Na Mwandishi Wetu

Mkojo wa mnyama mdogo anayefahamika kwa jina la sungura umegeuka almasi kwa wakulima wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Hii ni kutokana na uwezo wa mkojo huo kuzuia na kudhibiti wadudu waharibifu katika mazao ya chakula na biashara, ukitumika kama kiuatilifu.

Wakulima katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wanaolima mazao ya chakula na biashara sasa wamepata ahueni ya kuwasaidia kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao yao baada ya ugunduzi wa mkojo wa sungura.

Kwa mujibu wa Elisha Selemani, kijana mwenye umri wa miaka 30 na mkazi wa Mbalizi mkoani Mbeya ambaye ni mfugaji wa sungura, anasema mkojo wa mnyama huyo mdogo una madini (kemikali) ya ‘amonia’ ambayo harufu yake huwazuia wadudu waharibifu pale mazao yapoota.

Kijana huyo ni mmoja wa vijana na wanawake walionufaika na mradi wa Kilimo Bora kwa Wanawake na Vijana (KIBOWAVI) katika wilaya za mikoa ya Mbeya, Songwe na Katavi.

Mradi huo wa KIBOWAVI unafanyika kwa usimamizi wa shirika lisilo la kiserikali la Helvetas Tanzania chini ya programu ya AGRI – CONNECT umelenga kuendeleza ukuaji wa uchumi jumuishi na kuendeleza sekta binafsi na kuzalisha ajira katika mnyororo wa kuongeza thamani ya mazao ya mboga na matunda na kuongeza usalama wa chakula na lishe na ufugaji wa wayama wadogo wadogo katika mikoa hiyo.

Aidha, mradi huo umefadhiliwa kwa Euro milioni 5, sawa na zaidi ya Sh bilioni 14 za Tanzania kutoka Umoja wa Ulaya (EU).Mradi huu ulianza mwaka 2020 na unatarajiwa kumalizika mwaka 2024.

Sungura wa kufugwa wakiwa ndani ya banda la kisasa. PICHA|JAMHURI

Selemani ambaye ni mhitimu wa shahada ya kwanza katika fani ya utawala (Public Administration), anamiliki Kampuni ya Inoeli Poultry Farm inayojishughulisha na ufugaji wa wanyama wadogo wadogo kama sungura na ndege kama bata, kuku na kwale anaeleza kuwa wanatumia teknolojia rahisi kuvuna mkojo wa sungura na kinyesi chake ambacho hutumika kama mbolea ya samadi kwa ajili ya kilimo hai.

“Wateja wetu wakubwa ni wakulima wa mboga na matunda, ambao wamekuwa wakitupa oda nyingi na wakati mwingine kutokana na wingi wa wakulima tunapata changamoto ya kutosheleza soko,” anasema kijana huyo.

Anasema kuwa kutokana na mahitaji makubwa ya mkojo wa sungura wameamua kuwafundisha wafugaji wengine katika maeneo tofauti ambao huwauzia na wao hufanya usindikaji wake kwa kuweka mifuko maalumu (packaging) kisha kufikia masoko.

“Mkojo wa sungura kutokana na kufanya vizuri kama kiuatilifu, pia umesaidia kupunguza matumizi ya viuatilifu vyenye kemikali, ambayo matumizi yake yasipozingatiwa huleta madhara kwa watumiaji wa bidhaa, pia bei yake ni ghali tofauti na mkojo wa sungura ambao lita moja huuzwa Sh 2,000 tu,” anasema.

Kijana huyo anaongeza kusema kuwa kwa siku wanavuna lita tano za mkojo wa sungura kwa sungura zaidi ya 50 wanaowafuga.

“Faida nyingi tunayopata ni kuuza sungura kwa ajili ya kitoweo, ambapo sungura mmoja tunamuuza kwa bei ya kati ya Sh 20,000 hadi Sh 25,000 kutegemeana na mahitaji ya soko. Lakini pia tunajenga mabanda ya kisasa ya sungura,” anasema.

Mkulima mwingine, Agnes Ndeke, mkazi wa Utengule, Mbeya, anasema kuwa baada ya kuanza kutumia mkojo wa sungura ameona mabadiliko makubwa katika ukuaji na ubora wa mazao yake ya mboga na uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Natumia lita moja ya mkojo wa sungura na kuchanganya na lita mbili na nusu za maji kisha napiga kwenye mazao yoyote yakiwa bado machanga ili kuwazuia wadudu waharibifu na matokeo yake yameleta tija,” anasema Agnes ambaye ni mjane.

“Tunashukuru Shirika la Helvetas kwa kutuwezesha kupata elimu ya kilimo bora pamoja na kutuunganisha na masoko. Mradi huu umebadilisha maisha ya wanawake na vijana wengi sana na tumeachana na utegemezi,” anasema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mradi wa KIBOWAVI kutoka Shirika hilo la Helvetas, Daniel Kalimbiya, anasema kuwa lengo mahususi la mradi pia ni kuwajengea uwezo na mafunzo wakulima katika mbinu bora za uzalishaji wa mazao ya mboga na matunda pamoja na kilimo kinachozingatia mabadiliko ya hali ya hewa.

“Lakini pia kuwajengea uwezo wanachama wa vikundi vya uzalishaji katika mfumo wa kuweka na kukopa, kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika uzalishaji, uhifadhi baada ya mavuno, kuongeza thamani kwa usindikaji kwa kuzingatia fursa za biashara zilizopo,” anasema mkurugenzi huyo.

Kwa mujibu wa Kalimbiya, mradi wa KIBOWAVI unahudumia vikundi 600 na ulilenga kusaidia wakulima 75,000; kaya 15,000, watoa huduma ngazi ya jamii (CRPs), watoa huduma binafsi 100 (LSPs), wataalamu wa kilimo 100 wa ngazi ya vijiji/kata, wauzaji 50 wa pembejeo na wafanyabiashara vituo 11 vya kujifunzia, viwanda vitatu vya usindikaji na taasisi 50 za kuweka na kukopa.

     

By Jamhuri