogo.

Mhe. Dkt. Biteko amesema hayo leo wilayani Geita wakati wa hafla ya uwashaji umeme wa Vijiji vya Magenge na Kasesa vilivyopo Jimbo la Busanda, Wilaya Geita, mkoani Geita.

“Tunaleta umeme kwenye migodi midogo midogo, tunataka tupunguze gharama za uchimbaji madini kwa kutumia mafuta ya Diesel. Kiu yetu tuone umeme huu unachagiza maendeleo ya wakinamama, wakinababa na vijana katika vijiji,” amesema Mhe. Dkt. Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akikata utepe kama ishara ya kuwasha umeme katika kijiji cha Magenge mkoani Geita leo Octoba 1,
2023.

Ameendelea kusema kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona watu wanapata umeme na kufanya maendeleo. “Sisi tunaangalia wananchi walioko vijijini na miji midogo, wote waishi katika daraja moja,” amefafanua Dkt. Biteko.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigella amesema kuwa asilimia 80 ya vijiji vya Mkoa wa Geita tayari vina umeme, na kwa vijiji ambavyo havijapata umeme tayari Mkandarasi anaendelea na kazi ya kuunganisha umeme maeneo hayo.

Naye, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu amesema Mkoa wa Geita una jumla ya vijiji 461, ambapo vijiji 399 sawa na asilimia 86.6 vimepata huduma ya umeme kupitia miradi ya awali ikiwemo REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, REA Awamu ya Pili na REA Awamu ya Kwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela  akitoa maelezo ya awali kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati wa kuwasha umeme katika kijiji cha Kasesa mkoani Geita leo Octoba 1 , 2023.

“Katika Jimbo la Busanda jumla ya Vijiji 43 vitapatiwa Umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, ambapo Mkandarasi ameshawasha umeme katika vijiji 35, akiendelea na kazi katika vijiji 9 vilivyobaki vya jimbo la Busanda. Shilingi bilioni 10 zitatumika kutekeleza mradi huo,” amesema Mhandisi Olotu.

Katika Jimbo la Busanda, Wakala wa Nishati unatekeleza miradi mitatu ya umeme, ambayo ni Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mradi wa Kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo na Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akifurahia jambo na Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela na viongozi wengine mara baada ya kuwasha umeme katika kijiji cha Kasesa mkoani Geita leo Octoba 1, 2023.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizungumza na wananchi baada ya kuwasha umeme katika kijiji cha Magenge mkoani Geita leo Octoba 1, 2023.
Sehemu ya wananchi wakimsikiliza Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakati wa hafla fupi ya kuwasha umeme kijiji cha Magenge mkoani Geita leo Octoba 1, 2023.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akibonyeza kitufe kama ishara ya kuwasha umeme katika kijiji cha Magenge mkoani Geita leo Octoba 1, 2023.

By Jamhuri