Watoto sita wa kuanzia miezi saba na mtu mzima mmoja wamekufa baada ya kula samaki aina ya kasa anayesadikiwa kuwa na sumu.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kaimu Kamanda wa Polisi,Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Canute Msacky, tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Bweni wilayani Mafia mkoani Pwani.

Kamanda Msacky amesema kuwa watu hao akiwemo mtu mmoja mzima walipoteza maisha kwa nyakati tofauti tofauti kuanzia Machi 12, mwaka huu.

“Watu hao wanatoka katika kaya nne tofauti na walifariki kwa nyakati tofauti baada ya kula samaki ambapo kati yao watoto ni sita na mtu mzima mmoja,” amesema.

Amewataja waliokufa ni Ally Seleman (miezi nane), Ramadhan Karimu (miezi nane),Mohamed Makame (miezi saba), Minza Hatibu (miezi kumi), Abdala Nyikombo (miaka 4), Makame Nyikombo (miaka tisa) na Salima Mjohi (miaka 28).

Hata hivyo amesema kuwa tayari miili ya marehemu yote imeshafanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Mafia na imekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu zingine za mazishi.

Jeshi la Polisi Mafia limetoa wito kwa wavuvi kuacha tabia ya kuvua samaki aina hiyo ya kasa ambao ni nyara za Serikali hivyo atakayekamatwa na kasa hatua za kisheria zitachukuliwa.

By Jamhuri