Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

MKUU wa operesheni kikosi cha usalama barabarani Tanzania ,Kamishina Msaidizi wa Polisi Nassoro Sisiwaya ametoa onyo kwa madereva pikipiki wanaopakia mishikaki ,kufanya mbwembwe barabarani na kuacha mara moja kupita katika makutano ya barabara bila kuchukua tahadhari.

Ameeleza ,asilimia 47 za ajali zinasababishwa na madereva (bodaboda) kwa kuvunja sheria kwa makusudi ikiwemo kupita katika makutano ya barabara bila kuchukua tahadhari.

Akiwa Bagamoyo ,wakati wa zoezi la ukaguzi wa magari linalofanyika kwa madereva wa vyombo vya moto nchini ,Sisiwaya aliwataka pia, madereva wa mabasi makubwa na madogo wanaosafirisha abiria kutii sheria za usalama barabarani pasipo kushurutishwa.

Alieleza, wamejipanga kuwachukulia hatua kali za kisheria sanjali na kuwafikisha Mahakamani madereva watakaobainika kukiuka sheria za usalama barabarani.

Sisiwaya alieleza kuwa, katika kipindi hiki cha mvua madereva wa vyombo vya moto wanapaswa kuongeza umakini kutokana na uwepo wa ukungu, kuteleza kwa barabara na baadhi ya maeneo katika barabara kukatika au kuwepo na mashimo.

“Nipende kuwaasa madereva kutambua kipindi hiki tulichonacho cha mvua kuchukua tahadhari kubwa ili kuepusha kutokea kwa ajali zinazotokana na makosa ya kibinaadamu”.

Vilevile amefafanua, zoezi hili ni endelevu kwa nchi nzima la ukaguzi kwa madereva na akiwa Bagamoyo mkoani Pwani wameweza kupima ulevi kwa madereva wa mabasi makubwa na madogo yanayofanya shughuli za kusafirisha abiria, malori ya mizigo pamoja na magari madogo.

Nae dereva wa mabasi makubwa ya abiria, Hamisi Juma alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendesha zoezi la kupima ulevi madereva na kutanabaisha kuwa wapo ambao huendesha vyombo hivyo wakiwa wametumia vileo.

Aliliomba, Jeshi hilo kuwachukulia hatua za kisheria madereva watakaobainika kutumia vileo kwani ni chanzo cha ajali zembe.

Kadhalika, Serikali kurudisha vidhibiti mwendo kwenye mabasi ya abiria ili kuweza kupambana na ajali za mara kwa mara badala ya kutumia VTS pekee kama ilivyo sasa.

By Jamhuri