Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Bagamoyo

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani Aboubakary Mlawa, amechangia matofali 1,000 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Jumuiya hiyo Kata ya Zinga.

Hatua hiyo ni mkakati wa jumuiya hiyo ,kuhakikisha kila tawi na kata zinakuwa na ofisi ili kuondoka na changamoto ya kupanga ofisi .

Akichangia matofali hayo, Mlawa alieleza kuwa, ni wakati wa Jumuiya kuwa na ofisi ili kusogeza huduma za karibu kwa wanachama wao ,na Kuwa na sehemu za kufanya vikao.

“Huu ni mkakati na mpango kazi kuanzia ngazi ya chini ,niliwaasa wote waanze juhudi za kujenga ofisi, kutokana na jitihada mlizozionyesha, nawachangia tofali 1,000 zitazosaidia kujenga ofisi yetu ya kata, kwa pamoja tushirikiane tuweze kufanikisha ujenzi huu” alieleza Mlawa.

Awali Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo,Kata ya Zinga, Hashimu Mambo alieleza utekelezaji wa mpango kazi wa miaka mitano, ulianza kwa kuingiza wanachama wapya, pamoja hayo wamejipanga kuanzisha miradi ili kujiinua kiuchumi.

“Jengo letu linahitaji tofali elfu tatu, kwa sasa tuna tofali 800, saruji mifuko 10 na fedha ya fundi laki nne, mchanga lori mbili na kwa sasa tunahitaji vifaa mbalimbali vitavyofanikisha ujenzi wetu,” amesema.

By Jamhuri