Mwanamme mmoja mkazi wa Kidete mkoani Morogoro anayejishughulisha na kilimo,Piniston Nzali (20) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kujibu mashtaka matatu ya kuchapisha mtandaoni taarifa yenye kuharibu hadhi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Piniston pia antuhumiwa kwa kosa la kushindwa kusajili laini ya simu iliyokuwa ikimilikiwa na mtu mwingine.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali Sylivia mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Luboroga imedaiwa, Oktoba 8, 2022 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mshtakiwa alichapisha taarifa yenye kuharibu heshima au hadhi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Aidha, katika taarifa hiyo inadaiwa, mshtakiwa kupitia mtandao wa Tiktok alichapisha video inayomuonesha Rais Samia akiimba jambo ambalo halikuwa la kweli.

Mshtakiwa pia anadaiwa kuchapisha taarifa inayofanana na hiyo ikimuonesha Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiimba kosa alilolitenda Oktoba 10, 2022 huku akijua kuwa jambo hilo halina ukweli.

Katika shtaka la mwisho, inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Oktoba Mosi, 2022 na Oktoba 20, 2022 mshtakiwa alitumia laini ya simu ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na Benjamani Chaji bila kutoa taarifa ya mabadiliko ya umiliki kwa mtoa huduma.

Hata hivyo, mshtakiwa amekana mashtaka hayo na amerudishwa mahabusu mpaka kesho kesi hiyo itakapotajwa kwa ajili ya kueleza hatua za upelelezi ulipofikia