Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Ujumbe wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, (NHIF) umetembelea hospitali ya Regency ya Upanga jinjini Dar es Salaam na kuzungumza na uongozi ambapo wamekubaliana hospitali hiyo kuendelea kutoa huduma wakati masuala mengine yakishughulikiwa.

Ujumbe huo uliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga  aliyefika hospitalini hapo siku ya Jumamosi kuangalia namna huduma kwa wanachama wa NHIF zinavyoendelea hospitalini hapo. Akizungumza akiwa hospitali ya Regency mwishoni mwa wiki, Konga aliwoamba radhi wanachama  wa NHIF kwa usumbufu waliopata lakini aliwahakikishia kuwa wameshazungumza na uongozi wa  hospitali na wamewahakikishia kwamba huduma zitaendelea kama kawaida.

 “Nawaahidi wanachama wa NHIF kwamba baada ya mazungumzo yetu na Regency hakutakuwa na shida tena mtaendelea kuhudumiwa kama zamani kwasababu changamoto zilizokuwepo tunaendelea kuzungumza,” alisema Konga

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga wapili kutoka kushoto na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Regency, Lalit Kanabar  wakati Konga alipotembelea hospitali hiyo mwishoni mwa wiki kuangalia huduma za wanachama wa mfuko huo ambazo zinaendelea hospitalini hapo.

Baada ya mazungumzo hayo uongozi wa hospitali ya Regency kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Lalit Kanabar uliandika barua kwa NHIF kuhusu utayari wake wa kuendelea kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF.

“Tumekutana na uongozi wa NHIF tumezungumza na tumekubaliana huduma ziendelee wakati mambo mengine yanaendelea kujadiliwa na tumeshasaini mkataba na huduma kwa wanachama wa NHIF zilianza tangu siku ya Jumamosi,” alisema Kanabar

Naye Mtendaji Mkuu wa Regency, Lalit Kanabar aliomba radhi wanachama wa NHIF kwa changamoto waliyopata lakini aliahidi kuwa wanachama hao wataendelea kupata huduma bora kama kawaida kwenye hspitali hiyo.

“Huduma za wanachama wa  NHIF ziliendelea kutolewa hapa Regency tangu tarehe Moja Machi na zitaendelea kutolewa bila wasiwasi wowote na kama kuna changamoto zozote tutaendelea kuzitatua ila huduma zote wanachama watapata,” alisema.

Gazeti hili lilitembelea hospitali ya Regency jana Jumapili na kukuta huduma kwa wanachama wa NHIF zikiendelea kama kawaida hospitalini hapo.

Mmoja wa wagonjwa waliokuwa hospitalini hapo, Faraja John aliushukuru mfuko wa NHIF kwa kutembelea baadhi ya hospitali kuangalia namna huduma zinavyotolewa.

“Tulipata mshtuko kusikia kwamba huduma zitasitishwa lakini baada ya kuwaona NHIF kuja hapa na kutuhakikishia kwamba huduma zipo tunaona faraja kwamba sasa tutapata huduma bora kama mwanzo,” alisema

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga akizungumza na baadhi ya wanachama wa mfuko huo walipoenda kupata huduma kwenye hospitali ya Regency Upanga Dar es Salaam. Anayefuata ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Regency, Lalit Kanabar

Alisema wagonjwa wa NHIF waliofika kupata matibabu katika hospitali ya Regency wamepokelewa kama kawaida ingawa awali kulikuwa na tangazo la kuwakataa.

Mwanachama mwingine wa NHIF, Ibrahim Sanga, ambaye alikwenda kutibiwa kwenye hospitali hiyo alisema alipata huduma kama kawaida tofauti na habari za kwenye mitandao.

“Kwa kweli kulikuwa na taharuki wengi wetu tulikuwa hatujui tufanye nini lakini mimi nilikuja tu hapa kubahatisha lakini kumbe NHIF wamekuja na tayari wamezungumza na hospitali mambo yamekwenda vizuri na huduma zipo,” alisema

Machi 1, mwaka huu NHIF ilitangaza kuanza kwa matumizi ya kitita kipya hali ambayo ilisababisha mvutano kati yake na chama cha watoa huduma binafsi za afya APHFTA.

Siku ya Ijumaa (APHFTA), kilitangaza kwamba watoa huduma wote binafsi hawatatoa huduma kwa wagonjwa ambao ni wanachama wa NHIF hali iliyomlazimu Waziri wa Afya, Ummu Mwalimu kuingilia kati.

Ummy aliwataka wenye hospitali binafsi kuendelea kutoa huduma hizo wakati changamoto zingine na malalamiko yao yakiendelea kujadiliwa akisema kuwa milango ya majadiliano haijafungwa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Regency, Lalit Kanabar kulia akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Benard Konga aliyetembelea hospitali hiyo mwishoni mwa wiki kuangalia huduma za wanachama wa mfuko huo ambazo zinaendelea hospitalini hapo.

By Jamhuri