Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMediaPwani

Mkoa wa Pwani, umefikia asilimia 94.6 ya upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba ,hadi kufikia Machi mwaka huu, hatua ambayo ni nzuri inayokwenda kujibu changamoto ya upungufu wa dawa kwenye hospital, zahanati na vituo vya afya.

Rai yatolewa kwa viongozi na watendaji wa afya kusimamia kikamilifu bidhaa za afya na dawa ,ikiwemo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya kutolea huduma ili kupunguza mianya ya upotevu na wizi wa vifaa ,dawa na changamoto zinazotokana na usimamizi mbovu .

Akifungua mafunzo ya siku tatu ya mfumo wa mshitiri kwa waganga wakuu wa Halmashauri,maafisa ugavi, wakurugenzi wa Halmashauri Tisa za Mkoa wa Pwani ,mafunzo ambayo yameandaliwa na TAMISEMI na kufanyika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo,Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Zuwena Omari amehimiza usimamizi wa vifaa hivyo sanjali na mapato.

Amewaasa kila mmoja kwa nafasi yake kutimiza wajibu wake na kuhakikisha anatekeleza mfumo huo ili ulete matokeo chanya.

“Kwa mujibu wa kifungu 140(5)Cha kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016 imeeleza endapo bohari ya dawa MSD hatokuwa na dawa na vifaa tiba zilizyopo kwenye kinadi itatakiwa kutoa notisi ya bidhaa zilizokosekana ndani ya siku moja ya kazi tangu kupokea maombi.

“Kutokana na changamoto na kuibuka kwa hoja mbalimbali za ununuzi wa bidhaa za afya vituoni OR-TAMISEMI ilitoa waraka na moja wa mwaka 2018 ambao ulielekeza matumizi ya washitiri teule wa mikoa katika ununuzi wa bidhaa za afya pale vituo vinapokosa bidhaa hizo bohari ya dawa MSD”amefafanua Zuwena.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Dkt. Gunini Kamba ameeleza, mfumo huo unawezesha upatikanaji wa bidhaa za afya zinazokuwa zimekosekana bohari ya dawa hivyo kuimarisha na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa za afya.

“Hadi sasa tupo katika asilimia 94.6 ya upatikanaji wa dawa muhimu ,matarajio kufikia asilimia 100 tutapata dawa na huduma za bidhaa za afya bila manung’uniko kwa jamii”ameeleza Gunini.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaombele sekta ya afya ,na nyanja nyingine kubwa sekta ya afya kwa kuongeza wigo wa upatikanaji wa dawa ,vifaa tiba na ujenzi wa miundombinu ya majengo ya hospital za wilaya,vituo vya afya na ongezeko la bajeti ya sekta hii”ameeleza Gunini.

Mfamasia kutoka TAMISEMI Elihaki Javan ambae pia ni mwezeshaji wa kitaifa wa usambazaji wa mfumo wa mshitiri alieleza ,mafunzo wanatoa mafunzo hayo katika mikoa yote nchini ndani ya mwezi mmoja .

“Nia kufundisha watendaji wa Halmashauri wakiwemo waganga wakuu,maafisa ugavi , wakurugenzi kupata uwezo wa pamoja kutoa elimu kwenye vituo , Zahanati na hospital Kuwa na taarifa za mshitiri na taarifa sahihi kutoka mfumo wa kawaida wa makaratasi Hadi kielektroniki”ameeleza Javan.

By Jamhuri